Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Primary Question

MHE. IDDI K. IDDI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatoa vifaa tiba na dawa za kutosha kwenye vituo vya afya na zahanati zote katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala?

Supplementary Question 1

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kumekuwa na changamoto ya watu wenye bima wanapokwenda kwenye kituo cha afya ama zahanati kukosa dawa. Sasa Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba inaziunganisha bima zao za afya na maduka ya private ama maduka yaliyomo ndani ya hospitali za Serikali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; tumekuwa na changamoto pia ya upatikanaji wa dawa kwa wakati na Halmashauri ya Msalala tulitenga milioni 30 kununua dawa na tulipoomba dawa kutoka MSD waliweza ku-supply dawa kiasi cha shilingi milioni 17 tu na wakakosa dawa na fedha zipo. Kwa maelezo ya Wizara ni kwamba, wanapokosa dawa kuna yule mshitiri ambaye amechaguliwa kwa ajili ya ku- supply dawa. Washitiri hawa wana-supply mkoa mzima na mikoa mingi; sasa Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba inaanzisha washitiri hawa, hawa watu wanao- supply dawa kwenye kila wilaya ili kuondoa gharama kwanza za usafirishaji wa dawa, lakini pia kupatikana kwa dawa kwa wakati? Ahsante.

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, Mbunge wa Jimbo la Msalala, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya baadhi ya wateja wa bima kukosa dawa kwenye baadhi ya vituo vyetu ni kweli imekuwepo, lakini kwa taarifa ambazo tumeendelea kuzifanyia kazi, kasi ya ukosefu wa dawa kwenye vituo vyetu imeendelea kupungua. Hata hivyo, maelekezo ya Serikali yaliyotolewa ni kwamba, lazima vituo vyetu vyote na hospitali zetu zote na zahanati ziwe na dawa za kutosha kwa angalau asilimia 95 ya dawa zote muhimu. Hivyo, wateja hao wa bima wataendelea kuboreshewa upatikanaji wa dawa katika vituo vyetu ili kuepusha na changamoto ya kukosa dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wazo la kuwaunganisha na maduka ya binafsi; Serikali yenyewe tumeweka mkakati kwamba hatuna sababu ya kuweka kigezo cha kuongeza maduka binafsi wakati vituo vyetu vina uwezo na vinalazimika kuweza kuwa na dawa za kutosha. Kwa hiyo njia sahihi sisi ni kuimarisha upatikanaji wa dawa kwenye vituo vyetu badala ya kupeleka kwa maduka binafsi kwa sababu kwa kuimarisha dawa hizo katika vituo, hata wale ambao hawana bima pia watanufaika na utaratibu huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili kuhusiana na changamoto za upatikanaji wa dawa za wakati na hasa kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD); ni kweli kumekuwa na changamoto hiyo na Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa maelekezo wiki iliyopita kwamba MSD lazima wajipange kuhakikisha dawa zote zinapatikana kwa wakati na kuhakikisha kwamba vituo vyetu vinapata dawa kupitia MSD. Kwa hiyo suala hilo tunalifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mshitiri, ni kweli tulikuwa na mshitiri mmoja katika mkoa, lakini tulishatoa maelekezo kwenye mikoa yote kuongeza idadi ya washitiri, kuwa na angalau washitiri wawili, lakini hatua ya kwenda washitiri ngazi ya halmashauri bado tunaona haitakuwa na tija sana. tukishakuwa na washitiri ngazi ya mkoa ambao wana-supply vizuri, uzoefu unatuonesha tutakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Name

Deodatus Philip Mwanyika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Primary Question

MHE. IDDI K. IDDI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatoa vifaa tiba na dawa za kutosha kwenye vituo vya afya na zahanati zote katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala?

Supplementary Question 2

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Jimbo la Njombe Mjini tuna vituo viwili vya afya ambavyo vimejengwa kwa nguvu za wananchi na mapato ya ndani. Vituo hivi vimetembelewa na Mawaziri karibu wote wa TAMISEMI. Nipende kuuliza; ni lini sasa vituo hivi ambavyo viko tayari kwa asilimia 100 vitapata vifaa na watumishi ili viweze kuanza kutoa huduma kwa wananchi? Ahsante.

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deo Mwanyika, Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mwanyika kwa kuwasemea kwa ufasaha sana wananchi wa Jimbo la Njombe Mjini na kwa kweli hoja hii ameizungumza hapa zaidi ya mara mbili na sisi kama Serikali tumhakikishie tulishachukua hoja hii kwa ajili ya kupeleka vifaatiba kwenye vituo vile viwili vya afya, lakini pia kufanya mpango wa kupata watumishi pale na fedha tayari ziko MSD.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachosubiri ni manunuzi ya vifaatiba hivyo ili viweze kupelekwa kwenye Jimbo la Njombe Mjini. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili linafanyiwa kazi. Ahsante.