Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Masache Njelu Kasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Primary Question

MHE. MASACHE N. KASAKA Aliuliza:- Je, ni lini ujenzi wa mradi mkubwa wa maji Chunya Mjini na kata za jirani utaanza kutekelezwa?

Supplementary Question 1

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini pia naishukuru Serikali kwa kuweza kutekeleza Mradi wa Maji kwa Mji wa Chunya uliogharimu zaidi ya milioni 900 lakini mradi huu mpaka sasa hivi haujaweza kuwanufaisha wananchi wa Wilaya ya Chunya na hata kiwango cha upatikanaji wa maji bado kiko chini ya asilimia 30. Tatizo kubwa tukiuliza tunaambiwa mara umeme unakuwa ni mdogo, mara maji ni machache. Sasa Serikali itueleze, je, tatizo ni nini mpaka mradi huu uliotumia fedha nyingi za Serikali haujaweza kuwanufaisha watu wa Chunya?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwenye mradi mkubwa wa maji wa bwawa la Matwiga design ya mwanzo ilikuwa inasema itanufaisha vijiji 16, lakini kwenye review ilivyokuja utekelezaji wake ni vijiji nane. Je, Serikali haioni haja sasa kuweza kurudisha hii design ya mwanzo kurudisha vijiji 16 ili wananchi wa Tarafa ya Kipendao waweze kunufaika na mradi huu wa maji? Ahsante.

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Masache Kasaka kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nia na lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wote wanapata maji safi na salama na ya kutosheleza. Niseme tu msimamo wa Serikali ni kuona kwamba miradi iliyokamilika na matunda yale ya mwisho maji bombani yanapatikana. Kwa mradi huu wa Chunya Mjini nipende tu kusema kwamba Mheshimiwa Mbunge nilifika Chunya na tulitembea pamoja, mradi ule umekamilika tatizo ni hili la umeme ambalo linaendelea kushughulikiwa ili liweze ku-support ile pump maji yaweze kwenda ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa swali la Bwawa la Matwiga, niseme kwamba, katika miradi ambayo ilichukua muda mrefu kutekelezwa ni pamoja na huu, lakini kwa nia njema ya Serikali hii na mkakati mkubwa wa Wizara chini ya usimamizi wa Mheshimiwa Waziri mradi ule sasa hivi unatekelezwa vizuri na mimi pamoja na Mheshimiwa Mbunge tulifika pale tukiongozana na Mtendaji Mkuu wa RUWASA kwa maana ya Director General. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, yale maji ambayo tuliyaona pale kwa pamoja kwenye kile chanzo hayatatoa tu kwa vijiji vile nane, tayari kama Wizara tumekubaliana tutakuja kutoa maji katika vijiji vyote 16.

Name

Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Primary Question

MHE. MASACHE N. KASAKA Aliuliza:- Je, ni lini ujenzi wa mradi mkubwa wa maji Chunya Mjini na kata za jirani utaanza kutekelezwa?

Supplementary Question 2

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa Mradi wa Maji Chunya unafanana na ule mradi wa 2F2B pale Tegeta A, ujazo wa lita milioni sita. Je, Wizara inaweza ikatuambia ni lini mradi ule utakamilika ili uweze kusaidia wananchi wote wa Goba?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ule mradi wa tanki Mshikamano kwa ajili ya wananchi wa Mpiji Magohe, Makabe yote na Msakuzi.

Je, ni lini pia mradi huo utakamilika ili wananchi wapate maji salama?

SPIKA: Swali sio lako, kwa hiyo unapaswa kuuliza swali moja tu, sasa chagua mojawapo katika hayo ya kwako.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Niweze kufahamu mradi unaotaka kujengwa mshikamano kwa ajili ya wananchi wa Mbezi, Makabe na Mpiji Magohe utakamilika lini?

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Mtemvu kutoka Kibamba kama ifuatavyo:-.

Mheshimiwa Spika, Wizara sasa hivi inapitia miradi hii yote ambayo usanifu wake ulikamilika. Kwa hiyo nipende tu kumwambia Mheshimiwa Mbunge huo mradi upo katika miradi ambayo inakwenda kutekelezwa awamu hii kabla mwaka huu wa fedha haujaisha.