Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Thea Medard Ntara

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo Kikuu cha Taifa Kusini mwa Tanzania na Kanda nyingine ambazo hazina Vyuo Vikuu?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ambayo yamenikatisha tamaa, nimechanganyikiwa, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Serikali ilianzisha Kitengo cha SUA huko Tunduru, Waziri anijibu, je, ni lini tawi hilo litaanza kufanya kazi kama Chuo Kikuu Kishiriki au Centre na twende wote huko tukaone?

Swali la pili, Vyuo Vikuu Vishiriki vya Taasisi ya Dini vilivyopo Kusini kama hicho alichokitaja, Stella Maris na kile kingine kipo pale Songea kinaitwa AJUCO, vimeendelea kuzorota na vingine vimefungwa. Serikali ndio inatakiwa kusimamia hivyo vyuo ili viweze kusimama kwenye sehemu yake. Mheshimiwa Waziri ataniambia wanasaidiaje hivi vyuo ambavyo watoto wanaosoma ni Serikali hii hii ili viweze kusimama na kufanya kazi yake kikamilifu? Ahsante.

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Thea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Chuo chetu cha SUA kilikabidhiwa eneo katika majengo ambayo yalikuwa ya camp ya waliokuwa wanajenga barabara. Serikali imefanya yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli udahili katika chuo hiki cha Tunduru bado haujaanza na kinachokwamisha kuanza udahili pale ilikuwa bado kuna miundombinu ambayo siyo toshelezi. Bado hakuna mabweni pamoja na maabara katika eneo hili. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, katika mwaka wa fedha 2020/2021, Chuo chetu cha SUA kimepanga kuanza kutoa kozi fupi fupi pale katika eneo letu la Tunduru kwa wakulima wetu kwa lengo la kuongeza mnyororo wa thamani kwenye mazao ya korosho, mihogo pamoja na ufuta.

Mheshimiwa Spika, halikadhalika majengo yale yaliyopo kwa hivi sasa yanatumika kwa ajili ya kufanya mafunzo kwa wanafunzi wetu wanaosoma Shahada ya Wanyamapori na Utalii. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Chuo chetu cha SUA kinaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kutosheleza au kujenga miundombinu ili tuweze kuanza kutoa huduma pale mara tu majengo hayo yatakapokuwa yamekamilika.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, amezungumzia juu ya vyuo binafsi ambavyo vipo katika Kanda hiyo ya Kusini, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali imekuwa inafanya juhudi tofauti tofauti kuhakikisha vyuo hivi vinaendelea kutoa huduma. Serikali imekuwa ikifanya yafuatayo kupitia Tume ya Vyuo Vikuu:-

Mheshimiwa Spika, tumeendelea kufanya ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha kama vyuo hivi vinatoa huduma sawasawa na elimu Bora; Tume yetu imeendelea kutoa ushauri wa kitaalam; na Tumeendelea kutoa mafunzo kwa viongozi pamoja na Wahadhiri wa vyuo hivi. Katika mwaka huu fedha, TCU imeendesha mafunzo ya Wahadhiri pamoja na wamiliki zaidi ya 218 kuhakikisha kwamba vyuo hivi vinasimama sawasawa. Ahsante.