Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ramadhan Suleiman Ramadhan

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chake Chake

Primary Question

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN aliuliza: - Je, ni lini Serikali itajenga kituo kipya cha Polisi katika Wilaya ya Chakechake?

Supplementary Question 1

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ingawa Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu vizuri kwenye swali lake la msingi, naomba nimwulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza ni kwamba, wakati tunasubiri fedha zitengwe kwenye bajeti ya mwaka 2023/2024 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo kikubwa.

Je, Serikali haioni haja ya kujenga vituo vidogo vya Polisi (Police Post) kwenye maeneo tofauti ya Mji wa Chakechake? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kufuatana nami twende kwenye eneo la Chakechake akaone jiografia na kama ujenzi wa Kituo cha Vitongoji ndiyo ingekuwa suluhisho la wananchi kufuata huduma za kipolisi? (Makofi)

Name

Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja, ni kweli kwamba pale ambapo pana umuhimu Serikali inaweza ikasaidiana na wananchi kujenga Police Post kwa maana ya vituo vidogo vya Polisi panapohitajika. Hata hivyo, kwa sababu Kituo cha Chakechake kwa sasa kimechakaa, kinahitajika kujengwa kituo kipya, kipaumbele tumeweka kwenye kujenga kituo kipya katika mwaka wa fedha ujao. Namwomba Mheshimiwa Mbunge akubaliane nasi tulitekeleze hilo kwanza.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili juu ya umuhimu wa kuongozana naye kwenda vitongojini, niko tayari, hakuna kikwazo chochote. Wakati utakapofika tukaambiana basi tutaongozana. Nashukuru. (Makofi)

Name

Ussi Salum Pondeza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chumbuni

Primary Question

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN aliuliza: - Je, ni lini Serikali itajenga kituo kipya cha Polisi katika Wilaya ya Chakechake?

Supplementary Question 2

MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niulize swali dogo la nyongeza. Kama ilivyo Jimbo la Chakechake kuhusu kujengewa kituo; nami nimekuwa nikiuliza sana katika Jimbo langu la Chumbuni; na nimekuwa nikipewa ahadi zaidi ya mara sita, saba kwa vituo vyangu viwili vya Marubi na Chumbuni kuwa nitapata msaada kutoka Jeshi la Polisi na kujengewa; na tuliwahi kuuliza ikiwa Serikali iko tayari kuvirasimisha kwetu, kwa wananchi wa Jimbo la Chumbuni? Basi wafanye hivyo, halafu watupe kibali, nasi tunaweza kuendelea wenyewe. Ahsante.

Name

Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Pondeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli amekuwa akiuliza maswali ya Chumbuni na nilimwahidi katika kipindi cha bajeti cha Aprili – Juni. Niliweza kwenda Zanzibar na nilitembelea kituo chake. Kinachogomba ni upatikanaji wa fedha ndiyo maana tunaweka vipaumbele. Mheshimiwa Mbunge avumilie na akubaliane nami kwamba pale tutakapopata fedha, Chumbuni itapewa kipaumbele kama tunavyofanya kwenye maeneo mengine ya Chakechake na kwingineko. Nashukuru. (Makofi)

Name

Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Primary Question

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN aliuliza: - Je, ni lini Serikali itajenga kituo kipya cha Polisi katika Wilaya ya Chakechake?

Supplementary Question 3

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Liwale ina umri wa miaka 47 sasa, haijawahi kuwa na jengo la Kituo cha Polisi ukiacha lile jengo ambao wamepanga lililokuwa la benki. Nini, kauli ya Serikali kuipatia Wilaya ya Liwale jengo la Polisi? (Makofi)

Name

Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunafahamu Wilaya kongwe hizi zimekuwa na vituo lakini chakavu sana. Sasa kwa bahati mbaya Liwale hawajawahi kuna nacho. Namwahidi kwamba katika bajeti ijayo tutaweka kipaumbele ili Wilaya yake ianze mchakato wa kujenga kituo chake cha Polisi kama zilivyo Wilaya nyingine za Tanzania Bara. Nashukuru. (Makofi)

Name

Khalifa Mohammed Issa

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Mtambwe

Primary Question

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN aliuliza: - Je, ni lini Serikali itajenga kituo kipya cha Polisi katika Wilaya ya Chakechake?

Supplementary Question 4

MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami nimwulize swali moja dogo la nyongeza Mheshimiwa Naibu Waziri. Kituo cha Wete ndiyo Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba. Kituo kimechakaa, hakina hadhi: Ni lini Serikali itakikarabati kituo kile? Ahsante. (Makofi)

Name

Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mbunge wa Wete, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nafahamu na Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba vituo vingi vilivyojengwa siku nyingi vimechakaa sana. Kama atafuatilia, tumeanza kukarabati vituo vya Polisi vikianzia Makao Makuu pale Zanzibar na makazi yao. Tutaendelea kufanya hivyo maeneo ya Pemba kutegemea upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, tumeshakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba awamu ijayo nitatembelea Pemba na eneo la Wete ni eneo nitakalolipa kipaumbele katika ziara yangu. Nashukuru.

Name

Mohammed Said Issa

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Konde

Primary Question

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN aliuliza: - Je, ni lini Serikali itajenga kituo kipya cha Polisi katika Wilaya ya Chakechake?

Supplementary Question 5

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kuuliza swali dogo la nyongeza. Katika Bunge lililopita la bajeti, Wizara ya Mambo ya Ndani iliniahidi kituo cha Konde kutengenezwa kwa thamani ya shilingi 41,500,000 na bajeti tayari tumeshapitisha.

Je, ni lini Wakandarasi watafika kwenye Kituo cha Konde na kuanza matengenezo? Ahsante sana. (Makofi)

Name

Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika,
naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge wa Konde, swali lake la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, maadamu bajeti imepitishwa na ipo na anachosubiri ni Mkandarasi, tutawasiliana na Kamishna wa Polisi Zanzibar ili mipango ya kumpa Mkandarasi, kwa sababu tunatumia force account, aweze kuelekezwa engineer wa Polisi Zanzibar ili ukarabati wa jengo hilo uweze kuanza. Nashukuru. (Makofi)