Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Nusrat Shaaban Hanje

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: - Je, ni kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kutenganisha Mahabusu/Magereza ya Watoto na Watu wazima ili kuwalinda Watoto dhidi ya vitendo vya ukatili wa kingono vinavyoweza kujitokeza?

Supplementary Question 1

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nami nitauliza maswali pamoja na majibu hayo, nitauliza maswali mawili ya nyongeza kutokana na majibu ya Mheshimiwa Waziri, pamoja na kwamba amezungumiza suala la Kanuni za Magereza ambazo zinataka watoto watengwe tofauti na watu wazima wanapokuwepo Mahabusu. Mlundikano wa Mahabusu kwenye magereza zetu hauruhusu jambo hilo ni kwa nini sasa Serikali isiongeze au isipeleke Maafisa Ustawi wa Jamii ambao watakuwa wanashughulika na Watoto wanapokuwa kule kwa sababu ni vigumu sana ku-monitor. Kwa mfano, Gereza la Segerea kuna mahabusu si chini ya mia moja watoto na Maafisa wapo wawili tu ME na KE. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili; kwa nini sasa Serikali isipitie upya kujua idadi ya watoto ambao wana kesi kwenye Mahakama zetu na kwenye Mahabusu zetu yaani kwa maana ya Magereza ili sasa ile sheria kwa jinsi ilivyowekwa na ni nzuri, lakini utekelezaji wake ni mgumu ni kwa nini sasa wasipitie upya ili kuhakikisha kwamba watoto hawa wanasaidiwa kwa sababu hali za watoto wetu kwenye Magereza zetu ni mbaya mno. (Makofi)

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje Mbunge wa Viti Maalum, nayo nayajibu kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, kama Mheshimiwa atarejea kwenye jibu langu la msingi atagundua kwamba kuna sehemu nimesema kutakuwa kuna Maafisa wa Ustawi ambao watakuwepo maalum katika magereza kwa ajili ya kusimamia haki na maslahi na kuwalinda watoto hawa. Kwa hiyo, kama changamoto ni Maafisa hawa kuwa kidogo basi nimhakikishie tutajitahidi Serikali kupitia Jeshi la Magereza ili kuona kwamba tunaongeza Maafisa hawa ili watoto wetu waweze kupata huduma nzuri za kuweza kusaidiwa na Maafisa hawa pamoja na kwamba kuna nafasi nyingine ya kushughulikiwa na wazee wao na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine Mheshimiwa amegusia suala la kwa nini isipitiwe upya sheria au tuone namna, nimwambie kwamba sheria hii kwamba ipo vizuri, lakini kwa kuwa na yeye ameshauri tuipitie upya basi tutakaa tutaipitia sheria hii ili kama kutakuwa kuna mapungufu basi tutajua namna ya kuifanyia marekebisho.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge pia aliuliza umuhimu wa kujua idadi ya kesi za watoto. Kesi zote zinazokwenda Mahakamani zinasajiliwa kwa namba, kwa hiyo kama atauliza swali mahsusi kwa Mahakama maalumu au kwa Gereza maalum idadi hiyo itapatikana kwa namba na kwa majina ya wahusika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili; Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 inaweka misingi ya kulinda maslahi ya mtoto. Kwa hiyo, kwa mtu aliyechini ya kizuizi cha magereza anapopelekwa mahakamani kama hapati huduma inayostahili akiwa magereza anayohaki ya kutoa hiyo hoja kwa Hakimu ambapo shauri hilo lipo mbele yake na maelezo ya kisheria kwenda kwa wanaosimamia hizo selo yakatolewa. Nninakushukuru. (Makofi)

Name

Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: - Je, ni kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kutenganisha Mahabusu/Magereza ya Watoto na Watu wazima ili kuwalinda Watoto dhidi ya vitendo vya ukatili wa kingono vinavyoweza kujitokeza?

Supplementary Question 2

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa ya kuuliza swali. Katika kulinda haki za watoto ni lazima au ni sharti tuzingatie wale watoto ambao unakuta hawana kesi, bali mama zao aidha wameenda wakiwa wajawazito au wamekamatwa ni mahabusu au mfungwa akiwa na mtoto ambaye yuko chini ya miaka mitatu.

Mheshimiwa Spika, katika Gereza la Segerea tumeshuhudia wamama wanakuja na watoto wao pale wa jinsia tofauti, lakini wanachangamana na watu wazima. Kwa hiyo, unakuta mtu mzima labda anataka kwenda kuoga anavua nguo, yuko hivi na mtoto yuko pale. Tunajua kwamba makuzi ya watoto ubongo wao ni kuanzia miezi sifuri mpaka miaka mitano. Kwa hiyo, unakuta unam-affect kisaikolojia.

Mheshimiwa Spika, nataka kujua sasa, ni hatua gani Serikali inachukua kuhakikisha kwamba wale mahabusu au wafungwa ambao wamekwenda wakiwa wajawazito, wamejifungua wakiwa Magereza au wameenda na watoto wachanga, waweze kutengwa kwenye cell special ya akina mama wenye watoto au wajawazito wasiweze kuchangamana na hawa watu wengine? (Makofi)

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Matiko kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuna hatua nyingi ambazo huwa zinachukuliwa. Huo utaratibu upo na upo tangu zamani. Inawezekana tu labda kuna maeneo yeye ameyashuhudia, ameona kwamba watu wanachanganyika na wengine wanakuwa wanataka labda pengineā€¦ kama hivyo. Kikubwa nimwambie kwamba ziko hatua ambazo Serikali inazichukua ikiwemo ya kuwatenganisha ili sasa ikitokea hali kama hiyo, waweze kupatiwa msaada maalum. Ziko hatua nyingi tu ambazo tunazichukua kama Serikali na kama Jeshi la Magereza. (Makofi)