Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Leah Jeremiah Komanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Meatu

Primary Question

MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza: - Je, ni lini ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Kolandoto – Oldean Junction utaanza kwa kuwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ulishafanyika?

Supplementary Question 1

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali kwa kuonesha nia ya kuanza kuijenga hii barabara kwa sababu ni ahadi ya muda mrefu iliyoko katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipande cha kilometa 74 ipo mito minne ya Itembe, Chobe, Lyusa na Nkoma ambayo imekuwa inakwamisha kuleta tija ya daraja la Sibiti lililogharimu shilingi bilioni 34.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kutembelea kipande hicho na kuweza kuishauri Serikali kuanza kujenga madaraja kwa fedha iliyotengwa mwaka huu wa fedha unaoanza? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika barabara inayoiunganisha daraja la Sibiti kilometa 25 ambayo pia imetengewa fedha iko juu ya mbuga kali sana. Kujenga barabara hii inatakiwa ianze katika kipindi cha kiangazi. Ni nini kauli ya Serikali kuhusu kuianza barabara hii kama ilivyotengewa fedha mwaka 2021/2022? (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Meatu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Leah Komanya kwamba yale ambayo tumejadili sana ulivyokuja ofisini bado yanabaki kuwa hivyo hivyo na nitaendelea kuyaeleza hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Daraja la Sibiti ambalo lina barabara ya maingilio yenye urefu wa kilometa 25 nataka nimhakikishie Mheshimiwa Komanya na wananchi wa Meatu kwamba tayari mkataba umeshasainiwa na muda wowote barabara yenye urefu wa kilometa 25 unaanza kujengwa, lakini hautajengwa kwamba ni kilometa nusu Simiyu na nusu Singida bali tutajenga zaidi upande wa Singida ambako ndiko kwenye bonde kubwa kuhakikisha kwamba barabara hiyo inapitika.

Kwa hiyo, tayari muda wowote barabara itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami ambayo pia ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu madaraja aliyoyataja naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Meatu niko tayari kwenda kuyakagua kwa sababu ni barabara ambayo imeongelewa sana, lakini nimhakikishie kwamba tayari tumeshafanya design, kwa hiyo, kinachotegemewa sasa hivi ni kupata fedha ili tutakapoanza ujenzi basi tutasubiri pia na tutategemea ushauri wake pengine ikiwezekana tuanze kwanza kujenga madaraja hayo kabla ya kujenga barabara. Kwa hiyo, nitakuja kama alivyoshauri. Ahsante sana.