Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. David Mathayo David

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Same Magharibi

Primary Question

MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatoa vibali vya kuajiri Walimu wa kutosha kukabiliana na ongezeko la Wanafunzi na Wahitimu wangapi wapo kwenye soko la ajira?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri zetu nchini zina mazingira tofauti. Kuna Halmashauri ambazo zina mazingira magumu sana kiasi ambacho walimu wanapoajiriwa wanaripoti halafu wanaenda kutafuta sababu za kuhama kwenda kwenye maeneo mengine kwa kutoa hata sababu za kusema wanaumwa ili waende maeneo ya mjini.

Mheshimiwa Spika, Je, Serikali inatoa motisha gani kwa walimu ambao wapo kwenye mazingira magumu kwa sababu watoto wetu wanapomaliza Kidato cha Nne na Darasa la Saba wanapata mitihani sawa na wale ambao wana walimu wa kutosha sasa tutaendelea kuwa na watoto ambao hawafaulu, wanafeli kwa sababu walimu wanakimbia mazingira magumu, tunaomba Serikali itueleze inandaa mazingira gani mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili Utumishi inachelewa kutoa vibali vya kuajiri walimu na hasa walimu wanapokuwa wamestaafu ama wanapofariki ama wanapoacha kazi kutokana na sababu mbalimbali. Je, ni lini Serikali italeta sheria ibadilishwe au Muswada tutengeneze sheria kwamba TAMISEMI iruhusiwe kuajiri walimu wa kuziba mapengo moja kwa moja badala ya kuomba vibali Utumishi kwa ajili ya kuziba mapengo ya walimu ili kuweza kuokoa elimu katika nchi yetu. Ahsante. (Makofi)

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. David Mathayo Mbunge wa Same Magharibi.

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nichukue nafasi hii kutoa pongezi zangu za dhati kabisa kwake yeye Mheshimiwa Mbunge Dkt. David Mathayo wa Same Magharibi kwa maana amekuwa akifuatilia sana maslahi ya Watumishi wa Umma hasa wale wa Jimboni kwake Same Magharibi.

Mheshimiwa Spika, sasa nikienda kwenye swali lake la kwanza la motisha kwa Watumishi wa Umma hasa walimu wale waliopo pembezoni. Serikali imekuwa ikiweka kipaumbele sana cha kuona ni namna gani bora ya kuweza kutoa motisha kwa watumishi wanaoenda pembezoni kutoa huduma kwa Watanzania. Ndiyo maana hata jana nikiliarifu Bunge lako hili tukufu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ametoa maelekezo pale ofisini kwetu kwa watumishi housing cooperation kuweza kuhakikisha kwamba wanajenga nyumba pembezoni ambazo ni affordable kwa ajili ya watumishi hawa waweze kuweza kupata nyumba kwa gharama nafuu katika maeneo wanayofanyakazi lakini vilevile waweze kulipia kupitia mshahara wao.

Mheshimiwa Spika, ukiacha hilo huwa tunawaasa sana na kuwataka waajiri yaani halmashauri zetu nchini kuhakikisha wanatenga bajeti katika mapato yao ya kuweza kutoa motisha kwa watumishi hawa, hasa wale wapya ambao wanaenda kuripoti. Kuna baadhi ya Halmashauri nchini ambazo zimefanya hivyo wale wanaoripoti kazini wanapewa magodoro, wanapewa baiskeli na vifaa vingine vya kuweza kuwaongezea motisha ya kazi pale wanaporipoti.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili kuhusu ajira mbadala. Tatizo si Ofisi ya Rais, Utumishi. Tatizo linakuwa kwa ajili wenyewe kuto-focus mbele kujua wangapi wanastaafu katika kipindi cha mwaka wa fedha fulani, wangapi ambao wamefariki katika kipindi cha mwaka wa fedha fulani ili waweze kuomba vibali vile vya ajira mbadala kwa wakati. Kwa hiyo, unakuta mara nyingi wanasubiri mwaka wa fedha unapita wanasema kwamba ni utumishi iliyokwamisha vibali vile lakini unakuta hawavi-compile kwa wakati kuvipeleka TAMISEMI ili nao TAMISEMI waweze kuvileta katika Ofisi ya Rais, Utumishi kuweza kuvitoa.

Mheshimiwa Spika, mara nyingi Ofisi ya Rais, Utumishi tunapopata maombi ya vibali vya ajira mbadala huwa Katibu Mkuu anavitoa palepale kwa sababu tayari mshahara wao upo, bajeti yao ipo lakini tunahitaji tupate maombi yale kwa wakati.

Name

Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Primary Question

MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatoa vibali vya kuajiri Walimu wa kutosha kukabiliana na ongezeko la Wanafunzi na Wahitimu wangapi wapo kwenye soko la ajira?

Supplementary Question 2

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Tunaishukuru Serikali kwa kibali cha ajira ya zaidi ya nafasi 30,000. Katika nafasi zilizotangazwa hatuna kada ya Watendaji wa Vijiji na Kata.

Je, Serikali ni lini itatoa kibali cha ajira kwa Watendaji wa Kata na Vijiji?

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zacharia kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ipo mbioni kuwaajiri Watendaji wa Vijiji na Watendaji wa Kata na muda si mrefu tayari tutaanza kuweza kuwa-post wale Watendaji wa Kata kwenye maeneo yenu lakini vilevile bado tena narudia rai yangu kwa waajiri ku- compile orodha ya mahitaji yao kwenye Watendaji wa Vijiji, Mitaa na Kata na kuiwasilisha TAMISEMI kwa wakati ili waweze kuileta Utumishi ili pale zoezi hili la kuajiri hawa linapoanza basi tuweze kufidia maeneo yote ambayo yanauhitaji wa watendaji hao.

Name

Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatoa vibali vya kuajiri Walimu wa kutosha kukabiliana na ongezeko la Wanafunzi na Wahitimu wangapi wapo kwenye soko la ajira?

Supplementary Question 3

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, tunashukuru sana kwamba kuna ajira ya walimu imetokea lakini kumekuwa na changamoto sana kwa ndoa za walimu wengi, kwa sababu walimu wanaajiriwa mbali na familia zao na wanapoomba uhamisho baada ya miaka mitatu bado Serikali imekuwa inaleta ugumu wa kuwakutanisha kukaa kama familia.

Serikali inampango gani ya kuwasaidia walimu hao ili ndoa zao zipate kudumu na kuendelea na maisha ya kawaida. (Makofi)

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwakagenda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hivi sasa Serikali ipo katika kufanya HR audit kuweza kufahamu mahitaji ya watumishi ni wapi wa kada fulani wapo wangapi ili kuweza kuja kurahisisha hili analolisema Mheshimiwa Mwakagenda kwamba pale wanapoomba uhamisho kuweza kwenda kujiunga na wenza wao ili kuweza kuona na uhitaji na nafasi iliyopo, kwa sababu kwa sasa ni lazima kuwe na nafasi ambayo iko wazi kule anapotaka kwenda. Lazima kuwe na hiyo vacancy ili kibali kiweze kutoka cha uhamisho. Kwa hiyo, tukishamaliza HR audit tutajua wapi kuna mahitaji gani, wapi kuna mahitaji gani.

Mheshimiwa Spika, nimalizie tu kulijibu hili kwa kusema mara nyingi wenza hawa wapo Mijini kwenye Majiji na Manispaa hawapo pembezoni, kwa hiyo ndiyo maana tunafanya HR audit kuweza kuona ule uhitaji kwa ujumla ili vibali viweze kuwa vinatolewa kwa urahisi wa wenza waweze kuwafuata wenza wao.

Name

Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Primary Question

MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatoa vibali vya kuajiri Walimu wa kutosha kukabiliana na ongezeko la Wanafunzi na Wahitimu wangapi wapo kwenye soko la ajira?

Supplementary Question 4

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru pamoja na changamoto ya upungufu wa watumishi nchi nzima, lakini maeneo ya pembezoni ikiwemo Wilaya ya Nkasi ina upungufu wa watumishi 1,939. Je, Serikali inampango gani wa haraka wa kusaidia maeneo ya pembezoni ikiwemo Wilaya ya Nkasi?

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Nkasi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutoa kipaumbele cha ajira hasa kule pembezoni ambako kuna upungufu wa watumishi, lakini kama unavyofahamu Serikali inaajiri kulingana na uwezo wa bajeti.

Kwa hiyo, kadri tutakavyozidi kukusanya na bajeti yetu kuruhusu ndiyo tutakapozidi vilevile kuajiri watumishi wa kuweza kwenda kuwahudumia Watanzania hasa wale waliokuwa maeneo ya pembezoni.