Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Primary Question

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza:- Je, kwa nini Serikali isipitishe mkakati maalum kwenye bajeti ya mwaka 2022/2023 wa kujenga shule za msingi kwenye vitongoji vyote vyenye watoto zaidi ya 200?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, nimepokea wito wa Serikali kwamba tuendelee kushirikiana na wananchi kujenga shule; na kwa kuwa mwaka jana tulileta maombi ya kujengewa/kumaliziwa shule 58 za shikizi tukapata shule kumi tu kati ya 58 bado shule 48 zimeongezeka sasa hivi ziko 55.

Je, Serikali itatupatia lini fedha kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa shule hizo shikizi 55 ambazo zipo sasa hivi? Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, usajili wa shule za msingi na usajili wa shule za sekondari hufanywa kwa mikondo, mkondo mmoja wa shule za msingi una watoto 45 na mkondo mmoja wa shule za sekondari nadhani una watoto 40. Sasa maana yake ni kwamba shule yenye mikondo minne inatakiwa iwe na wanafunzi kwenye darasa moja wanafunzi 180 katika shule ambazo zimeshazidi idadi ya wanafunzi wanaohitajika kwenye mikondo. Kwa nini Serikali isiwe na mkakati maalum wa kitaifa wa kujenga shule mpya karibu na maeneo ambayo shule zimezidi idadi?

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mbunge kwamba moja ya mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kwamba tunamalizia shule shikizi zote na kwa awamu ya kwanza katika mwaka wa fedha huu hapa ambao tupo, Mheshimiwa Rais alitoa fedha na tukajenga madarasa 3000 nchi nzima kwenye maeneo ya shule shikizi.

Kwa hiyo, hizo shule kumi ambazo tulileta katika maeneo yako, na sasa hivi tuna mipango mingine ambayo tuna fedha, na baadhi ya fedha tutazielekeza katika maeneo ambayo bado yanaupungufu na yana mahitaji hususani katika shule shikizi, kwa hiyo, katika kipaumbele tutakachotoa ni pamoja na hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwamba tunatapisha shule zote ambazo zina wanafunzi wengi na ikiwemo kusajili katika maeneo ambayo sasa idadi ya wanafunzi ni kubwa hususani katika hizi shule shikizi ambazo zimezidi.

Kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa Mbunge haya yote yapo katika mpango wa Serikali na tunaendelea kuyatekeleza na mfano mzuri katika mwaka huu wa fedha na katika bajeti ambayo tumeipitisha hapa ya mwaka 2022/ 2023.