Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Primary Question

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza:- Je, ni lini barabara za kutoka Rubanga – Isulwabutundwe – Mkoba -Kukuruma – Kamhanga - Kishinda na Mkolani zitatengewa fedha na TARURA kwa ajili ya ujenzi?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, wananchi wa Isulwabutundwe, Dubanga, Isamilo, Mkolani, Busekeseke ni wananchi wavumilivu sana. Barabara hizi hazijalimwa kwa miaka 10 sasa; na tunaishukuru Serikali tumepata kiasi cha shilingi milioni 580 kwa ajili ya kulima kama alivyoeleza Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika barabara hizi, barabara ya Isamilo - Mkolani – Busekeseke ina urefu wa kilometa 18, tumepata morum kilometa 7; hii nyingine ya Mkoba Bridge – Isulwabutundwe – Mkolani – Dubanga tumepata kilometa tano. Sasa Mheshimiwa Waziri nilikuwa naomba kuuliza: Serikali haioni umuhimu wa kuweza kuongeza fedha kwa dharura ili kipande kilichobaki kuwekewa moorum kilimwe kwa pamoja, maana kukilima nusu kitaondoka, halafu tena mwakani tutaanza upya.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Wananchi wa Nyamikoma kupitia daraja la Kimilawinga, daraja hili inaponyesha mvua halipitiki kabisa na wananchi hawa ni lazima wapite Kimilawinga waende Lwenge, waende Kamwanga kwa ajili ya kupata mahitaji na mpaka Nzela:

Je, Serikali haioni umuhimu wa kutenga pesa sasa kwa ajili ya kwenda kujenga daraja hili kwa dharura? (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Swali la kwanza dogo ambalo aliuliza Mheshimiwa Kasheku Musukuma ni kutaka Serikali iongeze fedha katika zile barabara tulizozitoa ili kuhakikisha yale maeneo ambayo Moorum haijawekwa, basi yawekwe na yalimwe kwa pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimjibu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mwaka wa fedha huu unaokuja, kuna fedha vile vile imetengwa kwa maana ya mwaka 2021/ 2022 kwa ajili ya barabara hizo. Kwa hiyo, ninaamini kabisa kwamba zimepelekewa fedha na itafanya kazi kwa mwaka wa fedha unaokuja kwa sababu huu mwaka sasa tunaumalizia na ndiyo kazi ambazo zinazoendelea kwa wakati uliopo.

Mheshimwa Naibu Spika, jambo la pili, amezungumzia daraja linalopita Kinilawinga na amehitaji kwamba Serikali ilijenge kwa dharura. Nafikiri suala la madaraja siku zote, ninyi wote hapa mnatambua kabisa kwamba daraja linahitaji tathmini kwanza, baada ya tathmini ndiyo ujue gharama yake ni kiasi gani? Kwa hiyo, niagize tu TARURA wakafanye tathmini katika eneo hilo halafu walete Ofisi ya Rais, TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)

Name

Jeremiah Mrimi Amsabi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Serengeti

Primary Question

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza:- Je, ni lini barabara za kutoka Rubanga – Isulwabutundwe – Mkoba -Kukuruma – Kamhanga - Kishinda na Mkolani zitatengewa fedha na TARURA kwa ajili ya ujenzi?

Supplementary Question 2

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Kufuatia mvua nyingi ambazo zimenyesha katika Jimbo la Serengeti, barabara nyingi zilizo chini ya TARURA sasa zimeharibika sana ikiwemo barabara ya kwenda Iselesele, barabara ya kwenda Mosongo lakini pia barabara ya kuzunguka stendi ile. Pia barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami kuzunguka soko la Mji wa Mugumu nayo haijajengwa muda mrefu:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara hizi na zile za kufanyiwa marekebisho? Ahsante.

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Jeremiah Amsabi Mrimi, ameainisha barabara kadhaa ambazo zinahitajika zitengenezwe; na kwa kuwa nafahamu changamoto za barabara kama ambavyo Wabunge wamekuwa waki- debate humu ndani ya Bunge; niseme tu, jambo hilo tumelipokea na sisi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI katika ule mchakato wetu wa pamoja, tunaandaa plan ambayo itahakikisha barabara zote nchini tunazipitia, tunafanya tathmini ya kutosha na kutafuta fedha kwa ajili ya kuhakikisha hizo barabara zinatengenezwa.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, awaambie tu wananchi wa Serengeti wakae mkao wa kula, hizi barabara tutazifanyia kazi na kazi yake mtaiona kabla ya miaka hii mitano kwisha.Ahsante. (Makofi)

Name

Nusrat Shaaban Hanje

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza:- Je, ni lini barabara za kutoka Rubanga – Isulwabutundwe – Mkoba -Kukuruma – Kamhanga - Kishinda na Mkolani zitatengewa fedha na TARURA kwa ajili ya ujenzi?

Supplementary Question 3

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa kuna umuhimu sana katika barabara ya Singida – Supuka – Ndago ambayo kimsingi inapita katika Jimbo la Waziri wa Fedha pia.

Je, ni lini sasa Serikali itaichimba angalau kwa kiwango cha changarawe barabara hii ambayo zaidi ya miaka kumi haijafanyiwa marekebisho yoyote?

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Mbunge ameuliza barabara ya Supuka – Ndago ambako ni Jimbo la Iramba Magharibi ambapo anatokea Waziri wa Fedha wa sasa Mheshimiwa Mwigulu Nchemba. Niseme tu kabisa kwamba barabara hiyo itajengwa kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Name

Masache Njelu Kasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Primary Question

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza:- Je, ni lini barabara za kutoka Rubanga – Isulwabutundwe – Mkoba -Kukuruma – Kamhanga - Kishinda na Mkolani zitatengewa fedha na TARURA kwa ajili ya ujenzi?

Supplementary Question 4

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kuniona. Nami pia niungane na swali la msingi kama ilivyo Wilaya ya Geita Mjini, kulikuwa na matatizo ya barabara zilizo chini ya TARURA. Wilaya yetu ya Chunya pia ina matatizo mengi ya barabara zilizo chini ya TARURA zilizoharibika vibaya kutokana na mvua zilizonyesha mwaka huu.

Mheshimwa Naibu Spika, barabara ya kuanzia Lupa kwenda Nkunungu – Lupa - Lwalaje zimeharibika vibaya na kwenye fedha zilizokuwa zimetengwa, zilitengwa maeneo korofi:-

Je, ni lini Serikali itatoa fedha za dharura ili barabara hizo ziwewe kutengenezwa ikizingatiwa kuwa maeneo haya zinalimwa Tumbaku na msimu wa soko la Tumbaku unaanza wiki ijayo kwa hiyo, itashindwa kutoka kule? Nashukuru.

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Masache ameainisha baadhi ya barabara ambazo zimeharibika sana wakati wa mvua yakiwemo madaraja; na sehemu ya hizo barabara TARURA walipeleka fedha kwa ajili ya kutatua hizo changamoto za udharura kwa maana ya uharibifu wa hizo barabara. Sasa hivi ameomba tu kwamba Serikali ni lini tutatenga fedha kuhakikisha hizo barabara zinapitika?

Mheshimiwa Naibu Spika, jibu la msingi ni kwamba kadri ya upatikanaji wa fedha utakavyokuwa tutazitengeneza na bahati nzuri maeneo hayo mimi nayafahamu na nimeahidi kufika kujionea mwenyewe hali halisi. Nitakwenda na Mheshimiwa Mbunge na tutazungumza na wananchi. Ninaamini kabisa kwamba kutokana na bajeti ambayo Bunge lilipiga kelele na Serikali ikaongeza, tutafikia maeneo mengi sana mwaka huu wa fedha kuhakikisha tunapunguza hizo changamoto ambazo zinawakabili wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.