Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Augustine Vuma Holle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Vijijini

Primary Question

MHE. VUMA A. HOLLE Aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua mgogoro wa ardhi kati ya Kijiji cha Mgombe na Kambi ya Jeshi Mtabila?

Supplementary Question 1

MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Waziri, naomba kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa inafahamika wazi kwamba baada ya Kambi ya Wakimbizi kuondoka, Serikali ilifanya expansion, yaani iliongeza mipaka ya Kambi ile ikamega Vijiji vya Katonga, Mgombe, Nyamusanzu na Buhoro bila kufuata taratibu. Bahati mbaya wakawa wamekabidhiwa Jeshi; na kumekuwepo na jitihada za Ofisi ya Mkuu wa Wilaya wakishirikiana na Jeshi kutaka kuwarudishia wananchi maeneo. Sema walitaka kuwarudishia kipande kidogo, wananchi wakawa wamegoma.

Je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kufanya jambo hili kwa haraka ili wananchi wale waweze kupata haki yao ya mashamba hayo ambayo yamechukuliwa kwa muda mrefu, aidha kwa fidia ya maeneo au fidia ya fedha? (Makofi)

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vuma kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza uniruhusu nimpongeze tu Mheshimiwa Vuma, kwa juhudi zake anazozifanya kuhakikisha kwamba mgogoro ambao ulijitokeza tunaweza kuumaliza. Nampongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wafahamu kwamba Jeshi ni la kwao. Hili ni Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Watambue kwamba uwepo wa Jeshi ni kwa manufaa yetu sote. Kwa hiyo, tumekuwa na maeneo makubwa katika maeneo yetu, lakini lengo lake ni kuhakikisha kwamba maeneo hayo yanatumika kwa ajili ya shughuli za Jeshi na vifaa vya Jeshi. Kwa hiyo, wananchi wakitambua hivyo, nawaomba tu wawe na ushirikiano. Nafahamu ipo migogoro kadhaa lakini nafahamu pia juhudi imefanyika kuhakikisha migogoro mingi tumeweza kuimaliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namhakikisha Mheshimiwa Vuma kwamba suala la kumaliza mgogoro tunamaliza kwa kuwa kuna hatua nzuri tumezifikia. Vikao vya awali kama nilivyosema, vimeshafanyika, lakini sasa vikao ambavyo vitakuja kuendelezwa ni kuhakikisha kwamba tunamaliza mgogoro huu. Zipo Sheria za Ardhi na Sheria za Vijiji zitatumika ili kuhakikisha wananchi hawa wanapata haki zao.

Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, lakini naomba tuendelee kushirikiana; na wananchi wavute subira, tuko kwenye hatua nzuri ya kumaliza mgogoro huu. (Makofi)

Name

George Ranwell Mwenisongole

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbozi

Primary Question

MHE. VUMA A. HOLLE Aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua mgogoro wa ardhi kati ya Kijiji cha Mgombe na Kambi ya Jeshi Mtabila?

Supplementary Question 2

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza. Matatizo yaliyoko Kasulu Vijijini yanafanana na matatizo yaliyoko kwenye Jimbo langu la Mbozi katika Kijiji cha Sasenga na Itewe, kuna mgogoro kati ya wananchi na Kambi ya Jeshi. Napenda kumuuliza Waziri wa Ulinzi. Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua huo mgogoro ambao umekuwa ni wa muda mrefu kati ya hivyo vijiji na Kambi ya Jeshi 845KJ. (Makofi)

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwenisongole kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu kwamba katika Kambi ya Itaka kuna shida hiyo ya mgogoro. Niseme kwamba migogoro hii imesababishwa na mambo mengi ikiwemo lile suala tu la uzalendo, majeshi yetu, pale ambapo tulikuwa tunawaruhusu wananchi kufanya shughuli zao; na walipozoea kufanya shughuli zao wakaamua kuhamia katika maeneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, kwamba tunafanya utaratibu maeneo yote na tumeshatambua maeneo yote yenye mgogoro na kwa hiyo, tumejipanga kwa ajili ya kuitatua. Tumeanzisha kitengo maalum cha miliki kuhakikisha kwamba migogoro yote tunaimaliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Mwenisongole kwamba tunafahamu shida ya Itaka na kuna hatua zinachukuliwa, tunakwenda kutatua shida ambayo iko kwa wananchi. Vilevile nawasihi sana wanasiasa na viongozi mbalimbali, kwamba kuna wakati mwingine tumetafuta kura Waheshimiwa Wabunge tukiahidi kwamba tutawasaidia wananchi kupata maeneo ambayo ni ya Jeshi. Niwahakikishie tu kwamba tutafuata taratibu kuhakikisha kwamba haki inatendeka, wananchi wanapata haki zao na Jeshi linaendelea kufanya shughuli zake bila kikwazo chochote. (Makofi)

Name

Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Primary Question

MHE. VUMA A. HOLLE Aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua mgogoro wa ardhi kati ya Kijiji cha Mgombe na Kambi ya Jeshi Mtabila?

Supplementary Question 3

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Matatizo yaliyojitokeza huko Kigoma, ndiyo hali ilivyo katika eneo la Kampuni Mpanda Mjini.

Je, ni lini Serikali itakuja kutatua mgogoro wa wananchi na Jeshi katika eneo la Kampuni?

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu la nyongeza la Mheshimiwa Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua mgogoro uliopo na nikipongeze Chama Cha Mapinduzi kwa sababu mlezi wa Chama katika Mkoa ameliwasilisha suala hili mezani kwangu na mimi nimeshachukua hatua. Nimetoa maelekezo ili uchambuzi wa kina juu ya mgogoro huu niupate.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Kapufu asiwe na wasiwasi na tutakwenda kwa kasi kubwa kuhakikisha kwamba wananchi katika Jimbo hili la Mpanda wanakaa vizuri, waendelee na shughuli zao na Jeshi nalo liendelee na shughuli zake. Kwa hiyo, taratibu zinaenda vizuri Mheshimiwa Kapufu naomba avute Subira tu kidogo.

Name

Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. VUMA A. HOLLE Aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua mgogoro wa ardhi kati ya Kijiji cha Mgombe na Kambi ya Jeshi Mtabila?

Supplementary Question 4

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Wananchi wa Mtaa wa Kenyambi na Bugosi katika Mji wa Tarime wana mgogoro wa muda mrefu na Jeshi la Wananchi na Serikali imeshafikia hatua nzuri tu ya kufanya tathmini na ikarudia tena kufanya tathmini bado imebakiza malipo. Napenda kujua ni lini wananchi wale wataenda kulipwa fidia yao ili waweze kuondoka maeneo yale na kuwaachia Jeshi la Wananchi wa Tanzania? (Makofi)

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Matiko, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru kwa kutambua kwamba tunaendelea kuwajali wananchi wetu wa Tanzania na niseme tu kwamba migogoro hii ilikuwepo kadhaa lakini niseme kwamba kati ya migogoro hiyo, zaidi ya asilimia 50 ya migogoro tumeshaitatua. Yako maeneo ambayo tumeyatambua kwa ajili ya fidia na wananchi wameshalipwa, yapo maeneo mengi ambayo tayari tumeshalipa. Hii inaonesha tunao mwendelezo mzuri wa kuendelea kulipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wananchi hawa wa Tarime wavute subira kwa sababu tunatafuta fedha. Tukipata fedha kwa maeneo yote ambayo tumeyatambua yanahitaji fidia kwa wananchi wetu tutakwenda kuwafanyia malipo. Kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Mbunge kuvuta Subira na wakati mwingine tunaweza tukaonana ili nimueleze kwa kinagaubaga namna tunavyokwenda kutatua matatizo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Kicheko)