Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Nicodemas Henry Maganga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbogwe

Primary Question

MHE. NICODEMUS H. MAGANGA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka Wilayani Mbogwe maji kutoka Ziwa Victoria kwa ajili ya matumizi ya Wananchi?

Supplementary Question 1

MHE. NICODEMUS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza sijaridhishwa na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji kwamba kuna visima 26 Mbogwe. Naomba tu tuongozane naye akanionyeshe pale vilipo hivyo visima virefu vinavyotoa maji, maana mimi ni Mbunge wa Mbogwe na ninaishi Mbogwe na kuna taabu kubwa sana katika Sekta ya Maji. Ndiyo maana nikaiomba Serikali sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mbogwe ni Wilaya ambayo ipo karibu na mradi wa maji pale Kahama, ni vyema sasa Wizara ya Maji itupelekee mradi mkubwa wa Ziwa Victoria, maana hivyo visima anavyovisema Mheshimiwa, nakuomba twende na wewe, usifuate mambo ya kwenye makaratasi ukajionee na unionyeshe pale vilipo visima.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi/Kicheko)

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ombi lake namba moja limepita, kwani huo ni moto wa namna ya kutekeleza majukumu yangu; nimekuwa nikiambatana na Wabunge wengi, hata weekend hii tu nilikuwa Mbinga. Kwa hiyo, mimi kutembea huko, kwangu ni moja ya majukumu yangu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Nicodemus mantahofu, tutakwenda na miradi hii tutahakikisha mambo yanakaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kupitia mradi wa Ziwa Victoria, hili Ziwa litatumika vyema kwa maeneo yote ambayo miradi hii mikubwa itapitia. Mheshimiwa Nicodemus, wewe ni Mbunge katika Wabunge mahiri, umekuwa ukifatilia suala hili, tumeliongea mara nyingi na umeonyesha uchungu mkubwa kwa wana Mbogwe. Nikuhakikishie, Mbogwe maji yatafika na katika mwaka ujao wa fedha mambo yatakwenda vizuri pale Mbogwe. Tuonane baada ya hapa, tuweke mambo sawa, tuone namna gani tunaelekea. (Makofi/Kicheko)

Name

Venant Daud Protas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Primary Question

MHE. NICODEMUS H. MAGANGA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka Wilayani Mbogwe maji kutoka Ziwa Victoria kwa ajili ya matumizi ya Wananchi?

Supplementary Question 2

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Matatizo ya Jimbo la Mbogwe yanafanana vile vile na matatizo ya Jimbo la Igalula. Tuna Mradi wa Ziwa Victoria katika Jimbo la Igalula, lakini mradi ule mpaka sasa hivi umesimama:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa kupeleka maji katika Kata za Goweko, Igalula, Kigwa na Nsololo ili wananchi waanze kutumia maji ya Ziwa Victoria? (Makofi)

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mradi ambao tayari utekelezaji wake umeanza ni lazima ukamilike. Sisi Wizara ya Maji tunapoanza kazi ni lazima zikamilike. Kwa mradi huu ambao umesimama napenda nikutoe hofu Mheshimiwa Mbunge, tuonane baada ya hapa, lakini vile vile wiki ijayo tutaangalia fungu la kupeleka fedha ili pale kazi iliposimama, utekelezaji uendelee na tutahakikisha mradi huu unaisha ndani ya wakati ili maji yaweze kupatikana Igalula. (Makofi)

Name

Munde Abdallah Tambwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NICODEMUS H. MAGANGA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka Wilayani Mbogwe maji kutoka Ziwa Victoria kwa ajili ya matumizi ya Wananchi?

Supplementary Question 3

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii nami niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa, Mkoa wa Tabora ulifanikiwa kupata maji ya Ziwa Victoria; na kwa kuwa, Mheshimiwa Rais alipokuja kwenye Kampeni alisema kwamba, sasa maji ya Ziwa Victoria yapelekwe Urambo, Kaliua na Ulyankulu:-

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri ni lini sasa mnatarajia kuyatoa maji hayo Tabora Mjini na kuyapeleka Urambo, Kaliua, Ulyankulu pamoja na Sikonge? (Makofi)

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Maeneo ya Urambo, Kaliua, Ulyankulu na Sikonge, yote haya tumeendelea kuyaweka katika mikakati ya Wizara kuona namna ambavyo tutaendelea kupata fedha ili maeneo haya yote maji yaweze kufika. Tutafanya jitihada za makusudi kuona kwamba tunapeleka fedha mapema na hii itakuja kuingia mwaka ujao wa fedha.

Name

Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NICODEMUS H. MAGANGA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka Wilayani Mbogwe maji kutoka Ziwa Victoria kwa ajili ya matumizi ya Wananchi?

Supplementary Question 4

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Naipongeza Serikali kwa usambazaji wa maji ya Lake Victoria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, tatizo lililo katika ukanda huo linafanana kabisa na lile la Rombo na wanawake hawa wamezeeka sasa na kutoka upara kwa ajili ya kubeba maji:-

Ni lini sasa Wizara hii itaona ni wakati muafaka wa kusambaza maji ya Lake Chala kwa wale wananchi wa Rombo katika Mji ule wa Holili, Kata za Mahida, Ngoyoni na tambarare yote ya Rombo?

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Maeneo ya Rombo Mheshimiwa Shally nimeshafika. Nimeacha maagizo ya kutosha na hata miradi ambayo ilikuwa inasuasua pale niliacha maagizo na utekelezaji unaendelea. Nikutoe hofu kwamba nitarudi tena kuhakikisha ule mradi mkubwa tunakwenda kuutekeleza

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana mama yangu, amekuwa ni mfuatiliaji mzuri pamoja na Mbunge Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, wote mmekuwa mkifuatilia kwa jitihada kubwa. Hatutawaangusha. Sisi Wizara hatutakuwa kikwazo kwenu kwa sababu tunahitaji Wana-Rombo waweze na wao kupata ladha ya mageuzi makubwa ambayo yako ndani ya Wizara ya Maji. (Makofi)