Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mrisho Mashaka Gambo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arusha Mjini

Primary Question

MHE. MRISHO M. GAMBO Aliuliza: - Serikali imeongeza viwango vya tozo za utalii kwa Hifadhi zilizo chini ya TANAPA kuanzia mwezi Julai, 2021. Je, Serikali haioni umuhimu wa kusitisha tozo hizo ili kutoa fursa kwa Sekta ya Utalii nchini ambayo imeathirika sana na ugonjwa wa Corona?

Supplementary Question 1

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, naomba niweke wazi tu kwanza kwamba sijaridhika na majibu ya Mheshimiwa Waziri na Wizara kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla wake sekta ya utalii kwa Mkoa wa Arusha na nchi nzima imeathirika sana. Wananchi wengi sana wamekosa ajira, madereva wamekosa ajira kwa sababu magari hayatembei kutokana na uchache wa watalii, guides wamekosa ajira, wafanyakazi wa mahoteli wamepunguzwa kwenye maeneo yao, magari ambayo yangetembea, yangeweka mafuta shell zingeweza kufanya biashara zao.

Mheshimiwa Spika, tukiangalia kwenye ukanda wa Afrika Mashariki, karibu nchi nyingi zimeweza kupunguza tozo kipindi hiki. Mfano, Kenya, Nairobi National Park wamepunguza tozo kutoka Dola 43,000 mpaka 35,000. Ukienda Rwanda kwenye masuala ya gorilla wamepunguza kutoka Dola 1,500 mpaka Dola 500. Ukienda Uganda kwenye masuala pia ya gorilla wamepunguza kutoka Dola 700 mpaka 500. Naomba Wizara ya Maliasili na Utalii iangalie athari za ugonjwa wa Corona kwenye masuala ya ajira na masuala mengine.

Mheshimiwa Spika, swali langu la nyongeza, Wizara ya Maliasili na Utalii ina mpango gani wa kuipa ahueni sekta ya utalii ili kuweza kunusuru changamoto kubwa ya ajira ambayo imewaathiri wananchi wa Mkoa wa Arusha pamoja na Tanzania kwa ujumla?

Name

Dr. Advocate Damas Daniel Ndumbaro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Songea Mjini

Answer

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo Mheshimiwa Gambo ametoa takwimu, wenzetu wamepunguza kutoka Dola 1,500 mpaka 1,000, kutoka Dola 700 mpaka 500; hizo ndiyo takwimu zake. Viwango vya kuingia katika hifadhi zetu bado viko chini sana ukilinganisha na ubora wa hifadhi tulizonazo. Ukisema Serengeti hulinganishi na hifadhi yoyote iliyoko katika Afrika Mashariki; kule Rwanda unaona gorilla tu. Serengeti is a jewel, bado ni Dola 60. Kwa hiyo, viwango bado viko chini sana. Nilitaka kwanza hilo niliweke sawa.

Mheshimiwa Spika, la pili, Serikali inatoa tahafifu gani hasa kwa kipindi hiki? Wizara imegawa suala la utalii katika misimu miwili; high season na low season. Ongezeko hilo ambalo tunalisema litagusa kwenye high season tu; low season bado rates zitabaki pale pale.

Mheshimiwa Spika, hii ni kwa nini? Katika high season, sehemu kama Ngorongoro kwa siku moja yanaingia magari 400 ambayo yanaathari kubwa kiikolojia wakati kwenye low season yanaingia magari 70. Tunataka tu-balance sasa, hawa wafanyabiashara wetu ambao tutawapa tahafifu, waende sasa kwenye low season ili tutunze pia na ikolojia iliyopo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, AJIRA, KAZI, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, pamoja na kuunga mkono majibu mazuri yaliyotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii, lakini swali la msingi na maswali ya nyongeza yamegusa pia sekta ya ajira katika sekta hiyo ya maliasili.

Mheshimiwa Spika, naomba kuliambia Bunge lako Tukufu, wakati wa Covid, hata sasa na hata baadaye, kama kunatokea tatizo lolote linalohusiana na suala la wafanyakazi, tunaomba wafanyakazi, waajiri watumie platform yao ambayo ni ya dhana ya utatu ambayo tumekuwa tukiitumia mara nyingi kuamsha mijadala na kutafuta solution katika mazingira ya mawanda hayo ya sekta ya kazi, ajira na Serikali. Kwa hiyo, nawashauri watumie platform hiyo.