Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatatua changamoto ya kujaa maji mara tu mvua zinaponyesha katika baadhi ya maeneo ya Kata za Magomeni, Shangani, Ufukoni, Reli na Likombe katika Manispaa ya Mtwara Mikindani?

Supplementary Question 1

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali imejenga mifereji katika baadhi ya maeneo, lakini mfereji wa kutoa maji kutoka Kata ya Shangani, maeneo ya Kiangu kwenda baharini haufanyi kazi vizuri, maji yanajaa sana kwenye majumba ya watu. Sasa swali langu, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kwenda Mtwara kuuona mfereji ule na kufanya utaratibu wa kuhakikisha mfereji ule unatengenezwa kwa kiwango kizuri ili kusudi wananchi wale wasiweze kupata adha hiyo maji? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, maeneo mengi ambayo yanajaa maji katika Manispaa ya Mtwara Mikindani ni ambayo Serikali imepima viwanja ikawagawia wananchi, siyo kwamba wamevamia. Katika kujaa maji kule kunasababisha uharibifu na wakati mwingine vifo vya wananchi.

Je, Serikali sasa iko tayari kwenda kukaa na wananchi wale waone wanatatua vipi changamoto hizi kwa sababu kadri miaka inavyokwenda tatizo ni kubwa, linaharibu mali na wakati mwingine kugharimu maisha ya wananchi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani? Nakushukuru. (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tunza Malapo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza alilokuwa ameliomba, anaomba sisi kama Ofisi ya Rais – TAMISEMI hususani Waziri kuongozana na Mheshimiwa Mbunge kwenda katika eneo husika kushuhudia anachokieleza. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, niko tayari mara baada ya kupitisha bajeti yetu, nitaongozana naye pamoja na Mbunge wa Jimbo husika kuhakikisha tunaipatia ufumbuzi kero hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili ameuliza kama Serikali ipo tayari kukaa na wananchi, nimhakikishie tutakavyokwenda kule tutakaa na wananchi ili tuweze kupata suluhisho la tatizo hilo. Ahsante.

Name

Agnesta Lambert Kaiza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatatua changamoto ya kujaa maji mara tu mvua zinaponyesha katika baadhi ya maeneo ya Kata za Magomeni, Shangani, Ufukoni, Reli na Likombe katika Manispaa ya Mtwara Mikindani?

Supplementary Question 2

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Changamoto ya kujaa kwa maji yanayotokana na mvua iliyoko Mkoa wa Mtwara haina tofauti kabisa na changamoto iliyopo Mkoa wa Dar es Salaam hususan eneo la Jangwani. Kujaa kwa maji katika eneo la Jangwani imekuwa ni changamoto ya muda mrefu na haijawahi kupatiwa tiba ya kutosha. (Makofi)

Mhesimiwa Spika, swali langu ni kwamba, je, Serikali ina mkakati gani au inatueleza nini kuhusiana na changamoto hii ya kujaa maji pale Jangwani hasa ikizingatiwa kwamba Jangwani ni kiunganishi kikubwa sana cha wafanyabiashara wanaoelekea Kariakoo eneo ambao limebeba uchumi mkubwa sana wa nchi? Naomba Serikali basi itoe majibu ni lini itaweza kukomesha changamoto hii ya kujaa maji Jangwani. Ahsante sana. (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Agnesta Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge amejaribu kuoanisha eneo la Jangwani na maeneo yaliyoko kule Mtwara katika Manispaa ya Mikindani kwamba na lenyewe linajaa sana maji na anataka kufahamu mkakati gani ambao Serikali inao kuhakikisha tunatatua tatizo katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, cha kwanza nimhakikishie kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI tuna mradi mkubwa wa DMDP ambao unajenga miundombinu katika Jiji la Dar es Salaam. Sehemu ya miundombinu hiyo ambayo tumekuwa tukiijenga ni pamoja na mifereji mikubwa ambayo imekuwa ikihamisha maji kutoka katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na kupeleka baharini.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili, sasa hivi tuna Mradi mkubwa wa Mabasi Yaendayo Kasi na moja ya jukumu lao kubwa ni kuhakikisha lile eneo la Jangwani linapandishwa tuta kubwa ambalo litahakikisha ile kero ambayo inawapata wananchi inaondolewa. Kwa hiyo, nimhakikishie kabisa Serikali ipo kazini na ile kazi itakamilika na wananchi wa Jiji la Dar es Salaam hawatajutia kuichagua Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Ahsante. (Makofi)