Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Simai Hassan Sadiki

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nungwi

Primary Question

MHE. HASSAN SADIKI SIMAI aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza malalamiko ya muda mrefu ya ucheleweshwaji wa fedha za Mfuko wa Maendeleo wa Jimbo upande wa Tanzania Zanzibar?

Supplementary Question 1

MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa kumekuwa na malalamiko mengi sana kwa Wabunge na baadhi ya wananchi kutokana na ucheleweshwaji na matumizi mabaya ya fedha yanayofanywa na baadhi ya Halmashauri hasa kule Zanzibar: Je, Serikali haioni haja sasa kwa kushirikiana na Serikali ya Zanzibar kubadilisha utaratibu wa fedha hizi, badala ya kupitia Halmashauri sasa kupitia moja kwa moja kwenye account maalumu za Majimbo husika? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Kumekuwa na utaratibu usiokuwa rasmi kwa baadhi ya Halmashauri hasa kule Zanzibar, ukizingatia kwamba Jimbo la Nungwi hadi hii leo bado hivi tunavyozungumza hatujapata fedha za mwaka 2021/2022. Hii ni kutokana na hali ya sintofahamu iliyotokezea pale Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini A.

Je, Serikali inawahakikishiaje wananchi wa Jimbo la Nungwi kuhusiana na fedha hizo juu ya upatikanaji wake? (Makofi)

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Sadiki Simai, Mbunge wa wananchi wa Jimbo la Nungwi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili la Mfuko wa Jimbo lipo kisheria na limeelezwa kabisa katika Sheria Na. 6 ya mwaka 2012 na katika sheria hii imeeleza wazi kwamba fedha zote za Mfuko wa Jimbo zitakuwa zinapitia kwenye Halmashauri. Sasa kwa kuwa Mheshimiwa ameshauri hilo na kwa kuwa jambo hili lipo kisheria, basi atupe muda tuone namna ya kufanya kwa sababu inabidi twende kwenye sheria ili tuhakikishe kwamba fedha hizi zinakwenda kwenye mifuko ya Wabunge wenyewe. Hata hivyo tulilifanya hili, kwani ilifika wakati tukaona kwamba fedha nyingi zilikuwa zikitumika kinyume na utaratibu. Ndiyo maana Serikali iliamua sasa zipitie kwenye Halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Halmashauri hiyo ama Jimbo lake kwamba mpaka leo fedha zile hazijapatikana na kwa sababu labda zilitumika kwa mambo mengine, tuseme tu kwamba lengo la Mfuko wa Jimbo ni kusaidia kuboresha miradi ya maendeleo katika Majimbo husika na hakuna lengo lingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tunataka tutoe wito kwa Halmashauri zote, Mabaraza ya Miji yote, kwamba fedha hizi zitumike kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya jimbo na siyo vinginevyo. La kwanza, wahakikishe wanawajulisha Wabunge kwamba fedha zimeingia; la pili, wawape fedha hizi kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo lake tutalifutilia na tutahakikisha kwamba fedha zake tutazipata kwa wakati. Nakushukuru.

Name

Juma Usonge Hamad

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chaani

Primary Question

MHE. HASSAN SADIKI SIMAI aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza malalamiko ya muda mrefu ya ucheleweshwaji wa fedha za Mfuko wa Maendeleo wa Jimbo upande wa Tanzania Zanzibar?

Supplementary Question 2

MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Changamoto ya Mfuko wa Jimbo kwa upande wa Zanzibar kila siku kila tukija hapa kwenye kikao suala hili linaibuka. Mpaka muda huu nazungumza, mimi Jimbo langu la Chaani sijapokea kwa ukamilifu fedha hizi za Mfuko wa Jimbo. Tumekuwa tukilalamika kila session ya Bunge, bado Serikali hatujaona kuchukua hatua stahiki kwa ajili ya kutatua changamoto hizi ambazo tena tunakubaliana nazo sisi Wabunge kupitia upande wa Zanzibar. Nakushukuru. (Makofi)

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Usonge, Mbunge wa Jimbo la Mkwajuni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiri kwamba bado kuna changamoto kwenye Mfuko wa Jimbo pamoja na kuboreshwa kwa hizi sheria. Changamoto kubwa tuseme ipo kwenye Mabaraza ya Miji na kwenye Halmashauri. Tulichokipanga baada ya Bunge hili, twende tukakae na viongozi wote wa Mabaraza ya Miji na Wakurugenzi wa Halmashauri wote Zanzibar ili tuwaeleze umuhimu wa fedha hizi kufika kwa wakati kwa Waheshimiwa Wabunge ili waweze kutekeleza miradi yao.