Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:- Je Serikali inatumia sheria gani kuwahamisha wakulima kwenye maeneo ya mijini?

Supplementary Question 1

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, je, ni kwa nini miji inapopanuliwa maeneo ya mashamba ya mazao marefu yasiachwe mijini kama ilivyo katika nchi nyingine kama Malaysia ambapo kilimo cha michikichi na mazao mengine kinaendeshwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, sheria hiyo haihusishi baadhi ya Mikoa kama Kagera, Kilimanjaro na Arusha ambako wakulima wanaendelea kulima mijini mazao marefu?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kama nilivyotoa majibu ya swali la msingi, Serikali huwahamisha wakulima wa mazao ya aina zote kwenye maeneo ya mijini yaliyoiva kwa ajili ya ukuaji au uendelezaji wa miji kwa kuzingatia Sheria ya Mipango Miji, Na. 8 ya 2007 (Kifungu cha 7 na Kifungu cha 28 na Kanuni zake za mwaka 2008. Sheria hii hutumika kwa pamoja na Sheria ya Utwaaji wa Ardhi, Na. 47 ya 1967; Sheria ya Ardhi, Na. 4 ya 1999 na Sheria ya Upimaji na Ramani, Sura ya 324 ya mwaka 2002.

Mheshimiwa Spika, hivyo, sheria za nchi yetu zinazohusika na usimamizi wa uendelezaji wa miji haziruhusu uwepo wa mashamba ya mazao marefu mijini isipokuwa sheria hizo zinaruhusu kilimo cha mijini (urban farming) cha mazao mafupi yasiyozidi urefu wa mita moja hususan kilimo cha mboga mboga.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, sheria tajwa katika majibu niliyoyatoa katika swali la kwanza la nyongeza hapo juu zinatumika katika maeneo yote ya nchi yetu ya Tanzania na hivyo sheria hizi hazitumiki kwa kubagua baadhi ya mikoa fulani ya Tanzania. Sehemu kubwa ya mazao marefu yanayolimwa katika Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Kagera ambayo ni kahawa, migomba na miparachichi yana sifa ya kuhifadhi mazingira na kupendezesha mandhari ya miji na makazi kama ilivyo kwa miti ya vivuli na matunda.