Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 2 Sitting 7 Defence and National Service Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga taifa 94 2021-02-10

Name

Augustine Vuma Holle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Vijijini

Primary Question

MHE. VUMA A. HOLLE Aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua mgogoro wa ardhi kati ya Kijiji cha Mgombe na Kambi ya Jeshi Mtabila?

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijajibu swali, kwa ruhusa yako naomba nimshukuru Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama hapa mbele ya Bunge lako. Vile vile namshukuru sana Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na Amirijeshi Mkuu wa Majeshi yetu kwa kuniamini na kuniteua kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Ushetu, wapiga kura wangu kwa kuniamini na kunipitisha bila kupingwa na kwa kura nyingi ambazo walizitoa kwa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakupongeza wewe pamoja na Spika kwa ushindi mkubwa na kuaminiwa na Bunge hili. Vile vile nawapongeza Wabunge wote kwa kuchaguliwa na wananchi kuwa Wabunge wa Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa napenda kujibu swali la Mheshimiwa August Vuma Holle, Mbunge wa Kasulu Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kambi ya Jeshi ya Mtabila – 825/KJ ipo Wilayani Kasulu, Mkoani Kigoma. Eneo husika lina ukubwa wa ekari 12,206.05 ambalo awali lilitumiwa kama Kambi ya wakimbizi. Aidha, mwaka 2012 eneo hili lilikabidhiwa kwa Jeshi na kuwa Kiteule na mwaka 2014 kiliundwa Kikosi cha Jeshi Mtabila.

Mheshimiwa Naibu Spika, mgogoro wa ardhi ulianza baada ya wananchi wa Vijiji vya Mgombe na Katonga kuvamia eneo hilo kwa shughuli za kilimo na hatimaye kuweka makazi. Kwa sasa wananchi waliokuwa wamevamia eneo hilo wameondolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imeanza kuutatua mgogoro uliopo kwa kufanya vikao na uongozi wa Wilaya. Tarehe 11 na 12 Januari, 2021 Viongozi wa Kikosi cha Jeshi Mtabila walikutana na Uongozi wa Wilaya ya Kasulu na kuamua kuihamisha barabara inayokuwa inapita katikati ya kambi kuelekea Kijiji cha Shunga hadi Nchi ya Burundi ipite mpakani mwa eneo la Kambi. Pia, TANROADS wameweka alama za barabara tarehe 13 Januari, 2021 ikiwa ni hatua ya kuitambua barabara hiyo na kuiendeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu itatuma timu ya wataalam kukutana na uongozi wa Mkoa, Wilaya na Vijiji husika kwa lengo la kutatua mgogoro huo. Nawaomba wananchi wawe na subira wakati Serikali inalifanyia kazi suala hili na kulipatia ufumbuzi. Aidha, Wizara inawasihi Viongozi wa ngazi zote kuwaelimisha na kuwasisitiza wananchi katika maeneo yao kutovamia maeneo ya Jeshi. (Makofi)