Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Luhaga Joelson Mpina

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisesa

Primary Question

MHE. LUHAGA J. MPINA Aliuliza: - (a) Je, ni sababu gani zilizopelekea kuchelewa kukamilika kwa ujenzi wa Bwawa la kufua umeme wa maji la Julius Nyerere? (b) Je, kwa nini Mkandarasi ameshindwa kujaza maji kwenye Bwawa kufikia tarehe 15 Novemba, 2021 kama ilivyokuwa imekubalika? (c) Je, ni hatua gani zimechukuliwa kutokana na ucheleweshwaji huo?

Supplementary Question 1

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijauliza swali langu la nyongeza nimeshindwa kujizuia kumpongeza Dkt. Tulia Ackson kwa kuchaguliwa kwa kura zote kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mwenyezi Mungu ambariki ili atekeleze haki za Watanzania hapa Bungeni. Baada ya hayo, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa majibu haya yaliyotolewa, mrai wetu huu wa kufua umeme wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere hauwezi kukamilika kama mkataba ulivyosema. Tulipokuwa kwenye Kamati ya Bajeti mwezi wa 11 Waziri alikuja mbele ya Kamati akaieleza kwamba sababu za mradi huu kuchelewa ni Mkandarasi kukaidi dizaini iliyowekwa na wataalam ya kujenga mahandaki matatu kwa ajili ya kuchepusha maji, lakini badala yake alijenga handaki moja, jambo ambalo lilimfanya achelewe sana kukamilisha kazi hiyo, kwa hiyo ndiyo sababu kubwa ya msingi; na sababu za UVIKO-19 zilikataliwa; na majibu haya yako kwenye Hansard za Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tena wamekuja na majibu mengine, wanasema kwamba ni kuchelewa kwa mitambo ya kubebea ile milango ya vyuma (hoist crane system), ndiyo iliyochelewa kufika na mradi huu kuchelewa kwa sababu ya UVIKO-19.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu majibu haya yanakanganya, kwenye Kamati chini ya Hansard waliyakataa majibu hayo kwamba hayana ukweli wowote na wakasema kwamba majibu sahihi ni kwamba huyo alikuwa mzembe na kwamba watam-penalize kwa ucheleweshaji atakaoufanya wa kuchelewesha mradi huu ambao unacheleweshwa na Watanzania. Sasa Mheshimiwa Waziri atuambie; Kamati ni sehemu ya Bunge, na hapa wamekuja na majibu mengine, na ushahidi wa Hansard upo. Nini majibu ya Serikali ya kuchelewesha mradi huu, kwa sababu majibu mawili tayari yametolewa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni kuhusu katakata ya umeme inayoendelea na mgao wa umeme unaoendelea hivi sasa. Mwanzo tulielezwa kwamba sababu ya mgao wa umeme unaoendelea sasa hivi ni kwa sababu ya matengenezo ambayo hayakufanyika kwa miaka mitano, ndiyo maana wako kwenye maintenance. Baada ya muda mfupi tena tukaambiwa kwamba ni kwa sababu ya mabwawa yanayotumika kufua umeme kukauka na yamekauka kwa sababu ya mifugo pamoja na ukaidi wa binadamu. Sasa hivi tena, wakati huo huo TANESCO nao wanasema kwamba hakuna mgao wa umeme, baadaye TANESCO wanatangaza mgao wa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hebu tuelezwe na Serikali; kwa sababu suala la katakata ya umeme na mgao wa umeme hivi sasa linaathiri sana Watanzania; viwanda vinafungwa, wananchi wako kwenye dhiki kubwa, huduma za afya zimevurugika, huduma za maji zimevurugika. Kwa ujumla Taifa liko kwenye hali ngumu ya ukosefu wa umeme…

MWENYEKITI: Umeeleweka Mheshimiwa, umeeleweka.

MHE. LUHAGA J. MPINA: …tupate majibu sahihi ya Serikali ni nini kinachosababisha hali hii ya kukatikakatika kwa umeme kuendelea?

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nianze na swali la kwanza, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, mradi kwa mujibu wa mkataba unatarajiwa kukamilika tarehe 14 Juni, 2022. Wazungu wanasema do not cross the river before you reach there. Muda utakapofika kama mradi hautakamilika hatua za kisheria za kimkataba zitachukuliwa kwa aliyesababisha ucheleweshaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, lilikuwa linajitegemea, liliulizwa kwa nini maji hayakujazwa kufikia mwezi Novemba na sababu za kueleza kwamba cranes na milango vilichelewa kwa sababu ya UVIKO ni sababu pekee ya kuchelewesha kuziba diversion channel iliyokuwa inachepusha maji. Kwa hiyo maelezo hayo hayahusiani na mradi mzima, kwamba mradi umechelewa. Kama nilivyosema, muda wa kukamilisha mradi bado haujafika na tutakapofikia mto tutaivuka kutokana na mazingira yatakayokuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba hakuna taarifa zinazokinzana, isipokuwa taarifa zote hizi kwa pamoja zitashughulikiwa kulingana na muda utakavyokuwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, kuhusu kukatika kwa umeme; kwanza niombe kutoa maelezo ya Serikali, kwamba TANESCO haikatikati umeme, hakuna mtu ambaye ameajiriwa kwa ajili ya kukata umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mifumo ya umeme ina-respond kulingana na mazingira. Kikubwa zaidi kinachotokea ni kwamba pale ambapo mitambo yetu inazidiwa na matumizi yenyewe automatically inakata umeme. Sasa tunapokwenda kuangalia tatizo ni nini, tukilibaini basi tunawasha. Miongoni mwa tatizo ambalo limekuwa likitokea ni kwamba, mara nyingi mitambo inapokuwa imepata mzigo mkubwa ikakata umeme na wale watumiaji nao wenyewe wanazima vifaa vyao.

Kwa hiyo sisi tukirudi kwenye mtambo wetu tukawasha unakubali kuwaka kwa sababu mitambo inakuwa haipo. Sasa wale wenzetu wakiwasha tena inakata tena. Kwa hiyo pengine inaonekana kama kuna mtu anakata na kuwasha, lakini ni system yenyewe ina-respond. Tunachokifanya ni kuhakikisha kwamba tunaongeza nguvu zetu za mitambo ili kuweza ku-capture sasa mahitaji tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kidogo suala la kwamba tulisema maji, sasa tukasema gesi. Ni kwamba tulitarajia kuwa kwenye marekebisho ya mtambo yetu ya kufua gesi ambayo inazalisha sehemu kubwa sana ya umeme hapa nchini tuiongeze kwa sababu sasa tuna uwezo wa kuongeza megawatt takriban 290, twende tukarekebishe kwenye visima vyetu vya gesi ili sasa tuweze kupata gesi nyingi zaidi kwa sababu ya kutokuwa na hali nzuri ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme. Ule mgao au matarajio makubwa ya mgao tuliodhani tutakuwa nao hatutakuwa nao; na sababu kubwa za kutokuwa na mgao huo ni tatu. Jambo la kwanza, tumekaa pamoja na wataalam, kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwamba mgao usiwe mkali kiasi kile, tukabaini kwamba tunaweza tukapata ile gesi iliyokuwa kwa wenzetu wa PAET ambao ndio watakaokwenda kurekebisha mitambo yao, tukapitisha baadhi ya kiwango kidogo cha gesi kupitia mitambo yetu ya TPDC na hivyo kufidia upungufu wa gesi ambao tungeupata. Hiyo imekuwa ni sababu ya kwanza, kwamba lile pengo kubwa ambalo tungelipata kwa kutokuwa na gesi tutalipunguza kupitia gesi na kuichepusha kwa kupitia njia ya TPDC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo tunaliona, sisi sote ni mashahidi kwa sasa, hali yetu ya mabwawa imeanza kurudi katika hali nzuri na hivyo itaweza kutusaidia kujazia sasa kwenye maeneo ambayo yanatakiwa yapate umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, umeme ni supply and demand. Tulitarajia kwamba kutakuwa kuna mahitaji makubwa sana ya umeme. Kuna kitu kinaitwa load flow analysis. Yulipoifanya load flow analysis tulibaini kwamba kile tulichokitaratjia kitahitajika sicho ambacho kitahitajika. Baada ya kuwa tunahitaji takriban 280 hadi 300 tunaona zitakazohitajika ni kama megawatt 100, ambazo katika mfumo wa kawaida huwa hazipo hapa na pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nitoe kauli ya Serikali, ule mgao ambao tuliutarajia utakuwepo kwa makali yale na ukubwa ule hautakuwepo na tutahakikisha kwamba watu wanaendelea kupata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho niseme, katika kipindi hiki ambako kutakuwa na mgao mdogo au kutokuwepo kwa umeme katika maeneo mbalimbali tutaitumia vizuri nafasi hiyo ili kufanya mambo kadhaa yanayoboresha mfumo wetu. Mojawapo ni kuhakikisha tunapunguza mzigo katika njia za umeme tunazoziita feeder, zile ambazo zimezidiwa kutoa sehemu moja kwenda sehemu nyingine, kukatia miti na mapori ambayo yamekuwa yakiangukia maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, kuboresha vituo vyetu vya kupoza umeme. Kama jana tulifanya cha Muhimbili, leo tunafanya pale Kunduchi na kesho kutwa watafanya pale Ubungo ili kuhakikisha kwamba tutakaporudi katika hali ya kawaida baada ya wiki moja ama mbili, tunarudi katika hali nzuri ambayo itakuwa bora kwa watu wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.