Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Deodatus Philip Mwanyika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Primary Question

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: - Je, ni lini Vijiji na Vitongoji nchini ambavyo havijapatiwa umeme vitapatiwa huduma hiyo?

Supplementary Question 1

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Moja, baada ya ufuatiliaji wa karibu sana kwenye suala hili imedhihirika wazi kwamba kwa Jimbo la Njombe ni vijiji vinne tu, Mgala, Ngalanga, Mtila na Mbega ndivyo vilivyoingizwa kwenye Mpango ambao Mheshimiwa Naibu Waziri anauongelea. Kuna vijiji takriban 20 ambavyo vimesahaulika, vijiji hivyo ni Hungilo, Uliwa, Utengule, Diani, Makolo, Lugenge, Mpeto n.k. Naomba Serikali itoe kauli kuhusiana na suala hili na iwadhihirishie wananchi wa Njombe kama sasa baada ya maongezi kati yangu, Waziri na REA vijiji vilivyobaki vyote vimeingizwa katika Mpango huo.

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Pamoja na vijiji vingi kuunganishwa na hasa kwenye Jimbo letu la Njombe Mjini bado tuna ukatikaji wa umeme mkubwa sana ambao unaashiria kwamba pamoja na kuunganishwa, tatizo hili litaendelea kuwa kubwa. Tunaomba maelezo ya Wizara kuhusiana na ukatikaji wa umeme katika Mji wa Njombe ambao ni endelevu na hauishi. (Makofi)

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ni kweli mara ya kwanza vilichukuliwa vijiji vinne lakini baada ya Mheshimiwa Mwanyika kuwasiliana na ofisi na tunamshukuru na kumpongeza kwa ufuatiliaji wake mkubwa, Wizara imeamua iongeze scope ya kazi ya awali na kuongeza vijiji hivyo.

Mheshimiwa Spika, kimsingi vilikuwa havikuachwa lakini vilikuwa vimebaki kwasababu viko katika eneo linalokaribiana na mji. Kwa hiyo, vilikuwa havikuingia kwenye mradi wa REA lakini tumevichukua tukivi-treat kama peri- urban area. Kwa hiyo, vijiji hivyo 20, nimhakikishie Mheshimiwa Deo Mwanyika kwamba vimeingia na vitafanyiwa kazi katika awamu hii ya kupeleka umeme vijijini.

Mheshimiwa Spika, katika swali la pili, ni kweli. Maeneo ya Njombe yana tatizo kubwa sana la ukatikaji wa umeme. Naomba nitumie muda kidogo tu kukueleza tatizo kubwa tulilokuwa nalo Njombe na hatua taunazozichukua. Njombe inapata umeme kutoka katika kituo chetu cha kupooza umeme cha Makambako na kuna kilometa 60 kutoka pale Makambako mpaka Njombe, Njombe Mji na eneo kubwa la Mkoa. Sasa Njombe tunayo matatizo makubwa matatu.

Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa la kwanza ni baraka ambazo Njombe imezipata ya kuwa na miti mingi sana. Ile miti, pamoja na sisi kufyeka ile line ya kupitisha umeme, lakini miti inayokuwa nje ya line yetu ya umeme baadaye inaangukia ndani ya line yetu kwa sababu inakuwa ni mirefu sana. Kwa hiyo, tumeendelea kufyeka na kuhamasisha wananchi basi hata watuongezee line ambayo iko nje zaidi ya line yetu sisi ili tunapofyeka basi miti inayotokea nje ya line
yao isije ikaleta shida kwenye eneo letu.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo linatupa shida sana kwa Mkoa wa Njombe ni radi. Maeneo ya Njombe, kama nilivyowahi kusema hapa, Mkoa wa Kagera lakini pia Mbeya, tunayo matatizo makubwa sana ya radi ambazo zimekuwa zikileta shida kwenye miundombinu yetu ya umeme.

Mheshimiwa Spika, tunachokifanya kwa Mkoa wa Njombe kwa mfano kila tunapofunga transformer tunaifanyia earthing system. Ile earthing system inatakiwa uzamishe chini, lakini unapima udongo kuona resistance value ya udongo ni kiasi gani. Kama iko 0 - 60 inakuwa haina shida, kama iko zaidi ya 60 inabidi kutumia zile njia za kienyeji na za kitaalam za ku--treat udongo ili radi ikienda iweze kumezwa kule, tunatumia mbolea na vitu vingine kama hivyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, pengine tukifunga transformer tunachelewa kuiwasha kwa sababu tukipima resistance value ya udongo tunaona bado ina-resist sana radi, kwa hiyo, tunaamua kuiacha kwanza ili ipoe kidogo.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri.

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie. Naomba niruhusiwe kutoa nondo kama alizozitoa mwenzangu Ndaisaba jana kwa ajili ya uelewa mzuri.

Mheshimiwa Spika, lakini eneo la pili tunafunga vifaa vya muhimu sana vinavyoitwa surge arrester and combi unit kuhakikisha kwamba transformer haiharibiki mara kwa mara. Kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa Deo kwamba tutaendelea kuhakikisha kwamba…

SPIKA: Nakushukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri.