Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 6 Sitting 14 Youth, Disabled, Labor and Employment Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu 159 2022-02-18

Name

Mussa Ramadhani Sima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Primary Question

MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa muongozo kwa Vyama vya Wafanyakazi hasa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na kupunguza ada ya uanachama au kuondoa kabisa mfumo wa asilimia ili kuweka kiwango kitakachokubaliwa na wanachama wenyewe?

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Vyama vya Wafanyakazi kikiwemo Chama cha Walimu Tanzania (CWT) vimeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004 ambayo ndiyo inayoongoza vyama vya wafanyakazi, vyama vya waajiri na mashirikisho vikiwa na lengo la kusimamia haki na maslahi ya wanachama wake ambao ni wafanyakazi walio katika sekta ya elimu.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu 47(c) cha sheria hiyo kimetoa sharti kwamba katiba za vyama lazima zieleze kuhusu ada ya uanachama au njia yoyote ya kuamua ada hiyo. Kwa mantiki hiyo, chama kupitia katiba yake na wanachama ndio wenye mamlaka ya kujadili na kukubaliana masuala ya ada za uanachama katika chama husika na siyo Serikali.

Mheshimiwa Spika, katiba ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kupitia kifungu cha 23.1(c) kimetoa mamlaka kwa Mkutano Mkuu kufanya mabadiliko ya katiba kwa uamuzi wa theluthi mbili za wajumbe walio na haki ya kupiga kura. Hivyo kupitia mkutano huo, wanachama ndiyo walioamua kuhusu njia ya ukataji wa ada kwa asilimia mbili. Hivyo, kwa kutumia chombo hicho hicho wanachama wanaweza kuamua kuweka utaratibu mwingine wa ukataji wa ada husika bila kuvunja sheria. Ahsante.