Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Primary Question

MHE. AIDA J. KHENANI atauliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza changamoto ya maji katika Wilaya ya Nkasi?

Supplementary Question 1

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, nimeyasikia majibu ya wizara. Kwa kuwa mpango wa Serikali ulijiwekea malengo kufikia mwaka 2025 upatikanaji wa maji vijijini itakuwa ni asilimia 85. Na leo ni mwaka 2021 na umekiri hapa kupitia majibu yako takwimu ambazo umezisoma kwamba upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Nkansi ni asilimia 48 tu. Kwanza takwimu hizi si halisia. Lakini napenda kuwaambia Serikali kwa kuwa mpaka sasa tuna asilimia 48 hamuoni sasa kuna jitihada za ziada za kutumia chanzo cha Ziwa Tanganyika ili kuweza kufikia asilimia 85 kama malengo tuliyojiwekea? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Swali la Pili, huu mradi wa maji Namanyere wananchi wameanza kuangalia mabomba toka mwaka jana hawapati maji mpaka leo. Ningependa kujua kuna mkakati upi wa ziada wa Serikali wa kuweza kupelekea wananchi wa Namanyere na Kata zote za Jimbo la Nkasi Kaskazini maji ili waendane na kauli mbiu ya Mama Samia ya kumtua mama ndoo kichwani? (Makofi)

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mpango wa Serikali kufika mwaka 2025 kadri ya ilani ya Chama Tawala inavyotaka vijijini maji yatapatikana kwa asilimia 85 na zaidi ikiwezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo nipende kukutoa hofu Mheshimiwa Mbunge na nikupongeze unafuatilia kwa makini sana masuala haya ya wananchi wako na wewe ni mwanamke ndio maana unaongea kwa uchungu kwasababu unafahamu fika kubeba maji kichwani kwa umbali mrefu namna ambavyo ilivyotabu.

Kwa hiyo tutahakikisha tunawatua kina mama ndoo kichwani. Wewe ni Mbunge mahiri mwanamke na mimi ni Naibu Waziri Mwanamke wote tunafahamu adha ya kubeba maji kichwani tutashughulikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, huko nyuma tunafahamu fika RUWASA haikuwepo na kwa mwaka mmoja tu tumeona namna ambavyo RUWASA imefanya kazi kwa bidii. Na kufufua miradi ambayo ikisuasua na sasa hivi maji yanapatikana mabombani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutumia Ziwa Tanganyika Mheshimiwa Aida, kama ambavyo tumetoka kuongea kwa kirefu hapa majuzi wakati tunapitisha bajeti yetu. Huu ni mpango mkakati wa kutumia vyanzo hivi vya uhakika, kwa hiyo Ziwa Tanganyika nalo lipo kwenye mikakati ya wizara tutahakikisha tunalitumia ili kuona kwamba mabomba yapate kutoa maji na sio kushika kutu. Kwa hiyo, haya yote uliyoyaongea yapo kwenye utekelezaji wa wizara na ifikapo mwaka 2021/2022 mwaka mpya wa fedha Ziwa Tanganyika nalo tayari lipo kwene mpango mkakati wa utekelezaji. (Makofi)