Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hassan Seleman Mtenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtwara Mjini

Primary Question

MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itashughulikia urejeshwaji wa Fedha za Wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini ambao walijiunga na Pride kwa ajili ya kupata mkopo?

Supplementary Question 1

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa shauri hili lilizungumzwa toka mwaka 2018 na Ofisi ya Msajili Hazina wakapewa jukumu la kulisimamia tuna miaka zaidi ya mitatu sasa hivi imeshapita: Je, ni lini tutaelezwa kwamba shughuli hii itakuwa imemalizika?

Mheshimiwa Spika, swali la pili: Wananchi wa Mtwara ambao wanadai zaidi ya shilingi milioni 250: Ni lini Mheshimiwa Waziri atakuja kuzungumza na wananchi wa Mtwara ili waelewe mustakabali mzima wa fedha zao ambazo zimepotea mpaka sasa hivi haijulikani watalipwaje? (Makofi)

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mtenga kwa kufuatilia sana masuala ya wananchi wake wa Jimbo la Mtwara. Mara kwa mara akija ofisini anafuatilia masuala yanayohusu wananchi wa Mtwara katika sekta mbalimbali na anatumia vizuri uzoefu wake wa kuwa Katibu wa Mkoa wa Chama na maeneo tofauti tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la kwanza kwamba jambo hili limechukua muda, ni kweli lilichukua muda kwenye hatua za awali kwa sababu lilipokuwa kwenye ngazi za kimahakama, hatua nyingine hizi zisingeweza kufanyika, lakini baada ya kuwa shauri hilo limeshaamuliwa na Mahakama, kwenye hizi hatua nyingine, zinaweza zikafanyika kwa haraka.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie kwamba wananchi wake watapata uhakika haraka tu. Naamini nami nitapata uhakika kutoka kwa Msajili wa Hazina ili niweze kumuarifu makadirio hasa ya muda aliyokuwa anataka aujue kuwa ni lini?

Mheshimiwa Spika, hili la pili kwa ridhaa yako, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tukishamaliza Bunge tutapanga utaratibu ili tuweze kuwaandaa wahusika hao, nami niweze kufanya ziara kuweza kuwaelimisha nikiwa tayari na majibu ya uhakika kutoka kwa Msajili wa Hazina kuhusu kipindi ambacho kitatumika kuweza kuhakikisha kwamba hatua hizo za kiutawala zitakuwa zimekamilika.

Name

Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itashughulikia urejeshwaji wa Fedha za Wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini ambao walijiunga na Pride kwa ajili ya kupata mkopo?

Supplementary Question 2

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba tu Serikali inieleze, inakuwa wapi mpaka matatizo haya yanatokea? Ukizingatia kwamba watu wengi wanaoweka na kukopa kwenye hizo taasisi ni watu wa kipato cha chini; Serikali inakuwepo inaona jambo linaendelea mpaka linakua, wanakuja kunyang’anya ama kuchukua, watu wanaathirika. Kumbuka mambo ya DECI, ilikuwa hivi hivi. Leo PRIDE iko hivi hivi. Nataka nijue, Serikali inakuwa wapi mpaka inaacha mambo haya yanafikia hapo wananchi wanaathirika ambapo wengi wao ni wakipato cha chini? Nakushukuru. (Makofi)

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tunza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kazi ya Serikali kutoa miongozo na kusimamia hizi taasisi. Kwa upande mmoja Serikali ni pamoja na wananchi inapofika masuala ya kifedha kwa sababu taasisi zote za kifedha zinakuwa na mikutano yao ya kila mwaka, lakini mara nyingi sana wananchi wetu wakishaweka fedha kwenye maeneo haya ya kibenki, hawafuatilii sana mienendo ya kifedha kwenye maeneo walikoweka. Wakati Serikali inafanya yale mambo ya kiutawala, ni wajibu wao pia kuangalia mwenendo wa taasisi yao ambako wameingia mkataba na taasisi husika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, rai yangu, kwanza wananchi watumie taasisi za kifedha ambazo hazina mashaka mashaka. Tuna mabenki yanaendelea kuenea katika maeneo mengi, watumie mabenki ambayo yako accredited na Serikali, wasitumie taasisi zile ambazo zina mashaka mashaka, lakini hata taasisi zile ambazo ziko accredited kama ambavyo masharti ya kifedha yanasema, wanapokuwa na mikutano ya mwaka ya taasisi hizo, wachukulie umuhimu kufuatilia mienendo ya taasisi hizo ambazo wameingia mkataba nazo.