Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Primary Question

MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:- Katika eneo la Ndolezi Wilaya ya Mbozi kuna kimondo ambacho ni cha aina yake katika nchi hii na dunia kwa ujumla:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuhamasisha watalii wa ndani na nje ya nchi kuja kukiangalia Kimondo hicho ili kuchangia pato la taifa?

Supplementary Question 1

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Pamoja na majibu haya ambayo ameyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mazingira ya kimondo chenyewe yako kwenye hali mbaya sana, na ukiangalia miundombinu na barabara zinazoenda kule ziko kwenye hali mbaya sana, hivi sasa hivi kimondo kile hata uzio wa kukizunguka kimondo kile ku-protect haupo. Sasa je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha mazingira ya kimondo kile ili kiwe ni kivutio kizuri sana kwa utalii pamoja na kuinua pato la Mkoa mpya wa Songwe na Jimbo langu la Vwawa?
Mheshimiwa MWenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi ilishaandika barua ya kuomba Wizara hii ikikabidhi kimondo kwenye Halmashauri ili waweze kukiendeleza na kuweka vivutio mbalimbali ikiwa ni pamoja na migahawa, hoteli na vitu mbali mbali vitakavyowavutia watalii wa ndani na nje, Serikali ni lini sasa itakubali kukikabidhi kimondo hicho katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI, MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kutoka kwa Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga Mbunge wa Vwawa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza linahusu changamoto ya miundombinu kutokuwa bora au kutokuwa rafiki kwa shughuli za utalii kwenye eneo hili ambako kimondo chetu kipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua wazi kwamba ili kuweza kuboresha utalii miongoni mwa maeneo ambayo yanatakiwa kutiliwa mkazo, na kwakweli yanatiliwa mkazo na Serikali, ni pamoja na kuboresha miundombinu kwenye maeneo yenye vivutio kama hili la kwenye kimondo cha pale Mbozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango ya Serikali ambayo ametaka kuifahamu Mheshimiwa Mbunge ni kuboresha miundombinu hiyo kwa kutumia bajeti zake lakini pia kwa kushirikisha wadau. Kwa hiyo wakati Serikali inaendelea na utaratibu wa kutumia fedha zake za bajeti kuboresha miundombinu bado mheshimiwa Mbunge kwa kuungana na Serikali aweze kutafuta namna ambayo anaweza kushirikiana na Serikali kuweza kuwafikiwa wadau mbalimbali kwenye eno la Mbozi ikiwa wanaweza kufanya jitihada kuungana na Serikali katika kuboresha miundombinu kama alivyoitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na kimondo kukabidhiwa kwa Halmashauri, suala hili haina tofauti kubwa sana kiuendeshaji, Serikali ni ile ile, Halmashauri bado ni Serikali na Serikali kuu bado ni Serikali. Mawazo mema na mazuri yanaweza kupokelewa kulingana na ubora wake na wakati. Kwa hiyo nimshauri mheshimiwa Mbunge ashirikiane na Halmashauri na washauri waweze kutuandikia Wizarani tutaweza kupima kuona ikiwa sababu hizo za kukabidhi kimondo hicho kwa Halmashauri linaweza likafanya eneo hilo likafanyika utalii kwa namna bora zaid na kwa tija zaidi kuliko ilivyo sasa.