Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Kenneth Ernest Nollo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Primary Question

MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kiwanda cha Chumvi katika Kata ya Ilindi, Wilayani Bahi kitakachosaidia kuongeza mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Bahi na kutoa ajira kwa wananchi hasa akina mama?

Supplementary Question 1

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, shughuli ya uchimbaji chumvi kwenye kata ya Ilindi imekuwa ni ya muda mrefu na Halmashauri tumepanga mwaka ujao wa fedha tuweze kutenga fedha kwa ajili ya kujenga jengo ambalo sasa tutahitaji tupate mashine kwa ajili ya kiwanda kianze.

Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari aambatane na mimi baada ya Bunge hili ili kwanza akaone eneo lile na ikiwezekana kama alivyosema sasa SIDO waweze kutusaidia kiwanda kile kianze?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili, Serikali imesema kwamba Kata ya Chali na Kata ya Ilindi ni kata ambazo zina chumvi pale, lakini pamoja na ile kumekuwa na tatizo la upatikanaji wa maji kwa sababu ya chumvi Kata ya Ilindi haina maji kabisa kila sehemu maji yana chumvi na Kata ya Chali nayo haina maji ina sehemu moja ambayo ina chanzo cha maji, lakini Serikali imekuwa inaahidi haijatekeleza mradi ule.

Je, Waziri wa Maji yuko tayari vilevile naye aweze kufanya ziara kwenye Kata ya Ilindi na Kata ya Chali ili aweze kuona shida inayowakabili wananchi wa kata hizi kutokana uwepo wa chumvi ya kutosha?

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA. Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kenneth Nollo, Mbunge wa Bahi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema lengo la Serikali ni kuona tunahamamisha ujenzi wa viwanda vingi nchini ili kutumia malighafi tulizonazo, kwa hiyo, niko tayari kuambatana na Mheshimiwa Nollo ili twende kuangalia kwanza sehemu yenyewe ilivyo, lakini pia tuweze kupata taarifa sahihi na kuweza kuanza michakato ya kuona namna gani ya kuvutia wawekezaji katika kujenga kiwanda au viwanda katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la pili, ni kweli, kwa sababu kama alivyosema eneo lile lina chumvi kwa hiyo maana yake maji mengi yatakuwa ni ya chumvi. Serikali kupitia Wizara ya Maji najua wana mipango mingi, basi tutashirikiana na Wizara ya Maji ili kuhakikisha tunaona namna gani ya kuwasaidia ndugu zetu wa Bahi ili waweze kupata maji safi kwa ajili ya matumizi ya majumbani.

Name

Dr. Pius Stephen Chaya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Mashariki

Primary Question

MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kiwanda cha Chumvi katika Kata ya Ilindi, Wilayani Bahi kitakachosaidia kuongeza mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Bahi na kutoa ajira kwa wananchi hasa akina mama?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Manyoni Mashariki chumvi inapatikana katika Vijiji vya Mpandagani, Majiri na Mahaka.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi wa vijiji hivyo vitatu ili waweze kuwekeza katika viwanda vidogo vidogo? Ahsante sana.

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Chaya, Mbunge wa Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli sisi Tanzania tumebahatika kuwa na madini ya chumvi mengi kwa maana ya maeneo mengi, lakini uzalishaji wetu bado ni mdogo, ni wastani wa takribani tani 330,000 ambazo tunazalisha kwa mwaka. Kwa hiyo, kama nilivyosema, lengo la Serikali ni kuona sasa tunahamasisha viwanda vingi ili tuweze kuzalisha zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, na takwimu zinatuonesha kwamba tunaweza kuzalisha mpaka uwezo wa tani milioni moja kwa mwaka. Kwa hiyo tani 330,000 ambazo zipo ni kidogo. Kwa hiyo, jimbo la Mheshimiwa Dkt. Chaya ambao nao pia wana deposit nyingi za chumvi, basi nako pia tutaona namna gani ya kuona sasa tunahamasisha viwanda vingi ili viweze kujengwa katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Chaya kwa kuwa amekuwa akifuatilia sana suala hili na mimi nimuahidi kwa niaba ya Serikali kwamba tunafanya kila liwezekanalo ili tuweze kuwa na viwanda katika Mkoa huu wa Singida, Jimboni kwa Mheshimiwa Chaya kule Manyoni Mashariki. Ahsante sana.

Name

Shamsia Aziz Mtamba

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Mtwara Vijijini

Primary Question

MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kiwanda cha Chumvi katika Kata ya Ilindi, Wilayani Bahi kitakachosaidia kuongeza mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Bahi na kutoa ajira kwa wananchi hasa akina mama?

Supplementary Question 3

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lililopo Bahi linafanana kabisa na tatizo lililopo Mtwara; viwanda vingi vimekufa kikiwemo Kiwanda cha Kubangulia Korosho cha Olam ambacho kilikuwa kinatoa ajira kwa wnanachi wengi wa Mkoa wa Mtwara.

Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua viwanda hivyo?

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shamsia Mtamba, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mkoa wa Mtwara ndiyo ambao unazalisha korosho nyingi hapa nchini kuliko mikoa mingine na pia kumekuwa na viwanda vingi sana vya kubangua korosho ambavyo kama nilivyosema kabla tulikuwa na viwanda 12 vya Serikali ambavyo baadaye vilibinafsishwa. Lakini kuna vingine ambavyo vimekuwa havifanyi vizuri sana na tumeweza kuvirejesha Serikalini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda hiki cha Olam anachokisema of course kimefungwa kutokana na changamoto mbalimbali, lakini moja ya changamoto kubwa ambazo zilikuwa zinakabili viwanda vyetu ilikuwa ni upatikanaji wa malighafi, kwa maana ya korosho ghafi kwa ajili ya kubanguliwa katika viwanda hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, na moja ya mikakati ambayo Serikali sasa imefanya ni kuona sasa viwanda hivi vinapata malighafi katika mnada wa awali, kwamba viwanda vile vya kubangua korosho vipate malighafi zinazotakiwa, halafu baadaye sasa korosho zinazobakia ziende kwenye mnada wa kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mikakati inayowekwa na Serikali viwanda vingi sasa vitarudi kufanya kazi kwa sababu vitakuwa na uhakika wa malighafi, lakini pia na mazingira wezeshi ambayo Serikali imeanza kuyaweka ili kuvutia wawekezaji zaidi katika viwanda mbalimbali vikiwemo viwanda vya korosho katika Mkoa wa Mtwara.

Name

Leah Jeremiah Komanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Meatu

Primary Question

MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kiwanda cha Chumvi katika Kata ya Ilindi, Wilayani Bahi kitakachosaidia kuongeza mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Bahi na kutoa ajira kwa wananchi hasa akina mama?

Supplementary Question 4

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Serikali iliahidi kujenga kiwanda cha kusindika chumvi Ziwa Eyasi, Nyalanja katika Jimbo la Meatu; je, ni lini Serikali itatekeleza hilo? (Makofi)

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Leah Komanya, Mbunge wa Meatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, kama nilivyosema katika jibu la msingi kwamba tunahamasisha ujenzi wa viwanda mbalimbali hapa nchini ikiwemo viwanda ambavyo vinachakata chumvi. Katika jimbo la Mheshimiwa Komanya katika Halmashauri ya Meatu Serikali iliahidi kujenga kiwanda kwa ajili ya kuchakata chumvi iliyopo katika Mkoa huo wa Simiyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali kama Wizara tulipata andiko kutoka kwenye Halmashauri ya Meatu na andiko hilo tunalifanyia kazi. Lakini pia tunajua kwamba kuna taasisi moja ya Nutrition International ambayo yenyewe tayari imeshaanza kuongeza thamani chumvi inayochimbwa pale ambayo kweli soko lake lipo katika nchi za Rwanda na Burundi na maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba sisi Tanzania ambao ndio tuko kwenye Ukanda huu wa Pwani pamoja na Kenya, ndio wenye deposit kubwa za chumvi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa hiyo, ni vyema sana na sisi kama Serikali tumelitambua hilo kutumia soko hili ili tuweze kuzalisha chumvi nyingi zaidi, tuweze kuuza katika masoko ambayo yanatuzunguka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutakamilisha hilo, na Serikali inaendelea kulitekeleza andiko hilo ili angalau tuweze kukamilisha ujenzi wa kiwanda hicho kwa kuwavutia wawekezaji wengi zaidi, lakini pia na taasisi za Serikali ambazo zinaweza zikafanya uwekezaji katika eneo la Meatu. (Makofi)