Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Primary Question

MHE. ATHUMANI A. MAIGE aliuliza: - Je, ni lini Serikali itabadilisha mtambo wa kutengeneza hewa ya Naitrojeni Kituo cha Afya Upuge na kuleta mtambo wa hewa ya Oksijeni?

Supplementary Question 1

MHE. ATHUMANI A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu niulize swali la nyongeza. Katika kituo hicho pia kuna mtambo mkubwa wa kufua nguo ambao screen yake au kisomeo kiliharibika wakati mtambo unapelekwa kwenye site: Je, Serikali iko tayari kuleta spare nyingine ili kituo kile kiweze kufanya kazi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; katika kituo kile pia kuna mtambo mkubwa wa X-Ray ambao haufanyi kazi kwa sababu hakuna jengo la kufunga mtambo ule: Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kusafiri na mimi kwenda huko Upuge ili tukaone ufumbuzi wa kupata jengo jipya la kufunga mionzi? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Athuman Almas Maige, Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mtambo wa kufua nguo ambao umeharibika naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tutafanya tathmini ya mahitaji kwa maana ya gharama, lakini tutaona kati ya fedha ya mapato ya ndani na kutoka Serikali Kuu ipi inaweza ikatumika kuhakikisha mtambo huo unafanya kazi au tunanunua mtambo mwingine.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na Jengo la X-Ray, kwamba X-Ray ipo lakini hakuna jengo, naomba tulichukue suala hili tukalitazame. Pia nitoe wito kwa Halmashauri ya Tabora kuanza kuona uwezekano wa kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya kujenga jengo la X-Ray, kwa sababu tayari kuna mtambo na wana mapato ya ndani, wanaweza wakatenga kwa awamu kujenga jengo hilo ili tuweze kutoa huduma hiyo.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge tukapitie eneo hilo. Ahsante.