Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Florent Laurent Kyombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Primary Question

MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza: - Je, ni lini Serikali itawatambua watu wenye haki ya Uraia ili wapate Vitambulisho vya Taifa pamoja na kuwapa Uraia watu ambao siyo raia lakini wameishi nchini kwa zaidi ya miaka kumi na tano?

Supplementary Question 1

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru tena kwa nafasi. Ni mara ya pili nauliza swali kama hili katika Bunge lako Tukufu, lakini kwa imani kubwa niliyonayo kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, ndugu yangu, Mheshimiwa Engineer Masauni na Mheshimiwa Sagini, naamini sasa hili suala litakwenda kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Jimbo la Nkenge, Wilaya ya Misenyi, hasa Kata za Mutukura, Kakunyu, Minziro na maeneo mengine wamekuwa na mila na desturi zinazofanana kabisa na Nchi ya Uganda. Sisi tunaongea Ruganda lakini majina unayoyakuta upande wa Tanzania ni sawasawa na unayoyakuta upande wa Uganda. Wataalam wetu wa Uhamiaji wamekuwa wanatumia kigezo hicho kuwa-judge kwamba siyo raia kwa sababu ya lugha na majina yale.

Mheshimiwa Spika, swali langu; je, ni lini Serikali itatambua hayo mahusiano ya ukaribu ya mila na desturi wananchi wakapewa haki yao ya uraia na waweze kupata pia vitambulisho vya NIDA? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa sheria, kama aliyoitaja Naibu Waziri ya mwaka 1995 ya Uraia inaruhusu mwananchi ambaye amekaa katika nchi yetu kwa muda wa takribani miaka saba hadi kumi kwa tabia njema aweze kupata uraia wa Tajnisi. Sasa Mheshimiwa Waziri au Naibu Waziri, hamuoni ni muda muafaka twende wote katika kata hizo tukae na wananchi tuwaongoze wajaze fomu waweze kupata uraia na kuishi kwa amani katika nchi yao? Ahsante sana.

Name

Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Kyombo kwa namna anavyofuatilia kwa karibu maslahi ya wananchi wake, hususan anaoona wanakosa uraia ambao wanastahili.

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema, bahati nzuri vigezo anavifahamu, ametaja uraia mwema lakini viko vigezo vingine ambavyo vipo kwa mujibu wa sheria, kwa haraka nitaje vichache: -

Mheshimiwa Spika, tunasema kabla ya tarehe ya kuwasilisha maombi yake ya uraia awe alikuwepo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miezi 12 mfululizo; kwamba katika kipindi cha miaka kumi kabla ya muda wa miezi 12 awe ameishi ndani ya Jamhuri ya Muungano kwa kipindi kisichopungua miaka saba; awe na ufahamu wa kutosha wa Lugha za Kiswahili na Kiingereza au Kiingereza; awe mwenye tabia njema. Hiyo ni moja, lakini mbili za mwisho, awe amechangia au ameshiriki katika kukuza uchumi wa Taifa na mwisho aahidi kwamba akipata uraia anayo nia ya kuendelea kuishi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo ikiwa amekidhi vigezo hivi kwa kweli ana haki ya kupewa uraia.

Mheshimiwa Spika, ombi lake la pili, mimi na Waziri wangu, tuko tayari kuongozana naye na wataalam wetu ili kuona changamoto ambayo wanakabiliana nayo wananchi hawa walioko mpakani. Kuzungumza lugha ya nchi jirani hakiwezi kuwa kigezo cha kumnyima mtu uraia kwa sababu hali ya mipakani iko hivyo katika maeneo yote. Nashukuru.