Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Vita Rashid Kawawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Primary Question

MHE. VITA R. KAWAWA Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kusambaza umeme wa REA kwenye baadhi ya vitongoji vya vijiji vya Namtumbo?

Supplementary Question 1

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwanza naomba niipongeze Serikali Kuu kwa kazi nzuri inayoifanya ya kutusambazia umeme. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wananchi wa Namtumbo nyumba zao na taasisi wamefanyakazi yao nzuri ya wiring, lakini wanacheleweshewa kuunganishiwa umeme hususan kijiji cha Mbimbi na Taasisi ya Hunger Seminary na Shule ya Sekondari ya Msindo.

Je, Serikali inaweza kuielekeza TANESCO waharakishe uunganishwaji wa umeme katika vijiji na taasisi hizo?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mazingira ya Namtumbo maeneo mengi yana mchwa na yanasumbua sana nguzo za umeme zisizokuwa treated vizuri. Je, Serikali inaweza kuelekeza namna bora ya ku-treat nguzo zinazowekwa au kuwekwa nguzo rafiki na mazingira ya mchwa ya Namtumbo na kwingineko ili kuepuka hasara inayoweza kujitokeza katika mradi huu?

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Namtumbo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Namtumbo ni mojawapo ya Wilaya ambazo zilikuwa zinapelekewa umeme katika awamu ya tatu mzunguko wa kwanza wa REA. Kilichotokea ni kwamba baada ya kufanyika kwa kazi ya awali wakandarasi waliowengi waliongezewa kazi za nyongeza katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuwafikia wananchi walio wengi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Namtumbo imekuwa ni mojawapo kati ya maeneo ambayo yameongezewa maeneo ya nyongeza na hivyo kushindwa kukamilisha kazi iliyopangwa kwa wakati. Mkandarasi ambaye alikuwa anafanyakazi katika Mkoa wa Ruvuma NAMIS Cooperate ameongezewa muda wa kukamilisha kazi katika mkoa huo mpaka kufikia mwezi Aprili na katika Wilaya ya Namtumbo tayari ile kazi iliyokuwa imeongezeka nguzo zimesimikwa, waya zimepelekwa na kilichobaki sasa ni upatikanaji wa mita kuweza kuwafikishia huduma wale wote waliopelekewa umeme. (Makofi)

Kwa hiyo, nimuahidi Mheshimiwa Vita kwamba ifikapo mwezi Aprili tayari wale wote waliounganishiwa umeme watakuwa wamewashiwa umeme katika maeneo yao bila kuchelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili alitaka kujua uwezekano wa kuweka miundombinu itakayokuwa rafiki na ya uhakika katika maeneo ambayo tayari yana matatizo mbalimbali. Tunafahamu na sasa ni maelekezo ya Wizara kwamba katika yale maeneo ambayo oevu kwa maana ni maeneo yenye majimaji, katika maeneo ya hifadhi na katika maeneo yenye matatizo mengine na changamoto kama hizo za miti kuliwa na mchwa tumeelekeza kwamba wenzetu wa TANESCO na REA basi watumie nguzo za zege zinaitwa concrete polls ili kuhakikisha kwamba tukiziweka basi zinakuwa za kudumu na zinakaa kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niongezee kwamba kwa sababu Waheshimiwa Wabunge wanayafahamu maeneo yao yana matatizo gani, basi maelekezo ya Wizara ni kwamba wale wakandarasi watakaoenda kufanyakazi katika Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili wa REA wahakikishe wanawasiliana pamoja na mamlaka nyingine watakazoziona kwa maana ya TANESCO kupeleka …. kwa Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya lakini pia wafanye consultation kwa Waheshimiwa Wabunge ili waweze kutoa maoni yao na ushauri wao maeneo gani yanaweza yakafanyiwa nini hata kama siyo ya kitaalam lakini yakichanganywa na ya kitaalam yatatusaidia kuhakikisha miundombinu yetu inadumu katika maeneo husika. (Makofi)

Name

Francis Isack Mtinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Primary Question

MHE. VITA R. KAWAWA Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kusambaza umeme wa REA kwenye baadhi ya vitongoji vya vijiji vya Namtumbo?

Supplementary Question 2

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona naomba niulize swali moja la nyongeza.

Kwa kuwa changamoto zilizoko Namtumbo zinafanana kabisa na changamoto zilizoko Mkalama hasa Kata ya Mwanga ambayo haikuwahi kupata umeme kabisa katika awamu zote. Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu kata hii ambayo imekuwa ikiutizama tu umeme huu wa REA katika kata nyingine?

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Mkalama kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika,kama tulivyokwishasema kwamba katika Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili wa REA, tutapeleka umeme katika vijiji vyote Tanzania vilivyobaki bila kupata umeme ambavyo hesabu yake ilikuwa ni 2,150. Kazi hiyo itaanza mwezi huu wa pili na tunahakikisha kwamba kufika mwezi Septemba, 2022 vijiji vyote vilivyopo nchini Tanzania vitakuwa vimepata umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongezee kwamba tunapopeleka umeme vijijini, kimsingi tunapeleka kwenye Mkoa, Wilaya, Kata, vijiji halafu Vitongoji. Kwa hiyo, kuna vitongoji ambavyo pia vitanufaika na awamu ya tatu, mzunguko wa pili wa upelekaji wa umeme kwenye mradi huo ambao utaanza mwezi huu na kukamilika kufikia mwezi Septemba, 2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge wa Mkalama kwamba vijiji hivyo vilivyopo katika kata hiyo, vitapatiwa umeme kwa uhakika.

Name

Mwanaisha Ng'anzi Ulenge

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. VITA R. KAWAWA Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kusambaza umeme wa REA kwenye baadhi ya vitongoji vya vijiji vya Namtumbo?

Supplementary Question 3

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu Serikali inatekeleza Mpango wa peri-urban kuhakikisha vijiji vilivyopo ndani ya majiji navyo vinapatiwa umeme. Naomba kujua ni lini Serikali itaweka wazi ratiba yake ili na vijiji vilivyopo ndani ya Jiji la Tanga vitapelekewa umeme huo wa REA? Nashukuru. (Makofi)

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwanaisha, Mbunge wa Tanga kwa kueleza kwanza kidogo kwamba Serikali yetu kupitia maelekezo yanayotolewa na Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, imekuwa ikipeleka umeme katika maeneo mbalimbali kwa taratibu tofauti tofauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunao Wakala wa Umeme TANESCO ambao una jukumu na wajibu wa kuhakikisha wanapeleka umeme katika maeneo yote ya mjini na vijijini kwa maana ya kwamba ile miradi inayowekwa katika mazingira fulani, ikishakamilika, basi TANESCO wanaendelea kupeleka umeme katika maeneo hayo. Hata hivyo, tumekuwa na hizo REA I, REA II na REA III; pia tumekuwa na kitu kinaitwa densification (Mradi wa Umeme Jazilizi); vile vile iko hiyo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameisema ya peri- urban ambao ni mradi unaopeleka umeme katika maeneo ya mijini lakini yenye asili au uonekano wa vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa peri-urban ulianza kwa kupeleka umeme katika Majiji ya Arusha, Mwanza, Dar es Salaam, Mbeya na Dodoma na awamu ya kwanza imeelekea kukamilika, itakamilika mwezi wa nne mwaka huu na baada ya hapo sasa tutaingia katika awamu ya pili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba awamu ya pili itakapoanza basi Waheshimiwa Wabunge wote watafahamishwa na wale wote ambao ni wanufaika watapata nafasi hiyo. Pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo ya peri- urban bado yanapelekewa umeme na Wakala wa Umeme TANESCO kwa kuzingatia kwamba ni jukumu lake kuhakikisha kwamba anapeleka umeme katika mazingira yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa Mbunge kuwa taarifa itapatikana na ratiba kamili itafahamika. (Makofi)

Name

Jackson Gedion Kiswaga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Primary Question

MHE. VITA R. KAWAWA Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kusambaza umeme wa REA kwenye baadhi ya vitongoji vya vijiji vya Namtumbo?

Supplementary Question 4

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa nafasi.

Kwa kuwa wananchi wa Jimbo la Kalenga hasa Vijiji vya Wangama, Lupembelwasenga pamoja na Welu kwa kutaja tu vichache tayari walishaunganisha umeme, walishalipia na walishafanya wiring lakini hawajawashiwa umeme mpaka sasa.

Je, Serikali inatoa kauli gani ili wananchi hao waweze kuwashiwa umeme wao? (Makofi)

Name

Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Answer

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri katika maswali ya nyongeza. Vilevile nawapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa kuuliza maswali ya msingi sana katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wateja wote ambao wameshafanya malipo na wanasubiri kuunganishiwa umeme pamoja na wateja wote ambao wameshafanyiwa survey, lakini wanasubiri kuunganishiwa umeme, tumetoa muda wa miezi mitatu wateja wote wawe wameshaunganishiwa umeme nchi nzima. Kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Mbunge wa Kalenga kwa kuuliza swali hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ili kuharakisha shughuli za kuwaunganishia umeme wateja nchi nzima, tumebadilisha mpango wa wataalam wetu kusubiri magari, badala yake TANESCO itawanunulia magari ma-surveyor wote na ma-technician ili wawahi kuwaunganishia umeme wananchi, ndani ya muda uliokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongeze kidogo kuhusiana na suala la maeneo ambayo ni ya mijini; kulingana na swali ninalojibu ambalo Naibu Waziri amejibu vizuri, lakini niongezee kidogo. Iko mitaa mingi ambayo iko karibu na miji na vijijini hasa katika maeneo ambayo ni ya Majiji na Manispaa, likiwemo Jiji la Mbeya, Iringa, Mwanza, Dodoma hapa, mradi wa peri-urban unaendelea na miradi yote katika mitaa 122 itapelekewa umeme ndani ya miezi sita ijayo. Ahsante sana. (Makofi)