Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ndaisaba George Ruhoro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Primary Question

MHE. NDAISABA G. RUHORO K.n.y. MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza:- Je, nini mpango wa Serikali katika kunusuru uchumi wa nchi kutokana na ukosefu wa fedha za kigeni, hususani Dola ya Kimarekani?

Supplementary Question 1

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; kwa kuwa kuna Wakandarasi wengi wamesaini mikataba na Serikali hasa mikataba ya ujenzi; na kwa kuwa Mikataba hiyo imeathiriwa sana na mabadiliko makubwa ya viwango vya kubadilisha fedha za kigeni hasa dola za Kimarekani. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia Wakandarasi hawa ili wasishindwe kutekeleza miradi hiyo hasa miradi ya ujenzi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa mabadiliko ya viwango vya kubadilishia fedha za kigeni kabla hatujapitisha bajeti ya nchi ilikuwa shilingi 2,350, hiyo ni dola ya Kimarekani na sasa ni shilingi 2,500 hadi shilingi 2,600 na mabadiliko haya yameathiri bajeti ya nchi tuliyoipitisha hapa Bungeni hasa kwenye maeneo ambapo Serikali inahitaji kununua bidhaa nje ya nchi.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuinusuru bajeti yetu tuliyoipitisha hapa Bungeni ili iweze kutekelezeka vizuri? Ahsante sana. (Makofi)

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa maswali mazuri aliyouliza Mheshimiwa Ndaisaba; kuhusu swali la kwanza ambalo linahusisha Wakandarasi ambao watakuwa wameathirika na mabadiliko ya bei za kubadilishia fedha huku Mikataba yao ikiwa imeshasainiwa, nimwombe Mheshimiwa Mbunge na niwaombe Wakandarasi wa aina hiyo kufanya engagement, kufanya mashauriano na sekta zinazohusika kwa sababu masuala ya kimkataba ni ya sekta kwa sekta ili jambo hili liweze kusogelewa kwa umahususi wake katika eneo husika.

Mheshimiwa Spika, tunazo taarifa katika baadhi ya miradi ambako tayari walishafanya mashauriano ya aina hiyo kutokana na mabadiliko haya ambayo yalikuwa yanajitokeza ya kiuchumi. Kwa hiyo hata hawa ambao watakuwa wamekumbwa na jambo hilo, ni vizuri kufanya majadiliano katika maeneo husika.

Mheshimiwa Spika, kuhusu jambo la pili la kunusuru bajeti, Serikali inachukua hatua ambapo mpaka hivi sasa tumefanya utaratibu wa kuona namna ambavyo tunaweza tukabana matumizi ya ndani ya Serikali hasa katika maeneo ya matumizi ya kawaida ili kuweza kutoa fursa miradi ya wananchi isiathirike. Hilo ndiyo lilikuwa agizo la Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba, tunafanya utaratibu wa kuangalia matumizi ambayo siyo ya lazima ili fedha ambayo inapatikana iweze kutekeleza miradi ya maendeleo ili bajeti ya miradi ya maendeleo isiathirike.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ameendelea kutuongoza katika baadhi ya maeneo kuweza kuhakikisha kwamba tunapata fedha nyingi za kigeni ili ziweze kupunguza tatizo la uhaba wa dola ndani ya nchi na kuruhusu uhimilivu ama ustahimilivu, uimara wa bei ya kubadilishia fedha na uimara wa shilingi yetu ya Tanzania. (Makofi)