Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Esther Lukago Midimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha ununuzi wa Vifaa Tiba ikiwemo vya upasuaji katika Kituo cha Afya cha Mwabayanda Wilayani Maswa?

Supplementary Question 1

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniruhusu niulize swali la nyongeza pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwanza, naomba niipongeze Serikali kwa kuongeza bajeti ya madawa na vifaa tiba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Kituo cha Afya cha Mwabayanda jengo la kuhifadhi maiti liko tayari lakini halina friji, je, ni lini Serikali itapeleka friji ya kuhifadhia maiti? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa hospitali na vituo vya afya vya Mkoa wa Simiyu tuna upungufu wa madawa; je, Serikali imejipangaje kutupelekea madawa za kutosha kwenye hospitali na vituo vyetu vya afya? Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napokea pongezi zake kwa Serikali kwamba imetenga fedha kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na shilingi bilioni 30 mwaka 2015 mpaka takribani shilingi bilioni 270, karibu mara tisa ndani ya miaka hii mitano. Hiyo ni dalili kwamba Serikali inathamini na imedhamiria kuhakikisha inaboresha upatikanaji wa dawa, vitendanishi na vifaa tiba katika vituo vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu jengo la mortuary kukamilika na kuhitaji jokofu, naomba nimueleze Mheshimiwa Mbunge Esther Lukago Midimu kwamba Serikali inapeleka fedha kwa ajili ya kukamilisha miundombinu ya huduma kama ambavyo tulifanya katika Kituo hiki cha Mwabayanda. Pia tumeelekeza watendaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa baada ya Serikali kupeleka fedha katika vituo hivyo na kukamilisha miundombinu, ni wajibu wao pia kupeleka sehemu ya fedha za maendeleo, ile asilimia 40 au 60 kwa ajili ya kununua baadhi ya vifaa tiba ili kuboresha huduma katika jamii zao. Kwa hiyo, ni muhimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Maswa aone namna bora pia ya kutenga fedha za kununua jokofu kwa ajili ya chumba cha kuhifadhia maiti katika jengo lile la Kituo cha Afya cha Mwabayanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na upungufu wa dawa; Serikali imeendelea kuboresha sana upatikanaji wa dawa katika vituo vyetu kutoka asilimia 65 mwaka 2015 mpaka takribani asilimia 90-94 katika mwaka huu wa fedha. Lengo la Serikali, kwanza ni kuendelea kuboresha upatikanaji wa dawa kwa kuboresha makusanyo ya fedha za uchangiaji wa huduma za afya katika vituo vyetu. Pili ni kuendelea kupeleka fedha Bohari Kuu ya Dawa ili kuendelea kupata dawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kuboresha upatikanaji wa dawa kwenye vituo vya afya katika Mkoa wa Simiyu na nchini kote.

Name

Ally Anyigulile Jumbe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Primary Question

MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha ununuzi wa Vifaa Tiba ikiwemo vya upasuaji katika Kituo cha Afya cha Mwabayanda Wilayani Maswa?

Supplementary Question 2

MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo ya dawa yanayojitokeza katika zahanati zetu ni sawa na yanayojitokeza katika Zahanati za Ipinda, Kyela na hata pale mijini. Ni mpaka lini tutasubiri tatizo hili liishe?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Mlaghila Jumbe, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuboresha; kwanza bajeti ya dawa, vitendanishi na vifaa tiba lakini pili, imeendelea kuboresha sana upatikanaji wa dawa muhimu katika vituo vyetu. Ni kweli pamoja na maboresho haya bado kuna changamoto ya upatikanaji wa dawa katika baadhi ya vituo na halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, maelekezo ambayo Serikali tumeyatoa, kwanza ni kuhakikisha watendaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wanatumia vizuri fedha zitokanazo na uchangiaji wa huduma za afya kwa maana ya cost sharing. Tumejifunza kwamba baadhi ya halmashauri hazitumii vizuri fedha za cost sharing na tumewapa maelekezo kuhakikisha angalau asilimia 50 hadi 60 ya fedha za uchangiaji zinakwenda kununua dawa, vitendanishi na vifaa tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika swali la msingi, Serikali imeendelea kuongeza bajeti na itaendelea kuboresha upatikanaji wa dawa kwa kuongeza bajeti na kusimamia matumizi bora ya dawa katika vituo vyetu. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kulifanyia kazi suala hilo. Pia niwaombe Waheshimiwa Wabunge, kwa sababu sisi ni Madiwani katika mabaraza yetu kufuatilia kwa karibu matumizi ya dawa katika vituo vyetu na kuendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha makusanyo yanakuwa bora zaidi.

Name

Boniphace Nyangindu Butondo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kishapu

Primary Question

MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha ununuzi wa Vifaa Tiba ikiwemo vya upasuaji katika Kituo cha Afya cha Mwabayanda Wilayani Maswa?

Supplementary Question 3

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Kishapu na wananchi wa Kishapu kwa ujumla wameweza kujenga health centers tatu; Health Center za Dulisi, Mwigumbi na Mwang’halanga. Hata hivyo, health centers hizi zina upungufu mkubwa wa dawa na vifaa tiba lakini pia lipo tatizo la upungufu mkubwa wa wafanyakazi (watumishi). Je, Serikali inasema nini kuhusiana na suala zima la kutatua tatizo hili katika Wilaya ya Kishapu?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nawapongeza wananchi wa Jimbo la Kishapu kwa kuchangia nguvu zao katika ujenzi wa vituo vya afya vitatu, lakini kwa kuhakikisha kwamba vituo hivyo vinaanza kutoa huduma ili kuweza kuboresha huduma za afya katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimetangulia kujibu katika swali la msingi, lakini katika maswali ya nyongeza yaliyofuata ni kwamba hali ya upatikanaji wa dawa katika vituo vyetu imeendelea kuimarika. Hata hivyo, tunafahamu bado kuna changamoto katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika kata hizi ambazo zipo katika Jimbo la Kishapu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la muhimu ambalo Serikali inaendelea kulitekeleza; moja, ni kuhakikisha tunaendelea kupeleka dawa katika vituo hivyo kutoka Bohari Kuu ya Dawa kwa wakati na kuendelea kuboresha bajeti ya dawa katika vituo hivyo kwa kutumia fedha za mapato ya ndani na fedha zinazotoka Serikali Kuu. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Boniphace Butondo kwamba tutaendelea kushirikiana kwa karibu sana kuhakikisha vituo hivi vinapata dawa na vitendanishi vya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba baada ya ujenzi wa vituo vingi vya afya, automatically tunakuwa na upungufu wa watumishi. Hiyo ni hatua moja. Serikali imeanza na hatua ya ujenzi wa Vituo vya Afya, nasi sote ni mashahidi, tumejenga vituo vingi kwa wakati mmoja, lakini tunaendelea na hatua ya pili ya kuajiri watumishi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kuomba kibali cha ajira na kadri watumishi watakavyopatikana, tutahakikisha tunawapeleka katika Vituo hivi vya Afya katika Jimbo la Kishapu na pia katika majimbo mengine kote nchini. (Makofi)

Name

Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Primary Question

MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha ununuzi wa Vifaa Tiba ikiwemo vya upasuaji katika Kituo cha Afya cha Mwabayanda Wilayani Maswa?

Supplementary Question 4

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwanza naipongeza Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya kutujengea Hospitali ya Nyang’wale ambayo imekamilika kwa asilimia 90; lakini majengo hayo ambayo yamekamilika, anayatumia Mkurugenzi kama Ofisi zake na jengo la Halmashauri lipo kwenye asilimia 34:

Je, Serikali ipo tayari kuongeza fedha ili kukamilisha jengo la Halmashauri ili Mkurugenzi aweze kuhama? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Nyang’wale, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, majengo haya ya Hospitali za Halmashauri ambayo yamekamilika kwa asilimia 90 na kuendelea, maelekezo ya Serikali ni kuhakikisha majengo yale yanaanza kutoa huduma za awali za afya katika Hospitali hizo za Halmashauri. Ndiyo maana katika hospitali zote 67 za awamu ya kwanza tayari huduma za awali za OPD zinatolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kuelekeza kwamba Mamlaka za Serikali za Mitaa katika Wilaya ya Nyang’wale ifanye utaratibu wa kuhakikisha huduma za afya katika hospitali hii iliyokamilika kwa asilimia 90 kwa wananchi, angalau kwa kuanza na huduma za OPD. Pili, Serikali katika mpango wa bajeti wa mwaka ujao itatenga zaidi ya shilingi bilioni 34 kwa ajili ya kukamilisha Hospitali zote za Halmashauri 67 ambazo zilianza ujenzi mwaka 2018/2019 ikiwemo Hospitali ya Wilaya ya Nyangh’wale.

Name

Dorothy George Kilave

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Temeke

Primary Question

MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha ununuzi wa Vifaa Tiba ikiwemo vya upasuaji katika Kituo cha Afya cha Mwabayanda Wilayani Maswa?

Supplementary Question 5

MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nawapongeza kwa jinsi ambavyo wameweza kutujengea vituo vya afya viwili; cha Buza pamoja na Malawi na vyote vimemalizika katika Halmashauri yetu ya Temeke. Sasa nauliza:-

Je, vifaa tiba vitaingia lini; kwa sababu sasa ni muda mrefu hatujapata vifaa hivyo? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba vituo vya afya vikiwemo vya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke vimekamilika na kuna changamoto ya vifaa tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha ujao tutakwenda kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha vituo hivi vya afya vinapelekewa vifaa tiba. Katika swali langu la msingi nimesema, katika mwaka huu wa fedha jumla ya shilingi bilioni 26 zimeshatolewa tayari; na shilingi bilioni 15 vifaa tiba vimeshapelekwa kwenye vituo vya afya vilivyojengwa kwenye awamu ya kwanza na ya pili; na shilingi bilioni 11 zipo katika hatua za manunuzi kwa ajili ya kupeleka vifaa tiba katika vituo hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Vituo vya Afya hivi vya Temeke vilijengwa awamu ya tatu na awamu ya nne, kwa hiyo, vitakuwa katika mpango wa bajeti wa mwaka 2021/ 2022. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hilo litaendelea kufanyiwa kazi. (Makofi)