Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Amour Khamis Mbarouk

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tumbe

Primary Question

MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK aliuliza: - Je, Serikali inakusanyaje ushuru kwenye Boti zinazoondoka saa moja kamili asubuhi katika Bandari ya Dar es Salaam ilhali watumishi hufika kazini kuanzia saa moja na nusu na zaidi?

Supplementary Question 1

MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri au majibu ya Serikali.

Kimsingi majibu ni mazuri sana, ila uhalisia ulivyo ni kwamba, abiria anaweza kuwa na mzigo akatakiwa kulipa, lakini akiuliza alipie ofisi gani, akakosa hiyo ofisi na akatakiwa kumpa fedha mkononi mchukuzi ambaye ndiye atamlipia itakapofika saa 1.30. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maswali mawili ya nyongeza; kwanza, naomba kujua ni mzigo wenye uzito kiasi gani ambao mtu akipita nao hapo bandarini atatakiwa kulipa? (Makofi)

Pili, je, Serikali haioni umuhimu wa kupunguza au kuondoa kabisa ushuru wa wafanyabiashara wadogo wadogo wanaotoka Zanzibar kuja kuchukua biashara zao hapa Tanzania? Ahsante sana. (Makofi)

Name

Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Amour Khamis Mbarouk kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nipokee shukurani za Mbunge kwa niaba ya Serikali. Pili, naomba kujibu maswali yake mawili kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza amezungumzia suala la uzito; anataka kufahamu ni uzito kiasi gani ambao anastahili ama anapaswa kulipa anapopita pale bandarini? Ieleweke kwamba Mamlaka yetu ya Bandari nchini inaongozwa kwa mujibu wa Sheria ya Mwaka 2004 na miongozo mbalimbali ikiwepo Mwongozo wa Mwaka, 2003 na Aya ya 12(1) na aya ya 71(1). Miongozo hii inatuelekeza kwamba mzigo wa abiria yeyote anayetoka Bara ama kwenda Visiwani au Visiwani kuja Bara inatakiwa atozwe ukiwa hauzidi kilogram 21. Hilo la kwanza kupitia Mwongozo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, inaelekeza kwamba inatakiwa ujazo wa huo mzigo kwa maana ya cubic measurements usizidi moja, kwa maana ya ujazo wake ama nafasi inayochukua huo mzigo wako ni kiasi gani? Kuhusu wafanyabiashara wadogo kupunguziwa gharama pale bandarini; nataka nimhakikishie Mbunge ya kwamba kama wewe una bidhaa, kwa mfano, una baiskeli au TV ya matumizi yako binafsi, haitakiwi utozwe ushuru pale bandarini. Ila kama una zaidi ya hivyo, hii sheria itatuhusu sote. Ahsante. (Makofi)

Name

Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK aliuliza: - Je, Serikali inakusanyaje ushuru kwenye Boti zinazoondoka saa moja kamili asubuhi katika Bandari ya Dar es Salaam ilhali watumishi hufika kazini kuanzia saa moja na nusu na zaidi?

Supplementary Question 2

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, tunajua bandari yetu ni miongoni mwa chanzo cha mapato, na kumeibuka kuwepo kwa bandari bubu zaidi ya 58 katika Mikoa mbalimbali ambapo Serikali yetu inakosa mapato. Naibu Waziri ulikuwa Mwenyekiti wa Kamati na huu ni mfupa mzito ambapo mapato ya Serikali yanapotea.

Je, ni lini sasa mchakato wa kuangalia hizi bandari zote kama walivyokuwa wameahidi walipokuja kwenye kamati. Ni lini sasa mtazirasimisha rasmi ikiwemo na badari ya Mbweni ili Serikali iweze kukusanya mapato ya kutosha na kupeleka maendeleo kwa Watanzania? Ahsante. (Makofi)

Name

Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, kwanza nitambue Mheshimiwa Ester Bulaya kama ulivyosema nilikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma changamoto hizi tuliziona na hivi sasa kati ya bandari zote nchini tuna bandari 693 nchi nzima ya Tanzania ambazo ni bandari bubu. Na tunazo bandari 66 tu ambazo ni rasmi. Bandari ya Mbweni ambayo ni miongoni mwa bandari 24 ambazo tutakwenda kuzirasimisha hivi sasa ninavyosema.

Mheshimiwa Spika, badari hizi zinaingiza fedha kwa mwaka shilingi milioni 200 kwa hiyo, kuna umuhimu mkubwa sana wa kurasimisha bandari bubu ambazo zinaingiza fedha Serikalini. Nitoe wito pia kwa kuwa siyo kila sehemu tutaajiri kama TPA kwa maana tutashirikiana na halmashauri husika katika maeneo hayo ili hizo bandari ziewe kurasimishwa. Ahsante.