Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Anton Albert Mwantona

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rungwe

Primary Question

MHE ANTON A. MWANTONA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati majengo ya Zahanati ya Ukoma kuwa Kituo cha Afya cha Kata ya Kisondela Wilayani Rungwe?

Supplementary Question 1

MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaishukuru Serikali kwamba imetujengea vituo vitatu vya afya kwa mwaka uliopita, ambapo kuna Kituo cha Ndanto, Kituo cha Kiimo pamoja na Kituo cha Ikinjola ambavyo viko mwishoni kabisa kukamilika na watumishi wameshapelekwa; je, ni lini vifaa tiba katika vituo hivyo vya afya vitapelekwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwenye Kituo cha Afya cha Masukuru, jengo la X-Ra, liko tayari, pia na jengo la mortuary liko tayari, lakini kwa bahati mbaya sana x-ray hatuna na mtumishi wa mortuary pale katika Kituo cha Afya Masukuru hakuna. Ni lini x-ray pamoja na mtumishi wa mortuary katika Kituo cha Afya cha Masukuru watapelekwa? Ahsante sana. (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Anton Albert Mwantona, Mbunge wa Jimbo la Rungwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipokee shukrani za Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa ambayo imefanywa na Serikali hii Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kujenga Vituo vya Afya vitatu ndani ya mwaka mmoja. Nimhakikishie kwamba mipango ya ujenzi wa Vituo vya Afya inakwenda sambamba na mipango ya ununuzi wa vifaa tiba. Katika bajeti ya mwaka huu Serikali imetenga jumla shilingi bilioni 69.95 kwa ajili ya vifaa tiba kwenye vituo vya afya 530. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pia tutatoa kipaumbele kwenye vituo vya afya ambavyo vimekamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusiana na ukosefu wa mashine ya x-ray na mtumishi wa mortuary, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea kununua vifaa tiba hivi kwa awamu. Kwa hiyo, mara pale tutakaponunua x-ray za kutosha basi kituo hiki cha afya pia kitatazamwa pamoja na kupelekewa mtumishi wa mortuary, ahsante. (Makofi)

Name

Felista Deogratius Njau

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE ANTON A. MWANTONA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati majengo ya Zahanati ya Ukoma kuwa Kituo cha Afya cha Kata ya Kisondela Wilayani Rungwe?

Supplementary Question 2

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Katika Kata ya Wazo, Jimbo la Kawe tayari zahanati imekamilika, lakini hakuna Jengo la Mama na Mtoto. Ni lini Serikali itajenga jengo hilo ili kunusuru uhai wa akinamama hao? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba katika Kata ya Wazo zahanati imekwishajengwa lakini hakuna Jengo la Mama na Mtoto, lakini nafahamu Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni haiwezi kushindwa kujenga Jengo la Mama na Mtoto. Kwa hiyo, nitumie fursa hii kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kutenga fedha kwa ajili ya kujenga Jengo la Mama na Mtoto katika zahanati hii kwenye Kata ya Wazo.

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Primary Question

MHE ANTON A. MWANTONA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati majengo ya Zahanati ya Ukoma kuwa Kituo cha Afya cha Kata ya Kisondela Wilayani Rungwe?

Supplementary Question 3

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spikaa, nakushukuru sana. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge imeshafanya tathmini kuhusu mahitaji ya maeneo ya kujenga vituo vya afya ambako kuna watu wengi na ni mbali. Kituo cha Afya katika eneo la Kata za Igigwa, Kiloleli, Ipole na Usunga. Je, ni lini Serikali itatusaidia kujenga vituo hivyo?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kakunda, Mbunge wa Jimbo la Sikonge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweka utaratibu wa kuainisha maeneo yote ambayo ni ya kimkakati kwa ajili ya kujenga Vituo vya Afya kwenye Kata na Tarafa za kimkakati na nakumbuka Mheshimiwa Mbunge alikwisha wasilisha kata hizo kwa ajili ya kujenga hivyo vituo vya afya na sisi tunafanya tathmini kujiridhisha tu na vigezo vile, lakini nimhakikishie kwamba tunafahamu Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge ni moja ya halmashauri kubwa na ina umbali mkubwa kati ya kata na kata, hivyo tutaweka kipaumbele katika ujenzi wa vituo hivyo vya afya.