Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Benaya Liuka Kapinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbinga Vijijini

Primary Question

MHE. BENAYA L. KAPINGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatenga fedha za ujenzi wa Vituo vya Afya Kata za Ukata na Litumbandyosi, Halmashauri ya Wilaya Mbinga?

Supplementary Question 1

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza niishukuru Serikali kwa majibu hayo lakini nimkumbushe tu Mheshimiwa Waziri kwamba vituo hivi vya kimkakati tulikubaliana, pamoja na kujengwa Makao Makuu ya Kata, lakini pia vijengwe kwenye kata zile za mbali. Kwa hiyo, Kata ya Ukata iko mbali sana na hiki kituo cha Mkumbi. Kwa hiyo, nini maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali ilipeleka fedha milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Mapela na mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya vifaa tiba Shilingi milioni 320, lakini mpaka leo hii vifaa tiba katika kituo hiki cha afya havijafika. Sasa nataka kujua fedha hizi ziko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Kituo hiki cha Mkundi, Matiri, pamoja na Muungano, sasa hivi vimeshakamilika. Ni lini sasa tutapeleka watumishi pale ili vianze kufanya kazi?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Benaya Liuka Kapinga, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ilitoa mwongozo wa kujenga vituo vya afya kwenye maeneo ya kimkakati, vigezo vikiwa kwanza idadi ya wananchi katika eneo husika, lakini pili, umbali wa kituo kile kutoka kituo cha karibu zaidi au hospitali ya karibu zaidi. Kwa hiyo, ukitoa kata yoyote ambayo inakidhi vigezo hivyo ina sifa ya kuwa kata ya kimkakati kwa ajili ya kituo cha afya. Kwa taarifa tulizonazo bado idadi ya watu sio kubwa sana, kwa hivyo inakosa ile sifa kuwa kituo cha afya cha kimkakati kwa maana ya idadi ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi milioni 400 zilipelekwa katika kituo cha afya alichokitaja Mheshimiwa Mbunge na milioni 320 za vifaa tiba tayari zimepelekwa Bohari Kuu ya Madawa (MSD) kwa ajili ya kuleta vifaa hivyo. Tunaendelea kushikirikiana na Wizara ya Afya, kuhakikisha vifaa hivyo vinaletwa mapema iwezekanavyo ili huduma za afya zianze kutolewa katika kituo kile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na hivi vituo vitatu vilivyokamilika, kwanza tumshukuru Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha nyingi kukamilisha vituo vya afya vitatu na nimhakikishie Mbunge kwamba mpango wa ajira kwa watumishi kwa awamu ni kuhakikisha kwamba tunaleta watumishi kwenye vituo hivyo pia ili huduma zianze kutolewa.