Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Judith Salvio Kapinga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JUDITH S. KAPINGA K.n.y. MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza: - Je, lini Serikali itaboresha Mitaala ya Elimu ili mafunzo ya biashara yatolewe kuanzia shule za Msingi?

Supplementary Question 1

MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa dunia ya sasa ipo katika mapinduzi ya nne ya viwanda kuelekea mapinduzi ya tano ya viwanda. Je, mitaala inayoboreshwa itaendana na kasi hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; programu ya mageuzi ya kiuchumi ambayo imepelekea kuanzishwa kwa takribani programu 300 kwenye vyuo vikuu. Je, ni lini programu hizi zitahuishwa na kuanza kufundishwa? (Makofi)

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kapinga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokwishaeleza kwenye majibu ya swali la msingi kwamba, sasa tuko katika hatua za mwisho za uboreshaji wa mitaala hii. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika swali lake la kwanza anazungumza kuhusiana na suala la mitaala namna gani litaweza ku-cope na mapinduzi ya viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, mitaala inayoboreshwa inalenga kumpatia mhitimu maarifa, study pamoja na ujuzi utakaomwezesha kukabiliana na mabadiliko ya kisayansi, teknolojia na kiuchumi kwa ujumla. Mitaala hii imesisitiza sana masomo ya TEHAMA pamoja na kompyuta ambayo, tutaanzia katika ngazi ya elimu ya msingi na kwenda katika ngazi zote. Lengo kuu la kufanya maboresho haya ni kujiandaa na mapinduzi haya ya nne pamoja na ya tano ya viwanda ambayo yanahusisha matumizi ya teknolojia pamoja na kompyuta kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili anaulizia kuhusiana na tunaanza lini? Mradi huu wa Higher Education for Economic Transformation ni mradi wa miaka mitano na utekelezaji wake ulianza tokea mwaka 2021/2022 na tunatarajia kukamilisha 2025/2026. Kwa hiyo, kazi hii imeshaanza, wataalam wetu wameshapata mafunzo kwa ajili ya uboreshaji wa mitaala pamoja na programu hizi. Kazi hii inaendelea na kwa vile ni kazi ya miaka mitano, tutakuwa tunaendelea kuifanya mpaka kipindi hicho chote kitakapokuwa kimekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.