Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Jacquline Andrew Kainja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Zahanati katika Kata ya Ng’ambo iliyopo Tabora Mjini?

Supplementary Question 1

MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwamba na wewe umeweza kuona hili swali halijajibiwa na mimi nimegundua hivyo, lakini nimpongeze Waziri kwa majibu mazuri yanayoonyesha namna gani Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mama Samia Suluhu Hassan imeendelea kupanga bajeti kuendelea kuhakikisha maboma ambayo yanatakiwa kukamilishwa yakamilike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba tu nipatiwe majibu mazuri, ambayo yanaendana na swali langu ili niweze kuridhika sasa kwamba ni lini Serikali inaweza ikaona kuna mpango mzuri kwenye hizi Kata ambazo ni kubwa hazina zahanati ili wananchi hawa waweze kupata zahanati na siyo kwamba kuna maboma hakuna hata hayo maboma ambayo yanatakiwa kukamilishwa yaani ni ujenzi mpya, Serikali ina mpango gani na njia ipi madhubuti kuhakikisha kwamba Kata ambazo ni kubwa mfano, Kata hii ya Ng’ambo ambayo iko Tabora Mjini na zingine nyingi ambazo sijaziainisha zinaweza kupata ufumbuzi huo? Ahsante sana. (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrea, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwa sasa Mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwanza tunamaliza ujenzi wa Vituo vya Afya kwenye Tarafa zote nchini. Tangu uhuru tulikuwa tuna Tarafa 570 na tulikuwa na Tarafa 363 tu pekee ambazo zilikuwa na Vituo vya Afya na katika Awamu ya sasa hivi tulikuwa na Vituo vya Afya kama 207 ambavyo Serikali tayari imeshapeleka fedha kwa awamu mbili ambazo nafikiri kila Mbunge anazo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tukija kwenye level ya zahanati kwa kila Kijiji lengo la Serikali ambalo tumeliweka na ndiyo maana nimejaribu kuelezea hapa fedha ambazo tumezitenga ni kwa ajili ya kwenda kumalizia zahanati ambazo zimeanzishwa na nguvu za wananchi na nyingine zimeanzishwa na mapato ya ndani ya Halmashauri na ndiyo maana kwenye swali hili la msingi lilipokuwa linaulizwa, tumemshauri Mbunge wa Jimbo na Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Tabora kwamba, hamasisheni wananchi mkishirikiana na vyanzo vya ndani muanze ujenzi ili sisi kutoka Serikali Kuu tulete fedha kwa ajili ya kumalizia hiyo zahanati.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ukisema kwamba tutajenga zahanati vijiji 12,000 kwa wakati mmoja kwa sasa hivi hatuwezi kudanganya kwenye hilo, ukweli wetu ni kwamba tunamaliza Vituo vya Afya Tarafa zote, tunamaliza Hospitali katika Halmashauri zote halafu kwenye ngazi ya vijiji tutapeleka fedha, kwenye vijiji vyote ambavyo zahanati wananchi wamepeleka nguvu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hilo ndiyo jibu letu, ahsante. (Makofi)