Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Primary Question

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza: - Je, ni lini Serikali itabadilisha Muundo wa Utumishi wa Maafisa Utumishi/Utawala na Walimu ili waweze kuanza na Daraja E kama ilivyo Kada ya Sheria na nyinginezo?

Supplementary Question 1

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza naipongeza Serikali kwa nia hiyo njema ya kutamani kuboresha stahiki za watumishi, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa sasa tathmini imeshafanyika tangu mwaka 2015/2017 ya kufanya marekebisho ya muundo na mishahara ya watumishi: Je, ni lini sasa Serikali itatekeleza jambo hili?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kumekuwa na ucheleweshaji mkubwa sana wa mafao ya watumishi wanapostahili: Ni nini kauli thabiti ya Serikali kuwahakikishia watumishi wanapostahili watapata stahiki zao/mafao yao kwa wakati? (Makofi)

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Saashisha Elinikyo Mafuwe Mbunge wa Hai kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nitoe pongezi zangu kwa Mbunge wa Hai, Mheshimiwa Saashisha kwa kuwa anafuatilia sana masuala ya kiutumishi hasa yale ya watumishi katika jimbo lake na yale ambayo yanahusu wastaafu wanaotoka katika Wilaya ile ya Hai na jimboni kwake.

Mheshimiwa Spika, sasa nikienda kwenye kujibu swali lake la kwanza, Serikali tayari ilishaanza mpango wa kuweza kufanyia kazi ile tathmini iliyofanyika 2015/2017. Tayari kuna kada ambazo zilishafanyiwa kazi ambapo kwa zoezi lililofanyika mwaka 2015, kada ya Wahasibu, Internal Auditors na hawa washika fedha; kada hizo zilikuwa zinatofautiana sana katika ngazi ya mshahara, lakini ukiangalia elimu wanayosoma, ilikuwa ni moja. Kwa hiyo, tayari Serikali imeanza kufanyia mpango huo.

Mheshimiwa Spika, vile vile mwaka 2017 ilifanyika tathmini ya Watumishi wa Umma wote, kuangalia ulinganifu ikiwemo kwenye ma-engneer ukiangalia katika wanasheria na kadhalika. Sasa katika utekelezaji kama unavyofahamu Serikali itatekeleza pale tu kwa uwezo wa kibajeti katika kulipa mishahara. Kama tunavyoona jitihada zinazofanyika na Serikali za kuboresha uchumi wetu chini wa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan, uchumi wetu ukiboreka, basi tutafanyia kazi na kuboresha maslahi ya watumishi wetu.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili, Watumishi wa Umma inatakiwa inapofika mienzi sita kabla ya kustaafu, tayari waanze na kujiandaa na nyaraka mbalimbali. Sasa changamoto imekuwa ikijitokeza unakuta mtu ajira yake ya kwanza alianzia Halmashauri ya Kongwa, lakini anapokuja kustaafu, anastaafia Ukerewe, tatizo linakuwa kwenye documentation. Halafu mtu anakuja kukumbushwa suala hili la Maafisa Utumishi limebaki mwezi mmoja, anapoanza kufuatilia barua yake ya ajira, iko Kongwa. Sijui alipata uhamisho kwenda Songea; akatoka akaenda kustaafia Ukerewe.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, utakuta changamoto kwenye documentation na mtu huyu hana nauli, ndiyo maana mafao yanachelewa, lakini tayari tumeanzisha mfumo wa HCMIS ambao utahakikisha taarifa zote za mtumishi zipo na zinaanza kutoa notification walau miezi sita kabla.

Mheshimiwa Spika, wakati Serikali tunafanyia kazi mfumo huu, nawaasa Maafisa Utumishi wote nchi nzima kuhakikisha wanaangalia records za watumishi wao wanaokaribia kustaafu wawape taarifa walau mienzi sita kabla, ili isije ikafika nauli imekwisha, anakaribia kustaafu kesho, ndiyo anakumbushwa aanze kutafuta taarifa zake. (Makofi)

Name

Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Primary Question

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza: - Je, ni lini Serikali itabadilisha Muundo wa Utumishi wa Maafisa Utumishi/Utawala na Walimu ili waweze kuanza na Daraja E kama ilivyo Kada ya Sheria na nyinginezo?

Supplementary Question 2

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Hili suala la wastaafu kwa kweli ni kero kubwa katika nchi yetu. Nashukuru majibu ya Serikali, lakini niseme tu Serikali inatakiwa kujitahidi kwenye jambo hili, kwa sababu wastaafu waliomaliza ku-document document zao ambao wapo kwenye maeneo, wanaolia, wanaokwenda kwenye maofisi, wana miezi sita, miaka tano, miaka minne, ni wengi kuliko ilivyo kawaida.

Kwa hiyo, Serikali itafute mfuko thabiti wa kuzingatia mambo haya ili watu waweze kupata fedha zao. Watu wanakufa wanadai fedha, kwa nini mtu ameitumikia nchi, halafu anakufa anadai fedha.

Mheshimiwa Spika, naiomba tu Serikali itengeneze jambo hili liwe nzuri zaidi.

Name

Dr. Pindi Hazara Chana

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri na Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma. Naomba niliambie Bunge lako Tukufu, Serikali ya Awamu ya Sita na hasa Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma baada ya kuingia na kugundua kwamba wakati mwingine ucheleweshaji wa mafao hayo ya wastaafu yanatokana na haya malimbikizo ya michango. Michango mingi ambayo inatakiwa ipelekwe na waajiri, imekuwa ikicheleweshwa kupelekwa kwa mazingira ya aina moja ama nyingine. Serikali imekuja na suluhu hiyo ya kutengeneza mfumo ambao utawasaidia wafanyakazi wote kutambua ni lini wanastaafu na haki zao zikoje?

Mheshimiwa Spika, ili kurahisisha sasa na upande wa pili wa mifuko, tumewaagiza na wameshatekeleza. Kwa mfano, Mfuko wa PSSSF wameshatengeneza mfumo ambao unaitwa PSSSF Kiganjani. Mfumo huo sasa umeshasambazwa na unaendelea kusambazwa kwa wanachama wote. Wanachama ambao wanakaribia kustaafu, wamekuwa sasa wakiwezeshwa kuzitambua haki zao kupitia kwenye mfumo na kuanza kuwasiliana na ofisi zote kabla ya muda kustaafu ili kupunguza hiyo kadhia ambayo imekuwa ikiendelea.

Mheshimiwa Spika, hivyo hivyo tumewahagiza Mfuko wa PSSSF na mifuko mingine, kabla ya muda wa kustaafu, wastaafu wote watarajiwa tumeanzisha sasa vikao maalumu mfuko kukutana na wastaafu watarajiwa kuwatambua na kuandaa mafao yao mapema na hivyo kadiri tunavyokwenda kadhia hii itakuja kuondoka na tunapenda wastaafu waweze kupata mafao yao kwa muda unaotakiwa. (Makofi)

Name

Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza: - Je, ni lini Serikali itabadilisha Muundo wa Utumishi wa Maafisa Utumishi/Utawala na Walimu ili waweze kuanza na Daraja E kama ilivyo Kada ya Sheria na nyinginezo?

Supplementary Question 3

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nimemsikiliza Mheshimiwa Waziri wakati anajibu, amesema moja ya changamoto ya kuchelewa kulipwa kwa wastaafu ni pamoja na waajiri kuchelewa kupeleka michango. Wakati jana nimeomba mwongozo, nimepokea message 165, wengine hawajalipwa kuanzia mwaka 2012; lakini kwenye Bunge la Bajeti Mheshimiwa Waziri aliji-commit kwamba atafanya ziara kwenye vyombo vyote vya habari kuhakikisha wanapeleka michango ili Waandishi wa Habari na watu wengine binafsi walipwe kwa wakati. Sasa nataka niulize, ni lini ataanza hiyo ziara ili Waandishi wa Habari michango yao ipelekwe ili na wenyewe wawe na uhakika, baada ya kumaliza kazi zao wapate stahiki zao? Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Pindi Hazara Chana

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, masuala haya ya haki ya wafanyakazi ni masuala yanayotakiwa kuangaliwa kwa utaratibu mzuri sana. Masuala haya hayafanani tu labda na maamuzi ya mtu, kuamua kukaa hapa, ukae na nani na ufanye nini? Hapana, ni lazima kuyatengenezea utaratibu madhubuti.

Mheshimiwa Spika, naomba kumwambia Mheshimiwa Mbunge, tumeshaanza hiyo kazi. Kazi ya kwanza tuliyoifanya ni kupata ushirikiano kutoka kwa Waandishi wa Habari, kutambua vyombo ambavyo vimekithiri kwa kutokulipa mishahara na mafao ya Waandishi wa Habari. Kazi hiyo, tumeshaitekeleza na baada ya hapo sasa ndipo tutakwenda kuanza ziara ya kukutana na vyombo hivyo. Huwezi kuanza tu kukutana nao kabla hujapata taarifa.

Kwa hiyo, naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge Serikali inafanya kwa utaratibu, inatengeneza mikakati kusudi utaratibu huo ukianza kuchukuliwa hatua, hatua hizo ziwe zimezingatiwa kwa mujibu wa sheria na utaratibu. (Makofi)