Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Anton Albert Mwantona

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rungwe

Primary Question

MHE. ANTON A. MWANTONA aliuliza: - Je, nini mchango wa Serikali katika kuwawezesha vijana zaidi ya 100 waliomaliza Vyuo vikuu ambao wapo tayari kwa ajili ya kujiajiri katika kilimo Wilayani Rungwe kupitia Ofisi ya Mbunge?

Supplementary Question 1

MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu. Naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza private sector ni mdau kutoa ajira kwa wananchi ya wananchi wa Tanzania kwa kushirikiana pamoja na Serikali. Tukiangalia katika nyanja mbalimbali private sector imeathirika kwa kiasi fulani especially ukiangalia kwenye mambo ya shule na taasisi nyingine; uendeshwaji wa shule umekuwa ni mgumu kwa kiasi fulani kiasi kwamba utoaji wa ajira kwa vijana wetu umekuwa ni mgumu kwa kiasi kikubwa. Labda kutokana na UVIKO 19 na mambo mengine ambayo yako: Je, Serikali ina mpango gani kusaidia private sector na kufanya tathmini ya kina kwenye private sector kwa lengo la kuisaidia ili iweze kusaidia kutoa ajira kwa vijana wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwenye swali langu la msingi nimesema vijana ambao wamehitimu Vyuo Vikuu zaidi ya 100 wamejiunga pamoja na wapo tayari; na wameweka utaratibu wao, wamesema wenyewe ni kilimo cha makambi; kwamba wanaweza wakakaa sehemu wakaweka kambi, wakafanya kilimo. Walikuwa wanaomba Serikali iweze kuwasaidia mtaji wa pembejeo pamoja na soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza, Serikali ina kauli gani kutokana na hao vijana ambao tayari wameshajitoa, wako tayari kufanya kilimo cha makambi kuweza kuwasaidia ili waweze kupata ajira? Ahsante sana. (Makofi)

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU (MHE. PATROBASS P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anton Albert Mwantona, kama ifuatavyo katika maswali yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyooleza kwenye swali la msingi katika swali lake la pili ambapo amesema vijana tutawasaidia vipi ambao tayari wameshaji-mobilize ili waweze kupata fedha au kuwekewa mtaji waweze kuendelea na shughuli zao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili kama nilivyolieleza kwenye jibu la msingi ni kwamba tunashirikiana na Wizara ya Kilimo katika kuhakikisha kwanza tunatenga maeneo, na hapo kwenye Jimbo la Mheshimiwa Mbunge tayari kuna ekari 88.9 ambazo zinaweza kuwasaidia hawa vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Wizara ya Kilimo itaweka miundombinu na jukumu la mafunzo litabaki kuwa katika Ofisi ya Waziri Mkuu; na tatu, tutaenda sasa katika kuhakikisha mpaka kwenye hatua ya mwisho ya kutafuta masoko kwenye zao la kilimo au zao biashara ambalo watakuwa nalo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya hapa tuwasiliane, tuweke mpango mzuri kwa ajili ya kuwasaidia hao vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameuliza Serikali ina mpango gani wa kusaidia private sector kwa kuwa ndiyo mdau mkuu pia katika kutoa ajira? Tayari Serikali imeshaanza kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo kubadilisha sera mbalimbali hasa zile ambazo zinahusiana na masuala yanayogusa ajira. Katika sera nyingi ambazo ziko katika Wizara za kisekta tumeshaanza kufanya mapitio mapya kuweza kuhakikisha sera hizo zinaendana na usasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, mabadiliko mbalimbali ya sheria ili kuweza kuhakikisha kwamba kunakuwa na uwezekano mkubwa wa private sector kukua kama jinsi ambavyo tumerekebisha sheria ya kuajiri au kuratibu ajira za wageni. Tumeenda pia kwenye mabadiliko ya sheria na sera na mipango ya masuala ya uwekezaji na uchumi. Kwa hiyo, kwenye eneo hilo Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake, tunaona sasa ameendelea kuweza kuhakikisha kwamba private sector inaweza kufanya kazi kwa ukubwa zaidi na upana ili iweze kuajiri watu wengi zaidi. Nakushukuru.

Name

Judith Salvio Kapinga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ANTON A. MWANTONA aliuliza: - Je, nini mchango wa Serikali katika kuwawezesha vijana zaidi ya 100 waliomaliza Vyuo vikuu ambao wapo tayari kwa ajili ya kujiajiri katika kilimo Wilayani Rungwe kupitia Ofisi ya Mbunge?

Supplementary Question 2

MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Nina swali dogo la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala ya ajira kwa vijana yanawekewa msingi na Sera ya Maendeleo ya Vijana ya 2007. Serikali imekuwa katika mchakato wa kufanya mapitio ya Sera ya Maendeleo ya Vijana 2007 kuanzia mwaka 2016 mpaka 2018. Sasa swali ni: Je, Serikali ina mkakati gani wa kukamilisha Mapitio ya Sera ya Maendeleo ya Vijana mwaka 2007 ambayo yameanza kutoka 2016 mpaka 2018 na mpaka leo hajahitimishwa ili mapitio haya yaweze kuratibu ajira kwa vijana na yaweze kuwa na tija zaidi? (Makofi)

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU (MHE. PATROBASS P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Judith Kapinga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameuliza kuhusiana na nil ini Serikali hasa itakamilisha mchakato huu wa sera. Kwanza tunamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake wa masuala ya vijana wakati wote, lakini tayari sisi kwa upande wa Serikali tumeshaenda kwenye hatua mbalimbali; imetoka kwenye hatua ya makundi na wadau mbalimbali kuweza kuwashirikisha ili waweze kutoa michango yao katika sera. Hivi karibuni nadhani kama haitachukua muda sana, ndani ya mwaka huu tutakuwa tumeenda kwenye hatua ya kutoa taarifa rasmi ya namna gani ambavyo tumeenda ukamilishaji wa sera hii ya vijana ya mwaka 2007. Ahsante.