Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Omar Issa Kombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wingwi

Primary Question

MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza: - Je, ni lini wananchi wenye sifa wa Shehia ya Njuguni, Majenzi na Chomboni – Micheweni wataunganishwa na TASAF?

Supplementary Question 1

MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri sana, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni nimeona baadhi ya wananchi wakifutwa kwenye mpango wakati bado hali zao ni mbaya sana, na naomba nimtaje mwananchi ambaye ni mfano, anaitwa Ndugu Hamad Faki Hamad maarufu Fofofo kutoka Shehia ya Mjini Wingwi, hali yake ni mbaya sana lakini amefutwa.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anatoa kauli gani kwa TASAF dhidi ya hali kama hizi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Serikali inatoa kauli gani dhidi ya taarifa ambazo zinasambaa kwa wananchi ambazo zinaleta wasiwasi kwamba wanakwenda kufutwa kwenye mpango wakati hali zao bado ni mbaya. Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya taarifa hizi? Ahsante.

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kombo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kumpongeza yeye mwenyewe Mheshimiwa Kombo, Mbunge wa Wingwi, kwa sababu pia ni mjumbe wa Kamati ya USEMI ambayo inasimamia Wizara yetu hii Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na amekuwa akifuatilia sana masuala haya ya TASAF hasa jimboni kwake kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nikienda kwenye maswali yake anauliza ni vigezo gani ambavyo hata huyu amemtaja Mzee Hamad Faki vimemuacha. Sijui hasa kwenye kesi hiyo kama individual na nitakaa naye Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kujua kwa nini Mzee Faki alitoka katika mpango wa TASAF, tukitoka hapa nitakutana naye ili tuweze kulijua.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda niseme jambo moja katika mradi huu awamu hii ya pili imekuwa ina component mbili; component ya kwanza ni ile ambayo tulikuwa tumeizoea kwenye awamu ya kwanza ya mradi huu wa TASAF, ni ule wa cash kwenda kwenye kaya hizi, lakini component ya pili ni public works. Kwamba kaya huenda ina watu watano, na mkuu wa kaya anaweza akawa ni mtu mzima labda ana miaka 70 lakini ndani ya kaya ile kuna watu wenye uwezo wa kufanya kazi. Basi watafanya kazi na kulipwa ujira kutoka kwenye mradi wa TASAF, kwenye miradi ile ambayo wameibua wao wenyewe katika maeneo yao husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye swali lake la pili, ya taarifa hizi kwamba wanufaika wanaenda kufutwa. Niseme taarifa hizi si za kweli, walengwa hawa hawaendi kufutwa, na tulifanya uhakiki kabla ya kuingia kwenye awamu ya pili ya mpango huu na kaya zimeongezwa. Serikali hii ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake mwenyewe alielekeza tuongeze idadi ya kaya kwenye mpango huu wa TASAF, na kaya zimeongezwa na hauendi kufutwa.