Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Catherine Valentine Magige

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. CATHERINE V. MAGIGE aliuliza: - Je, ni lini Serikali itamlipa Mkandarasi anayetengeneza kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Loliondo hadi Mto wa Mbu ili iweze kukamilika na kurahisisha maisha ya Wakazi wa Ngorongoro?

Supplementary Question 1

MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa barabara hii ya kutokea Wasso kwenda Mto wa Mbu ina kilometa 206, lakini kwa miaka minne barabara hii imejengwa kilometa 49 tu; na barabara hii imekuwa inaleta usumbufu mkubwa kwa wananchi wa Ngorongoro. Hivi juzi tu kuna mama amefia njiani akiwahishwa hospitali kujifungua na tumeona Mheshimiwa Mama Samia akitangaza utalii na barabara hii inahusu utalii. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara hii? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Kwa kuwa mkandarasi huyu anadai shilingi bilioni 21 na walimwongezea muda, alikuwa amalize kujenga barabara hiyo Oktoba, 2019: Je, hamwoni kwamba mnaingiza Serikali katika hasara ya kulipa penalty? (Makofi)

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa
Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Catherine kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kwamba Mkandarasi anadai shilingi bilioni 21; na anapokuwa amewasilisha hati ya madai, lazima kuna kazi ya kuhakiki madai yao yanafanyika. Kazi hiyo imeshafanyika na Juni mwaka huu 2021, Mkandarasi huyo amelipwa zaidi ya shilingi bilioni 12. Kwa hiyo, mchakato unaendelea, wakikamilisha uhakiki huko Wizara ya Fedha atalipwa fedha ili kazi iweze kuendelea. Mimi mwenyewe nimefika katika barabara hii na nilipata shida kweli barabarani, anachokisema ni kweli, ni barabara ngumu sana, tulipata pancha za kutosha, lakini Serikali imeweka nguvu barabara hii ikamilike.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la pili, barabara hii ni kweli ina urefu wa kilometa 206, inavyo vipande vinne. Kwa hiyo, tunaanza na hiki cha kwanza; kutoka Wasso kwenda Sale na twende mpaka Mto wa Mbu. Tuna- engage vyanzo mbalimbali kupata fedha ili barabara hii iweze kukamilika. Mheshimiwa Mbunge ambaye pia ni Naibu Waziri wa Serikali hii ya Awamu ya Sita tulikuwa pamoja na anajua tulifanya juhudi kubwa. Tukifanya mpango kumaliza barabara hii, itabadilisha uchumi wa wale watu wa Ngorongoro, itapeleka huduma za kijamii na pia itafungua milango ya watalii na pato la Taifa kwa ujumla wake litaongezeka katika eneo hili. Ahsante.