Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mrisho Mashaka Gambo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arusha Mjini

Primary Question

MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza: - Je, kuna mpango gani wa kutoa mwongozo wa upandishaji mishahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi?

Supplementary Question 1

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa gharama za maisha kwa wananchi wote bila kujali kama wanafanya kazi sekta binafsi au sekta za umma ni zilezile gharama kama mchele, unga na gharama nyingine.

Je, Serikali ina mpango gani ya kuhakikisha kwamba mishahara kwenye sekta binafsi na yenyewe inapanda inakuwa angalau shilingi 370,000 kama ilivyo kwa sekta ya umma? Kwa sababu sasa hivi maeneo mengi ni shilingi 100,000 kuendelea kidogo.

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, amesema kwamba wanategemea kutoa mwongozo wa kupandisha mishahara kwa sekta binafsi mwezi Novemba; je, watakapotoa miongozo na mishahara itakapopanda, wakati wengine wa Serikali tayari wameshapandishiwa mishahara toka tarehe 1 Julai; je, mwongozo huo pia utalipa na malimbikizo kwa muda ambao wenzao wameshaanza kulipwa?

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu la nyongeza la Mbunge wa Arusha, Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza niseme tu kwamba katika mishahara hii ya watumishi wa umma na wale wa sekta binafsi kuna utofauti mkubwa. Katika sekta binafsi tunazo kada tofauti tofauti, wapo wafanyakazi wa mashambani, wapo wa viwandani, wapo ambao ni makampuni binafsi, wapo waliojiajiri wenyewe na ambao wameweza kuajiri watu wachache. Kwa hiyo, uki- standardize na ukawa na standard level ya mishahara kwa kima cha chini inaweza ikaleta ugumu sana tumefanya study kuna best practice katika nchi nyingi ambazo tumeona kwamba huwezi uka-standardize kila mmoja na ndiyo maana bodi inaundwa ili ikafanye utafiti katika kuangalia uhalisia wa hali ya uchumi, lakini pia kazi zinazofanyika katika kila eneo ili iweze kuweza kupanga kulingana na category walizonazo hao wafanyakazi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wafanyakazi wa viwandani wana category yao, lakini pia na wale wa mashambani na maeneo mengine kulingana na uhalisia wa uchumi wa nchi husika. Kwa hiyo, tumelifanya hilo utafiti katika best practice ya nchi zaidi ya saba Mheshimiwa Mbunge. Kwa hiyo, niƱa imani kwamba bodi ya kima chini italeta ushauri ambao ni sahihi.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, ndiyo mwenye dhamana ya kuamua kwamba hapo kuna haki? Kwa sababu tunachopaswa kuangalia ni zile kazi za staha lakini atumishi aweze kulipwa mshahara wake ambao unafanana na hali halisia ya uchumi.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ameuliza kuhusu mishahara hii kwamba kwa upande wa Serikali tayari tumeshatangaza mabadiliko ya mishahara. Kwa upande wa private sector kama kutakuwa na malimbikizo.

Mheshimiwa Spika, kwa nchi yetu hatuna utaratibu wa restrospectivity, tuna utaratibu wa pale sheria au agizo linapotolewa ama kanuni, itakapopitishwa ndipo kwenda mbele hatua hiyo inafanyika. Kwa hiyo, hili suala la mishahara litaanzia pale kima cha chini kitakapokuwa kimerasimishwa na kutangazwa na Serikali. Ahsante.