Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Primary Question

MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:- Je, ni lini serikali itakuwa tayari kuanza mradi wa TACTIC ili kufikia Malengo Makuu ya Serikali ya mwaka 2020 – 2025 katika kuboresha miundombinu ya barabara?

Supplementary Question 1

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kifupi sana uniruhusu. Ninafahamu kwamba mradi wa TACTIC ni mradi mbadala baada ya mradi wa TSP. Mradi wa TSP umekuwa mkombozi mkubwa sana kwenye nchi yetu kwenye miji, majiji na Serikali kwa pamoja. Utakumbuka hata ukiitazama Mbeya leo ukaitazama Mwanza, Tanga, na Manispaa nyingine za Kigoma, Ujiji na maeneo mengine, zaidi ya kilometa 457 zilijengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu toka Juni, 2019 barabara nyingi sana zilitangazwa na wakandarasi wakahitajika, wakajaza fomu ili wapate kazi. Sioni jitihada za Serikali ambazo zitatusaidia kuhakikisha barabara hizi zinatengenezwa kwa wakati. Barabara ziko nyingi, mfano ukienda hata Mbeya leo barabara ya kutoka machinjio ya Ilemi kwenda Mapelele inategemea fedha hizi ili ijengwe kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda barabara ya Buswelu ambayo itakwenda kuunganisha soko la mbogamboga mpaka stendi mpya inategemea barabara hii. Barabara ya Mkuyuni kwenda Nyakato inategemea fedha hizi. Soko jipya la Kirumba linategemea fedha hizi. Hata ukienda kule kwa Mheshimiwa Ummy, barabara ambayo inakwenda Masiwani kwenda Hospitali ya Wilaya inategema fedha hizi. (Makofi)

Sasa jitihada za Serikali za Serikali kuhakikisha fedha hizi zinapatikana: ni lini Serikali itahakikisha mradi huu unaanza mara moja ili fedha hizi zipatikane tuone matokeo?

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali inafahamu kwamba TARURA haina uwezo wa kujenga barabara hizi bila fedha hizi tunazozitegemea leo zipatikane. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Swali lake la kwanza la msingi Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula Mbunge alijaribu kuainisha umuhimu wa mradi huu wa uendelezaji wa miundombinu katika miji kwa maana ya TACTIC kwa kutaja maeneo mbalimbali ikiwemo katika Jimbo ambalo anatokea Naibu Spika wetu Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson. Ametaja Jimbo ambalo anatokea Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mheshimiwa Ummy Mwalimu pamoja na Jimbo lake Mheshimiwa Mbunge, Jimbo la Nyamagana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunatambua umuhimu wa barabara hizi na tunatambua umuhimu wa mradi huu. Ndiyo maana tumesema Serikali ipo katika hatua za mwisho za majadiliano na hata katika ile miji yote ambayo imeainishwa kwenye huu mradi mtaona tumetuma wataalam katika kila Halmashauri, wameshafika huko kujadiliana mambo gani ya msingi yaingizwe katika huo mradi. Hiyo yote ni nia njema ya kuhakikisha kwamba huu mradi unakamilika kwa wakati. Ninaamini chini ya uongozi wa Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia Hassan Suluhu; chini ya uongozi wa Waziri wa Nchi, Mheshimiwa Ummy Mwalimu jambo hili litakamilika kwa wakati na huu mradi utatekelezeka kwa vitendo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili amesema kwamba TARURA haina uwezo wa kuzijenga barabara hizo. Ni kweli, ndiyo maana tumekuja na huu mradi wa TACTIC kuhakikisha zile changamoto za barabara katika hayo maeneo yote yaliyotajwa tunazitatua. Kwa hiyo, lengo letu ni kuhakikisha tukidhi vigezo, tumalize majadiliano na mwisho wa siku barabara zianze kujengwa kwa sababu hilo ndiyo lengo la Serikali. Ahsante.

Name

Mussa Ramadhani Sima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Primary Question

MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:- Je, ni lini serikali itakuwa tayari kuanza mradi wa TACTIC ili kufikia Malengo Makuu ya Serikali ya mwaka 2020 – 2025 katika kuboresha miundombinu ya barabara?

Supplementary Question 2

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mradi huu wa TACTIC, Singida mjini pale unatarajiwa kujenga soko la kisasa la vitunguu, soko la Kimataifa. Pia, wananchi wa Singida Mjini wanataka kujua ni lini mradi huu utakamilika? Kwa sababu feasibility study imekwishafanyika. Sasa ni lini, ili waweze kuendelea na soko lao la Kimataifa?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kama nilivyojibu katika maswali madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Stanslaus Mabula, Mbunge wa Nyamagana na ndivyo ambavyo nitamjibu Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Mussa Sima, kwamba nafahamu kwamba kulikuwa na awamu ya kwanza ya majadiliano, sasa hivi tuko katika majadiliano awamu ya mwisho. Ndiyo maana katika sehemu ya huo mradi tumewatuma wataalam kuhakikisha wanaainisha maeneo yale muhimu yanayojengwa na mradi huu ni component ya mambo mengi ndiyo maana kuna masoko, barabara, kuna madampo ndani ya huu mradi wa TACTIC. Huu mradi utakapokamilika maana yake utasaidia mambo mengi ikiwemo mpaka kujenga stendi za kisasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba awe na subira kwa sababu tuko hatua za mwisho na hii kazi itafanyika. Ondoa wasiwasi. Chini ya Awamu ya Sita, barabara hizi zitajengwa, mradi huu utafika na wananchi wa Singida Mjini na maeneo yote ambayo yameainishwa katika huu mradi watafaidika na mradi huu. Ahsante.

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Primary Question

MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:- Je, ni lini serikali itakuwa tayari kuanza mradi wa TACTIC ili kufikia Malengo Makuu ya Serikali ya mwaka 2020 – 2025 katika kuboresha miundombinu ya barabara?

Supplementary Question 3

MHE. ANTHONY P. MAVUNDE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kwa kuwa mradi huu unaligusa pia na Jiji la Dodoma na kwa kuwa wataalam walishakaa na kuibua miradi hii kuanzia ngazi ya mtaa, kata mpaka Ofisi ya Rais, TAMISEMI: -

Je, ni lini sasa Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na Wizara ya Fedha mtakaa pamoja mkwamue vikwazo vilivyopo ili wananchi waweze kunufaika na huu mradi? (Makofi)

Name

Ummy Ally Mwalimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana Naibu Waziri, Mheshimiwa Silinde kwa majibu mazuri, pia namshukuru Mheshimiwa Anthony Mavunde na mleta swali, mtani wangu Mheshimiwa Mabula kwa swali zuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, tunatambua kwamba mradi wa TACTIC ni mradi wa kimkakati katika Halmashauri za Majiji na Miji 45. Serikali ya Awamu ya Sita kama alivyosema Naibu Waziri, tumeweka mradi huu kuwa ndiyo mradi wetu wa kielelezo katika kujenga miundombinu ya barabara, masoko pamoja na madampo ya taka katika miji 45.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu swali la Mheshimiwa Anthony Mavunde ni lini TAMISEMI tutakaa na Wizara ya Fedha? Ndiyo maana nilitaka kusimama. Jumatatu ya tarehe 10 Mei, 2021 nilikaa mimi pamoja na Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Mwigulu kwenye Ofisi ya Wizara ya Fedha pamoja na wataalam wetu na tukakubaliana kwamba majadiliano yamekamilika, sasa tunapeleka World Bank kwa ajili ya taratibu za kusaini mkataba wa kuanza ujenzi wa mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu mradi huu ni muhimu sana kwa Jiji la Mbeya, nafahamu mradi huu ni muhimu sana kwa Jiji la Arusha, nafahamu mradi hii ni muhimu sana kwa Jiji la Dodoma, pia ni muhimu sana kwa Jiji la Mwanza. Na mimi Tanga Jiji mradi huu kwangu ndiyo utanipa kura za kurudi Bungeni mwaka 2025.

Kwa hiyo, kutopatikana kwa TACTIC maana yake sitarudi Bungeni 2025. Kwa hiyo, naubeba kama mradi wangu, lakini na kwa Majiji mengine yote 45 tutahakikisha tunaanza utekelezaji mara moja. Ahsante sana. (Makofi)