Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Primary Question

MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza: - Je, Serikali haioni ni kuwakandamiza Wananchi wa Itigi kwa kuondoa Miji kwenye bei ya kuweka umeme kutoka shilingi 27,000 hadi shilingi 320,000?

Supplementary Question 1

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu haya marefu ya Serikali na historia ambayo hapa haitusaidii sana, dhamira ya Serikali pamoja na kujenga Bwawa la Mwalimu Nyerere pamoja na kuweka mahela kwenye mafuta ya petroli ambao watumiaji wa petroli wala hawahusiki na umeme huu vijijini.

Je, ni lini sasa Serikali itaangalia namna iliyo bora ya kupatana na wananchi ambao wanahitaji kuweka umeme kama wanashindwa kupunguza bei ili wapatane naye basi alipe sehemu ya gharama na gharama nyingine azilipe polepole kulingana na makubaliano watakayokubaliana, Serikali iko tayari kufanya jambo hili?

Mheshimiwa Spika, pili, kulikuwa na bei wakati huo Mheshimiwa hapa amejibu amesema ilikuwa shilingi 177,000 na shilingi 27,000 huko vijijini kabisa, vijiji miji ambayo kama Itigi ambao wameiondoa sasa katika ile laki moja na sabini saba kuja laki tatu ishirini. Je, Serikali iko tayari kurudisha vile vijiji miji ambavyo kutokana tu kupimwa eti tayari ni mji! Je, wako tayari sasa kuturejeshea katika ile bei ya shilingi 177,000?

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Yahaya Massare, Mbunge wa Manyoni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kulipa gharama za kuunganishwa umeme awamu kwa awamu au taratibu, tumeshaanza kuufanyia mkakati na majadiliano yanaendelea kuona namna bora ya kuweza kufikia azma hiyo. Changamoto kubwa ni kwamba gharama za bidhaa zinabadilika mara kwa mara, kwa hiyo mtu akilipa kidogo kidogo kwa muda ambao tutakuwa tumekubaliana, akamalize ndani ya muda huo labda pengine itatusaidia, lakini akichukuwa muda mrefu na pengine kushindwa kumaliza ndani ya ule muda tuliokubaliana, tutajikuta huduma hii inakuwa ni changamoto kwa kuitekeleza.

Mheshimiwa Spika, tayari wataalam wetu wa TANESCO wanaendelea kuangalia namna bora ya kuweza kupunguza hizi gharama za kuunganisha umeme kwa awamu moja kwa wateja wetu ili kuweza kufika azma ya kuwaunganishia wananchi wote umeme, lakini hasa kwenye maeneo ya mijini kwa sababu gharama za vijiji tayari zimepunguzwa.

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la pili, wenzetu wa TANESCO walishirikiana na wenzetu wa TAMISEMI kubaini na maeneo gani ya miji na ni maeneo gani ya vijiji na gharama ya vijijini ikabaki kuwa shilingi 27,000 na gharama za mijini zikasemwa hizi gharama nyingine ambazo tayari Serikali imeweka ruzuku ndani yake. Hata hivyo, Serikali ya Awamu ya Sita ni sikivu kwa wananchi itaendelea kufanya kazi kuendelea kuona namna ambayo inaweza ikawafikishia huduma bora Watanzania hata kwa kufanya majadiliano mengine ya kuona maeneo gani ipeleke kwa gharama gani kwa ajili ya kufikisha azma ya wananchi wote kupata umeme.

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na napenda niongezee kidogo kwamba ni dhahiri kwamba yapo maeneo ya miji, kwanza tafsiri yetu ya miji na vijiji inatokana na sheria ya TAMISEMI, lakini dhahiri kwamba yako maeneo ya miji na majiji manispaa ambayo yako pembezoni yana sifa zote za maeneo ya vijijini.

Mheshimiwa Spika, kwa bahati nzuri tumebaini maeneo hayo na tumekubaliana na maombi ya Waheshimiwa Wabunge wengi pamoja na kwamba maeneo hayo yapo kwenye mipaka na miji na majiji lakini ukienda ukiona ni dhahiri kabisa kwamba yana sifa za maeneo ya vijiji kwa maana ya mazingira na hali ya kipato.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo katika bajeti ya Wizara ya Nishati tutatoa maelezo na utaratibu wa kuzingatia uhalisia wa maeneo haya katika kupanga bei ya kuunganisha. Ahsante. (Makofi)