Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Michael Constantino Mwakamo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Vijijini

Primary Question

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza: - Je, ni Ranchi ngapi nchini zimeshawapokea wafugaji na kuwapatia nafasi ya kufuga kwenye Ranchi hizo kama Serikali ilivyotoa maelekezo?

Supplementary Question 1

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kwenye majibu ya msingi ya Mheshimiwa Waziri hajaeleza na wala hajaitaja Ranchi ya Ruvu iliyopo pale Vigwaza kama imeshatengwa, sasa kwa kuwa kuna migogoro mingi ya wakulima na wafugaji kwenye Mikoa ya Pwani na maeneo mengine ya jirani kama Wilaya ya Chalinze na Kibaha Vijijini; Je, Serikali haioni huu ni muda sahihi sasa kupanga na Ranchi ile ili kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji kwenye maeneo hayo?

Swali la pili; kwa kuwa Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba migogoro mingi ya wakulima na wafugaji inapelekea watu wengi kupata ulemavu wa kudumu na wengine kufariki na kwa sababu ipo Ranchi hiyo ninayoitaja ya Ruvu ambayo haijafanyiwa; Je, Waziri haoni kwamba ni muda sahihi wa kufika kwenye maeneo ya Mkoa Pwani hasa Wilaya hizo za karibu kuwaelimisha wafugaji wadogo kwenda kuomba na kupata utaratibu wa kukaa kwenye Ranchi hizo kuondoka kwenye Bonde la Ruvu ambalo lina migogoro? (Makofi)

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru na kumpongeza sana lakini pili kwanini Ranchi ya Ruvu haikutamkwa katika majibu haya. Ranchi ya Ruvu katika maelekezo ya muda mrefu uliopita ya Serikali haikupangwa kwa ajili ya vitalu vya muda mrefu. Ranchi ya Ruvu na Ranchi ya Kongwa hazikupangwa. Kwa hivyo, baadaye kwa utashi na maelekezo ya viongozi wetu wakuu na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutaka kuona tunatatua changamoto ndiyo uamuzi wa kukata vitalu vya muda mfupi ukafanywa kwa hivyo Ranchi ya Ruvu ikapangiwa ikatwe vitalu jumla ya 19 na hivi sasa ninavyozungumza jumla ya Ng’ombe zaidi ya Elfu Tisa katika vitalu hivi vidogo vidogo vilivyopo katika eneo nzima la Ranchi Ruvu vimeshagawiwa kwa wafugaji, hili ni jambo la kwanza.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni namna ya kuweza kuwatoa wale wafugaji walioko katika maeneo ya Bonde la Mto Ruvu na labda kuwapa nafasi huku. Serikali jambo hili inalifanyia kazi siyo peke yake katika Mto Ruvu lakini vilevile na mito mingine kama Kilombelo, Ruaha na mingineyo. Maelekezo ya Serikali ni kwamba iko Kamati ya Mawaziri Nane inayofanya tathmini ili tutakapotoka na majawabu, tutatoka na majawabu ya pamoja yatakayokwenda kutatua kabisa tatizo hili la muda mrefu la wafugaji, wakulima na watumiaji wengine wa ardhi. Ahsante sana. (Makofi)

Name

Ridhiwani Jakaya Kikwete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chalinze

Primary Question

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza: - Je, ni Ranchi ngapi nchini zimeshawapokea wafugaji na kuwapatia nafasi ya kufuga kwenye Ranchi hizo kama Serikali ilivyotoa maelekezo?

Supplementary Question 2

MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, nami naomba niulize swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri wa Mifugo.

Mheshimiwa Spika, zaidi ya jumla ya hekta 2,208 zimegawiwa kutoka kwenye Ranchi ya Ruvu kwenda kkwetwa wanavijiji vinavyozunguka au katika Halmashauri ya Chalinze vikiwemo vijiji vya Kindogonzelo, Kitonga, Magulumatali, Vigwaza na Milo. Je, ni lini Serikali inakuja kutukabidhi vipande hivyo vya ardhi kwa ajili ya wananchi wetu sasa kuweza kugawana ili kuweza kutengeneza utaratibu mzuri wa kufuga. Ahsante. (Makofi)

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa
Spika ahsante sana umetupa elimu nakushukuru.

Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali zuri la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Chalinze Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Mrisho Kikwete kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwamba tumetenga hekta 2,208 hii ni kwa sababu ya lile jibu la msingi nililolitoa lililoulizwa na Mheshimiwa Mwakamo la kuondosha migogoro kati ya wakulima na wafugaji ni moja ya jitihada za Serikali na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Spika, tayari hatua za mwanzo za kiutawala ndani ya Wizara zimeshafanywa, vimeshapimwa na kutengwa maeneo haya, hatua inayofuata sasa ni kwenda kuwakabidhi Halmashauri ya Chalinze na Kibaha na hasa Jimbo la Chalinze, Jimbo la Kibaha Vijijini na Jimbo la Bagamoyo. Mara tu baada ya Bunge Wizara itakuwa iko tayari kabisa kuhakikisha kwamba sherehe hizi za kwenda kuwakabidhi na waweze kujipangia matumizi zinakwenda kufanyika. Ahsante sana. (Makofi)