Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Abeid Ighondo Ramadhani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Kaskazini

Primary Question

MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:- Je, ni lini Serikali itavipatia huduma ya maji safi na salama Vijiji vya Kinyamwenda, Igauri, Matumbo, Itamka na Msimihi katika Jimbo la Singida Kaskazini?

Supplementary Question 1

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, Serikali baada ya kukamilisha miradi ya maji, hasa vile visima virefu, huanzisha kamati za watumiamaji, lakini kamati hizi zimekuwa zikishindwa kujiendesha na hivyo kufikia mahali kushindwa kabisa kutoa huduma au kufa. Na ningependa kushauri pengine Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wale watumishi wanaotakiwa kuajiriwa na watumiamaji, na hizi kamati, waajiriwe moja kwa moja na Wizara badala ya hizi kamati halafu zile fedha kidogo zinazopatikana zielekezwe kwenye ukarabati na ununuzi wa vifaa?

Mheshimiwa Spika, lakini swali lingine la pili. Serikali ilichimba visima virefu katika Kijiji cha Misinko na Kijiji cha Kitongoji cha Gairo katika Kijiji cha Sagara, lakini baada ya kukamilisha kuchimba visima vile maji yale yalionekana yana chumvi nyingi sana na hivyo hayafai kwa matumizi ya binadamu. Serikali iliahidi kuchukua sample ya yale maji na kuyapima ili yaweze kutumiwa na binadamu, jambo ambalo hadi sasa halijafanyika.

SPIKA: Sasa swali Mheshimiwa.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kuhakikisha kuja na mkakati mbadala wa kuwapatia maji safi na salama wananchi wa vijiji vile? Na hapa ningeomba Mheshimiwa Naibu Waziri angeambatana na mimi twende tukaonje yale maji yalivyo na chumvi na hayafai kabisa kwa matumizi ya binadamu.

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Abeid Ramadhan, Mbunge wa Singida Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la Kamati za Watumiamaji, hili Mheshimiwa Waziri ameshakuwa akiongea mara nyingi na ameshawaagiza mameneja wote wa maeneo yote ya Mamlaka za Maji pamoja na RUWASA kuona kwamba, wanaajiri vijana wetu wanaotokana na chuo chetu cha maji pale Dar-Es-Salaam, hasa kwenye eneo la uhasibu. Hii ni kwa sababu, kumekuwa na ubadhirifu mkubwa sana katika hizi jumuiya.

Mheshimiwa Spika, na mfano mzuri uko pale kwenye Jimbo lake Pangani. Palikuwa hakuna mhasibu, waliweza kukusanya labda laki saba tu kwa mwezi, lakini baada ya kumuajiri binti ambaye ni mhasibu, msomi, mwenye profession hiyo sasa hivi wanaweza kukusanya takribani milioni nne na nusu. Hivyo, tunaendelea kutoa wito katika majimbo yote tuweze kushirikiana kuona kwamba, kamati zile tunaruhusu hawa vijana wanaajiriwa.

Mheshimiwa Spika, na kuhusiana na mishahara yao itoke Serikalini; kwa sasa hivi inakuwa ni ngumu, lakini kwa sababu wao wenyewe wanakusanya fedha za kutosha wana uwezo wa kujisimamia na kuweza kulipana hiyo mishahara. Pamoja na hilo, tayari Mheshimiwa Waziri ametupia jicho la ziada kuona nyakati zile za kiangazi namna gani ya kuweza kuzisaidia jumuiya hizi.

Mheshimiwa Spika, lakini katika suala la maji chumvi kuweza kupatikana baada ya kisima kuchimbwa:-

Mheshimiwa Spika, tayari pia wataalamu wetu wameelekezwa kwenda kusimamia na kuona namna bora ya kuona chumvi hii inaweza ikatibika. Na endapo itashindikana basi, chanzo mbadala cha maji kitaweza kufikiriwa na kutumika katika utoaji maji kwenye jamii.

Name

Dr. John Danielson Pallangyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arumeru-Mashariki

Primary Question

MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:- Je, ni lini Serikali itavipatia huduma ya maji safi na salama Vijiji vya Kinyamwenda, Igauri, Matumbo, Itamka na Msimihi katika Jimbo la Singida Kaskazini?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali langu, je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Naibu Waziri ya kuvipatia huduma ya maji Vijiji vya Nkonekoli, Nkure, Njani, ambayo aliitoa wakati alipozuru jimboni kwetu mwezi Disemba kuelekea sikukuu za Christimas? (Makofi)

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ahadi ni deni, kwa sababu tumeahidi lazima tuje tutekeleze. Mara baada ya utaratibu mzima wa upatikanaji wa fedha kwenye eneo lako, lazima wataalamu waje na ni lazima maji yapatikane kwenye Jimbo lako la Arumeru, ahsante.