Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Rehema Juma Migilla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ulyankulu

Primary Question

MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:- (a) Je, kwa nini barabara ya Mpanda – Ulyanhulu – Kahama haikujengwa katika kipindi cha 2015 – 2020 kama ilivyoelekezwa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2015 - 2025? (b) Je, ni lini sasa ujenzi wa barabara hiyo utaanza kama ilivyoelekezwa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2020 – 2025?

Supplementary Question 1

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Majibu ya Serikali kupitia Waziri hayaoneshi matumaini kwa wananchi wetu wa Ulyankulu kwamba wanaenda kupata lami. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, barabara hii ilikuwemo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2015/2020 lakini pia kwenye Ilani ya Uchaguzi ya 2020/2025 barabara hii imo. Majibu ya Serikali yanaonesha barabara hii kwa kipindi chote hicho itakuwa tu kwenye upembuzi yakinifu.

Je, kwa miaka hii mitano mingine barabara hii ina uhakika wa kutengenezwa ili wananchi wangu waweze kupata barabara ya lami? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili ni kwamba Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alipotembea Jimboni kwetu Ulyankulu alitoa ahadi ya kututengenezea kilometa tatu kwenye Jimbo letu la Ulyankulu. Lakini tangu kipindi hicho mpaka leo hakuna hata kilometa moja iliyotengenezwa kwa kiwango cha lami.

Swali langu ni je, kupuuzwa kwa kutekeleza kwa kujengwa kwa hii barabara kwa hizo kilometa tatu ni kupuuza ahadi ya Mheshimiwa Rais au na kuwadharau wananchi wake waliompigia kura? Naomba majibu. (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG.
GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Migilla, Mbunge wa Ulyankulu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Migilla kama amenisikiliza kwenye jibu langu la msingi ni kwamba tayari usanifu wa kina unaendelea na utakamilika Septemba mwaka huu. Barabara haiwezi ikaanza kujengwa kabla ya kukamilika kwa usanifu. Atakuwa ni shahidi kwamba wakandarasi wanaofanya usanifu wako field na Wizara inatambua kwamba barabara anayoitaja ni barabara muhimu sana kwani katika Jimbo lake tunatambua lina uzalishaji mkubwa sana wa mazao kama mahindi, mpunga na hata tumbaku.

Mheshimiwa Spika, hii barabara sasa ndiyo inayokwenda kwenye mbuga ambazo zimetambuliwa kama National Park ya Ugalla na nimhakikishie kwmaba katika bajeti ya mwaka ujao pia tumetenga fedha kwa ajili ya kufungua na kuanza ujenzi wa Daraja la Ugalla ili kuunganisha Jimbo lake na Mkoa wa Mpanda. Ni barabara ambayo tayari wakandarasi wapo wakiwa wanaifungua.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimalizie kwa kumhakikishia Mheshimiwa Migilla haitatokea na haiwezekani Serikali hii ikapuuza ahadi za viongozi wetu wa Kitaifa. Ahadi imeahidiwa mwaka uliopita isingekuwa rahisi tuwe tayari tumeshajenga hizo barabara na ndiyo maana tunasema tayari wakandarasi wako site wakifanya usanifu wa kina.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge barabara hiyo itajengwa na wananchi waiamini Serikali yao kwamba yaliyoahidiwa na yaliyoko kwenye Ilani yatatekelezwa. Ahsante sana.