Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Longido

Primary Question

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaboresha Miundombinu ya Minada ya Mifugo kwa kujenga mazizi ya kisasa, vyoo na ofisi za kupokea tozo na kodi za mnada?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo ya nyongeza, lakini kabla sijauliza maswali yangu madogo kuna kumbukumbu naomba kuiweka kwa usahihi kuhusiana na suala zima la ushuru na tozo za minada ya mifugo katika Wilaya ya Longido tulipata heshima kubwa ya kutembelewa na Rais kama wiki mbili zilizopita tarehe 18 na kuna Waandishi wa Habari ama wamempa Rais habari ambayo siyo sahihi, baada ya kufungua kiwanda kikubwa cha nyama ambacho kimezinduliwa kilijengwa na wawekezqji kwa zaidi ya shilingi bilioni 17 akapata taarifa kwamba inazalisha chini ya kiwango kwa sababu Halmashauri ya Wilaya ya Longido inatoza kodi na ushuru mkubwa unaosababisha wafugaji kupeleka mifugo Kenya.

Mheshimiwa Spika, kumbe Halmashauri ya Wilaya ya Longido haijawahi kuchukua hata shilingi katika kile kiwanda tangu kianze na kodi zinazokusanywa zinaenda Wizarani na taarifa hiyo ilitoka katika taarifa ya Ikulu wananchi wa Longido walikereka sana na hiyo kauli, nikaomba sasa basi nitoe hapa wasikie kwamba nimewasema na ndipo sasa niulize maswali yangu mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza kwa kuwa viwanda hivi vilivyojengwa nchini hivi karibuni vya kisasa ikiweko hicho cha Eliya Food Products kilichoko Longido zinapata malighafi pungufu kulingana na uwezo wake.

Je, Serikali imeweka mpango na mkakati gani wa kuhakikisha kwamba malighafi ya kulisha hivyo viwanda inapatikana?

Swali la pili; kwa kuwa Wilaya ya Longido ni Wilaya ya wafugaji kwa asilimia 95 na afya ya mifugo inategemea kwa asilimia kubwa upatikanaji wa maji hasa maji ya mabwawa - malambo yale.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuyafufua mabwawa na malambo yaliyofukiwa na udongo kwa miaka mingi katika Wilaya ya Longido na hasa Kiseriani ambapo maji kidogo yaliyobaki mwaka huu yanakwamisha wanyamapori? Juzi nimeweka post ya Pofu aliyekuwa anatolewa na Wamasai amekwama katikati ya lile bwawa pamoja na binadamu, sisi tunatumia maji ya mifugo na binadamu pia.

SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Kiruswa..

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Wizara ya Maji inawahusu mtatusaidiaje kufufua mabwawa yaliyofukiwa katika Wilaya ya Longido?

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Stephen Kiruswa Lemomo Mbunge wa Longido kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza linahusu mkakati wa Serikali wa kuhakikisha viwanda hivi vinapata rasilimali, tumejipanga juu ya kuhakikisha tunaweka utaratibu wa unenepeshaji kupitia vikundi na kwa watu binafsi. Mkakati wetu ni kuwa na wanenepeshaji wasiopungua 500 nchi nzima ambao miongoni mwao watakwenda kuingia mikataba na viwanda, kwa mfano kiwanda cha Eliya Foods kimeshaanza utaratibu huo wa kuwa na suppliers ambao wanawapa mikataba kwa ajili ya kupeleka ng’ombe pale kiwandani na hii itatusaidia sana hata katika lile jambo la mwanzo alilolizungumza la tozo kwa kuwa utaratibu tuliouweka wale wote watakaokuwa na mikataba na viwanda vinavyofanya uchakataji kwa ajili ya export tutawaondoshea baadhi ya tozo hizo ili kurahisisha vile viwanda viweze kupata malighafi kwa urahisi na kwa bei nzuri.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni hili la maji katika bajeti ya mwaka 2021/2022 tunayo malambo ambayo tunayatengeneza kwenye maeneo mengine ya nchi hii, lakini nafahamu Longido uko mradi mkubwa wa maji ambao unakwenda kuwahudumia wananchi wa Longido. Tumekaa na wenzetu wa Wizara ya Maji na nimpongeze sana yeye Dkt. Kiruswa na timu nzima ya pale Longido Mkoani Arusha kwa kuwashawishi wenzetu wa Wizara ya Maji waweze kutoa matoleo ambayo yatatengeneza mabirika yahudumie mifugo na wakati huo huo yaweze kuhudumia wanadamu na sisi ndani ya Serikali tunaendelea na ushauriano ili kusudi jambo hili liweze kufanikiwa.

Mheshimiwa Spika, hivyo mradi ule mkubwa wa maji uliokwenda kuzinduliwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha kwamba uweze kuhudumia maji haya yaweze kuhudumia binadamu na mifugo pia. Ahsante sana.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa nilitaka niongezee jibu sehemu ndogo ili Mheshimiwa Mbunge ambaye anawasemea sana wananchi wa Longido aweze kulibeba hilo jibu. Wizara ya Fedha pia kushirikiana na Wizara ya Mifugo tunaangalia upya sehemu ya tozo ile ambayo tuliiweka ambayo inahusu pia sekta ya mifugo pamoja na maeneo mengine ambayo yamesababisha upande wa huku Serikali Kuu iweze kuongeza hiyo sehemu ambayo ameisemea, kwa hiyo naamini kwenye kikao hiki hiki kinavyoendelea tukiwa tumeshakamilisha Mheshimiwa Mbunge atarudi Longido akiwa na jibu lililosahihi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu sehemu ya kufufua bwawa tayari tumeshakamilisha makubaliano na Waziri wa Maji ambaye anafanyakazi nzuri sana, tumeshatoa fedha za kununua mitambo ya kuchimba mabwawa ambako kila ukanda wa nchi hii utakuwa na mtambo wake wa kuchimba mabwawa. Kwa hiyo kwa wafugaji hata kama wataamua kuchimba bwawa kila baada ya mazizi mawili Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wetu amesema wachimbe tu na wata-manage wenyewe kutoa maeneo ya kuchimba hayo mabwawa. (Makofi)