Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Angelina Adam Malembeka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Benki ya Wavuvi nchini?

Supplementary Question 1

MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri yanayotia moyo. Lakini katika sentensi yake tu ya kwanza amesema ile ni Benki ya Maendeleo ya Kilimo na mimi nazungumzia wavuvi.

Sasa ninataka kujua, je, ni vigezo gani vinavyotumika ili hao wavuvi waweze kupata mikopo katika hiyo Benki ya Kilimo?

Swali la pili; ninataka kujua, kwa kuwa wavuvi wengi bado hawajapata elimu kuhusiana na mikopo hiyo; Je, Serikali ina mpango gani wa kuzungukia wavuvi hao ili wapate elimu waweze kunufaika na mikopo hiyo? Ahsante.

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza kuhusu ni vigezo gani. Kwanza ni kuomba ama kama nilivyoeleza katika jibu la msingi, mtu mmoja ama kikundi, waombe kwa watoaji wa mkopo kwa maana ya benki. Tunashauri vikundi, hasa vya ushirika kwa kuwa ni rahisi zaidi kulingana na sera yetu kupata mkopo kisha benki watakapokuwa wameombwa wataeleza nini kimepungua na nini kinachohitajika ili mwombaji aweze kukamilisha utaratibu. Kwa hiyo namshauri Mheshimiwa Malembeka na wavuvi wote kutembelea katika mabenki mbalimbali na wanaweza kupata msaada wa kuelezwa ni nini hasa vile vigezo vinavyohitajika.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili la utoaji wa elimu ni endelevu na limekuwa likiendelea kufanywa wakati wote, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Malembeka ya kwamba tutaendelea kufanya kazi hii ya kutoa elimu kwa wavuvi wetu juu ya uvuvi endelevu katika Taifa letu na wenye manufaa. Ahsante sana. (Makofi)