Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA aliuliza: - Je, ni kwa kiasi gani mifuko ya uwezeshaji kiuchumi iliyoanzishwa kwa lengo la kuwaondelea wananchi umasikini na kuwajengea uwezo wa kiuchumi imenufaisha wanawake wa kitanzania kutoka mikoa ya nje ya Dar es Salaam?

Supplementary Question 1

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na nashukuru sana Serikali kwa majibu mazuri. Sasa nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali haioni ipo haja ya kufanya tathmini ya mifuko hii ya uwezeshaji kwa kuzingatia muda mfuko ulipoanzishwa, jumla ya mikopo iliyotolewa, ruzuku na dhamana pamoja na hali ya marejesho. Na tathmini hii pia iangalie hasara na faida ili kwa kufanya hivyo, Serikali iweze kuja na mikakati ya kuimarisha utendaji wake na iwe na tija kwa maendeleo ya wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili ni kutokana na changamoto kubwa za ajira kwa vijana, je, Serikali haioni ipo haja sasa ya kuweka vipaumbele vya kutoa startup capital kwa wahitimu wa vyuo maana mara nyingi vijana hawa wanakuwa na bankable ideas lakini wanashindwa namna ya kupata mikopo, ruzuku na dhamana zenye riba na vigezo nafuu? (Makofi)

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA
NA AJIRA (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana kwa sababu amekuwa mfuatiliaji kwa wakati wote katika masuala haya yanayohusu maendeleo ya vijana lakini pia wanawake na Watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kuna haja kubwa ya kufanya tathmini ya muda kuhusiana na masuala ya ruzuku na dhamana ambazo zimekuwa zikitolewa kila wakati ili kuangalia kama inaleta tija. Katika hatua hiyo, Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa tayari tumekwishakuanza kufanya zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya mifuko yote 54 na ile mitatu ambayo ipo chini ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu tayari tumekwisha kuanza kufanya zoezi hilo ili kuweza kuangalia namna gani ambavyo itakuwa na tija zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ambayo baadhi ya hayo ambayo tumeyabaini, ukiacha kazi ya timu ambayo bado inaendelea, tumebaini kwamba katika fedha hizi nyingi zinatolewa wakati mwingine vikundi vinakuwa havijaunganishwa vizuri zaidi na tumeenda kwenye hatua ya kuona kwamba lazima sasa kuwe na tija ya kutoa mafunzo kabla ya kutoa mikopo hii. Vilevile kuweza kufanya na kuangalia yale maandiko ya mpango kazi au mpango wa biashara kwa maana ya zile business writeups ambazo zinazletwa kwa ajili ya wao kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hatua nyingine pia tunaangalia namna ya kuweza kutanua wigo wa kutoa mikopo hii au fedha hizi na uwezeshwaji huu kwa makundi mengi zaidi na kuona jinsi gani ambavyo inaweza ikaenda kwa mtawanyo kwa maana ya uwiano mzuri katika mikoa lakini pia katika Majimbo na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, tumebaini jambo jingine ambalo katika mikopo hii ambayo imekuwa ikitolewa, na tutakubaliana kwamba fedha hizi zimekuwa zikitolewa katika mifumo mbalimbali. Ukiangalia kwenye Halmashauri kuna ile 4:4:2 kwa maana ya fedha ambazo ni asilimia 4 kwa wanawake, 4 kwa vijana na 2 kwa watu wenye ulemavu. Fedha hizi zimekuwa zikitolewa nchi nzima lakini kwa sehemu kubwa utaona kwamba marejesho yamekuwa ni hafifu sana. Kwa hiyo, tulitegemea kwamba fedha hizi zikitolewa, vijana hawa waweze kuzifanyia kazi na wa-graduate waende kwenye hatua ambayo watawaachia wengine waweze kukopa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaenda kwenye hatua nyingine ambayo bado ipo katika hatua ya mashauriano kuona kama tutaweza kutoa asilimia 50 ya vifaa na 50 iwe fedha kwa ajili ya operational cost kwa sababu ili tuweze kama ikitokea wameshindwa kulipa, tumewapa trekta au mashine za kushona nguo ama tumewapa vifaa vitendea kazi labda mashine za kufyatua tofali na ilikuwa mkopo labda wa milioni 10; tukawapa milioni 5 gharama za mashine na milioni 5 nyingine wakapewa kama fedha taslimu maana yake ni kwamba hata wakishindwa kurejesha walau tunaweza tukarejesha ile mashine ya kufyatua tofali ikawasaidie vijana wengine kuliko sasa hivi mfumo wa returns umekuwa mgumu na halmashauri zimekuwa zikihangaika wakati mwingine kulazimika kuwapeleka mahakaman. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la Mheshimiwa la kuona namna gani ambavyo tunaweza tukatengeneza startup capital kwa wanafunzi wahitimu wa vyuo vikuu ni pamoja na mpango mzuri ambao tumekuwa nao katika Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu…

MWENYEKITI: Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri utajibu hapo kwa ufupi.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA
NA AJIRA (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Ni pamoja na mpango huu ambao tumeanza kuona bado lipo katika kuona namna gani ambavyo vijana wa vyuo vikuu tutawaingiza kwa programu tatu ambazo zipo. Kwa sasa tumeanza na programu ya uanagenzi ambayo kimsingi inatumika kwa wale ambao hawajamaliza chuo kikuu lakini tuna programu maalum ya internship ambayo tayari tunawachukua vijana hawa na kuwaunganisha kwenye maeneo ya ajira. Sambamba na hilo, tunatoa mafunzo pia na kuwasaidia kuweza kupata mikopo kwenye maeneo ya halmashauri lakini pia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana unaotolewa na Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hilo pia tumelichukua na tutalifanyia kazi, nakushukuru. (Makofi)