Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Shabani Omari Shekilindi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lushoto

Primary Question

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza: - Je ni lini Serikali itapeleka Watumishi wa kada ya Ualimu na Afya katika Wilaya ya Lushoto?

Supplementary Question 1

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza namshukuru Waziri kwa majibu yake mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ina Shule za Msingi 163 na Shule za Sekondari 53. Jumla ni shule 216 na watumishi ambao wapo pale kwenye shule ya msingi na sekondari mwaka 2006 ambao ni asilimia kama 40. Kuna upungufu watumishi 1,958: -

Je, Serikali ina mpango gani wa haraka kupeleka walimu 1,958 kada ya uwalimu katika Wilaya ya Lushoto ili kuendeleza taaluma ya Wana-Lushoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Halmashauri ya Lushoto ina Hospitali ya Wilaya moja na vituo vya afya na zahanati 68, lakini watumishi walioko pale ni 335. Kwa hiyo, kuna upungufu wa watumishi 763. Hiyo ni idadi kubwa sana. Kwa hiyo, ni asilimia kama 35: -

Je, Serikali ina mpango gani wa dharura kupeleka watumishi wa kada ya afya 763 katika Halmashauri ya Lushoto ili kunusuru kuokoa maisha ya wananchi wa Lushoto hasa akina mama wajawazito, watoto na wazee? Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya watumishi wa Sekta ya Afya na Sekta ya Elimu iko nchini kote na Serikali imechukua hatua. Kwanza hatua ya kufanya tathmini ya upungufu wa watumishi katika sekta zote, lakini pili katika mwaka wa fedha uliopita zaidi ya watumishi 9,000 waliajiriwa, lakini pia kupelekwa katika halmashauri hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa ambayo imefanyika, tumefanya tathmini kwa kuweka mpangilio na kutambua mikoa na halmashauri zenye upungufu mkubwa zaidi ikilinganishwa na mikoa na halmashauri nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna halmashauri ambazo ndani ya mkoa husika zina upungufu mkubwa ikilinganishwa na halmashauri ndani ya mkoa huo huo. Tumetoa maelekezo Makatibu Tawala wa Mikoa kufanya internal redistribution ya watumishi ndani ya mkoa ili halmashauri yenye upungufu mkubwa ndani ya mkoa ipate watumishi kwanza ndani ya mkoa. Pili, tunakwenda kwenye ngazi ya mkoa kwa maana katika nchi nzima kuhakikisha ile mikoa yenye upungufu mkubwa zaidi inapata kipaumbele kwenye ajira zinazofuata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Shekilindi kwamba kwenye ajira zinazofuata halmashauri yake itatoa kipaumbele cha hali ya juu kwa sababu ya upungufu huo ili kuhakikisha Walimu na watumishi wa sekta ya afya wanapata huduma bora. Ahsante sana.

Name

Emmanuel Lekishon Shangai

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Primary Question

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza: - Je ni lini Serikali itapeleka Watumishi wa kada ya Ualimu na Afya katika Wilaya ya Lushoto?

Supplementary Question 2

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro ni moja ya halmashauri ambazo watumishi wanahama sana na kwa mwaka jana tu watumishi zaidi ya 93 wamehama. Pia watumishi waliohamia ni 14 tu. Kwenye ajira iliyofanyika mwezi Juni, 2021, watumishi 11 ambao waliajiriwa wakiwa na ajira nyingine baadaye Serikali iliwarudisha, lakini hakuna watumishi wengine walioletwa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi wengine ambao wanataka kuhamia Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro hawapewi nafasi ya kuhamia kutoka kwenye halmashauri zao. Je, watumishi watapelekwa lini kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro ili waweze kuhudumia wananchi? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Ngorongoro, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi wanaopangiwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa wanapangiwa kulingana na taratibu na miongozo na kanuni za utumishi wa umma, lakini wanawajibika kufanya kazi katika maeneo yale isipokuwa wakiwa na sababu za msingi sana za kuomba uhamisho na sababu hizo mara nyingi ni zile za kiafya na baadhi ya sababu ambazo zinakubalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeweka mkakati wa kuhakikisha kwamba watumishi wengi ambao wanapangiwa hasa maeneo ya vijijini hawahamishwi na hivi sasa uhamisho kutoka ngazi ya Halmashauri vijijini kwenda kwenye Manispaa na Majiji umesitishwa ili kuhakikisha kwamba watumishi wengi walioko katika maeneo hayo wanaendelea kubaki pale ili kutoa huduma kwa wananchi. Hii itatuwezesha kuondokana na wimbi la watumishi kuhama kutoka halmashauri za vijijini kwenda mijini kama ilivyo Ngorongoro. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba suala hilo lilishafanyiwa kazi na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, mkakati ni kwamba Halmashauri ya Ngorongoro ni moja ya halmashauri zenye upungufu wa watumishi na itapewa kipaumbele mara ajira zitakapopatikana ili kuweza kupunguza pengo la upungufu wa watumishi katika halmashauri hiyo. Ahsante.