Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Conchesta Leonce Rwamlaza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza: - Je, Serikali haioni kuwa kuajiri Walimu bila kujali muda wa kuhitimu, baadaye baadhi yao watashindwa kuajiriwa kutokana na umri wao kuwa mkubwa?

Supplementary Question 1

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa sasa Serikali inasema inatumia mfumo wa online katika kupokea maombi ya Walimu; na kwa kuwa malalamiko ni mengi ambayo yalikuwa yanahusu Walimu kutoajiriwa kutokana na mwaka waliohitimu. Sasa napenda kuiuliza Serikali; haioni sasa kuna haja pale nafasi zinapopatikana za kuajiri waweke ukomo kwa wale wanaoomba kwamba mwaka huu tutapokea maombi ya wahitimu wa vyuo vya Walimu wa mwaka fulani hadi mwaka fulani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Walimu kutoajiriwa muda mrefu kunawafanya wakae mitaani, lakini pia miaka inapita wengine wanaweza kutoajiriwa kwa sababu ya umri walionao. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuwapatia refresher courses kwa sababu wale Walimu waliokaa muda mrefu wanapokuwa hawakuajiriwa wanasahau baadhi ya mafunzo yao na hata zile methodologies za kufundisha. Je, Serikali haioni kwamba wanastahili kupewa refresher courses na wako tayari kuzitoa? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfumo huu wa Online Teachers’ Employment System ni mfumo ambao kwanza umeleta uwazi, lakini pia umeleta haki kwa wale Walimu wenye sifa kuajiriwa bila kuwa na upendeleo wowote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuwa na ukomo wa ajira, tumesema vigezo vyetu vilikuwa vitatu; kigezo cha kwanza kilikuwa ni wale waliohitimu muda mrefu zaidi. Ndiyo maana zaidi ya asilimia 75 ni wale waliohitimu mwaka 2014 hadi 2017. Hiyo consideration iliwekwa ili wale wenye umri mkubwa wapate nafasi ya kuajiriwa kabla ya umri wao wa miaka 45 kufikiwa na kukosa fursa ya kuajiriwa Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, wale walioajiriwa mwaka 2018 hadi 2019, wahitimu wa miaka hiyo walikuwa wana mahitaji maalum na walio wengi walikuwa wenye ulemavu. Kwa hiyo bado itakuwa siyo sahihi sana kuweka kigezo cha kwamba tuajiri miaka miwili au mitatu; kwanza hatujui ni Walimu wangapi watajitokeza katika miaka hiyo kulingana na mahitaji yetu na ni wangapi watachujwa na kuwa na sifa husika. Tunaweza tukasema kati ya 2018 na 2019 lakini wakatokea wachache wenye sifa na tukakuta tumeweza kuathiri zoezi hilo. Kwa hiyo tutaendelea kuhakikisha kwamba tunawapa fursa wote kuajiriwa, lakini tunatumia vigezo vyetu kuona nani kwa sasa apate ajira na nani anaweza akapata ajira awamu inayofuata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na Walimu kukaa muda mrefu zaidi bila ajira, ni kwa sababu tumekuwa na baraka nzuri kwamba Walimu wengi wanazalishwa kwenye vyuo vyetu kila mwaka ikilinganishwa na kasi ya ajira ambayo ipo Serikalini lakini pia kwenye taasisi binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la msingi ni kwamba mara baada ya kuajiriwa katika shule zetu kuna taratibu za refresher courses na on-job training na mentorship ambazo watazipata. Kwa hiyo automatically ukishaingia kwenye shughuli zao za kazi watapata mafunzo kazini na kuwawezesha kuwa competent zaidi. Ahsante.

Name

Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Primary Question

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza: - Je, Serikali haioni kuwa kuajiri Walimu bila kujali muda wa kuhitimu, baadaye baadhi yao watashindwa kuajiriwa kutokana na umri wao kuwa mkubwa?

Supplementary Question 2

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inafanya kazi nzuri sana ya kujenga majengo ya sekondari kwenye shule nyingi sana hapa nchini. Katika Jimbo langu la Bunda kuna shule nane, zina upungufu wa Walimu wa sayansi 56, na tunaposema walimu wa sayansi maana yake tuna masomo ya baiolojia, fizikia, kemia na hisabati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, je, ni lini Walimu 56 wa sayansi watapelekwa katika Shule za Sekondari za Hunyari, Chamuriho, Mihingo, Mekomariro, Salama, Esparento, Makongoro, Nyamang’uta; ni lini hawa Walimu 56 watakwenda huko? Tunapouliza maswali haya maana yake ni kwamba watoto wako darasani, lakini Walimu wa sayansi hawapo. (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Getere, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa Walimu wa sayansi bado ni changamoto ambayo Serikali tunaitambua na tumeweka mkakati wa kuhakikisha katika ajira zetu tunaweka kwanza kipaumbele cha Walimu wa masomo ya sayansi. Katika zile ajira ambazo zimepita asilimia kubwa ya walimu walioajiriwa ni Walimu wa masomo ya sayansi. Hata hivyo, tumeweka mkakati pia kwenye ajira zinazofuata, walimu ambao wataajiriwa kwa kiasi kikubwa ni Walimu wa sayansi ili kuwezesha kupunguza pengo la upungufu wa Walimu wa sayansi katika shule zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Getere kwamba wakati wa ajira hizo Halmashauri yake ya Bunda na shule hizi alizozitaja zitapewa kipaumbele kupata Walimu hawa wa sayansi ili kupunguza pengo la Walimu 56 ambao hawapo katika halmashauri hiyo. Ahsante.