Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mussa Ramadhani Sima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Primary Question

MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa muongozo kwa Vyama vya Wafanyakazi hasa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na kupunguza ada ya uanachama au kuondoa kabisa mfumo wa asilimia ili kuweka kiwango kitakachokubaliwa na wanachama wenyewe?

Supplementary Question 1

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru, nadhani kwa majibu haya ya Serikali inanishawishi sasa kuja na Hoja Binafsi Bungeni ili tuwasaidie walimu, tuisaidie pia Serikali na vyama vya wafanyakazi.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekiri kabisa kwamba kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini kwamba vyama sasa na wanachama wanapanga ada yao ambayo watalipa wanachama.

Sasa nataka kujua; Serikali inapata wapi uhalali wa kukusanya ada za wanachama na kuwapa vyama hali ya kuwa wanajua wako baadhi ya watumishi, hasa walimu wanakatwa bila ridhaa yao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kada ya ualimu ndiyo kada pekee sasa hivi ina vyama vitatu vinavyotetea haki za walimu. Kuna Chama cha Walimu ambacho kinatoza ada asilimia mbili; kuna Chama cha CHAKAMWATA ambacho kinatoza ada asilimia moja; lakini kuna Chama kingine cha KUWAHATA, chenyewe kimeweka fixed amount ya shilingi 5,000.

Mheshimiwa Spika, sasa Serikali haioni haja ya kuleta mwongozo ambao uta-regulate mwenendo wa vyama hivi ili sisi walimu tusiwe soko holela la watu kuja kujitafutia ujira kwenye nanihii yetu hii? Naomba majibu.

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Sima, amekuwa mtetezi mzuri wa maslahi ya walimu, na yeye mwenyewe amewahi kuwa kiongozi katika vyama hivi vya walimu na kwa hiyo, nimpongeze yeye pamoja na walimu wenzake; Mwalimu Kassim Majaliwa Majaliwa, Mwalimu Jenista Mhagama, Profesa Ndalichako na walimu wengine wengi pamoja na Mwalimu Spika ambaye leo tunaye hapa, Mheshimiwa Dkt. Tulia mwenyewe; nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye jibu, hapa ni kweli kwamba suala hili linasimamiwa kwa mujibu wa sheria na ni Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004. Sheria hii inatoa miongozo wa namna gani ambavyo vyama vya wafanyakazi vinaweza vikasimamia maslahi yake. Na ni takwa la Mkataba wa Kimataifa wa ILO (International Labour Organisation) Sheria Na. 3 katika mkataba huo katika kifungu cha tatu inaeleza kwamba vyama hivi viwe huru na vijiendeshe na kujitaribu vyenyewe, na Serikali anaendelea kuwa regulator tu.

Mheshimiwa Spika, sasa kwenye eneo la vyama kama alivyosema katika zile asilimia, vikao vikuu kwa mujibu wa katiba ndivyo vinakaa na kufanya maamuzi. Lakini hata hivyo, kwenye Chama hiki cha CHAKAMWATA tayari kimekwisha kusimamishwa na msimamizi wa masuala ya vyama vya wafanyakazi na kesi inaendelea, iko mahakamani.

Mheshimiwa Spika, pili, kwenye suala la Chama cha KUWAHATA ambacho wanachaji shilingi 5,000, wanaochajiwa ni wale tu ambao ni wanachama, kama siyo mwanachama hana haki ya kukatwa fedha hizo. Kwa hiyo tutafanya ufuatiliaji na tutashirikiana na Mheshimiwa Mbunge kuweza kuhakikisha haki za walimu zinalindwa kwa sababu walimu ndio nguzo kuu ambayo inatutengenezea Taifa letu, tunapata wataalam kutokana na walimu na walimu hawa ni wadau wa muhimu kwa Serikali hii ya Mama Samia Suluhu Hassan, na hatutawaacha, tutaendelea kutetea haki zao. Ahsante sana. (Makofi)