Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Primary Question

MHE. DEO K. SANGA aliuliza:- Mradi wa Maji wa Bwawani umekuwa ukisuasua kujengwa ikiwemo kuzungushiwa uzio:- Je, ni lini mradi huo utakamilika?

Supplementary Question 1

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili. La kwanza, pamoja na mradi huu kutoa maji katika Mji wa Makambako, bado haijakamilika ikiwepo pamoja na kujenga tenki la lita laki 5 ambalo lilikuwepo kwenye mradi, huo uzio wa eneo la chanzo cha maji pamoja na kukamilisha ofisi ya mamlaka ambayo ilikuwa ndani ya huo mradi. Je, ni lini sasa vitu vyote vitatu vitakamilika? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa kuwa Serikali imetupatia fedha za mkopo nafuu kutoka India kwa ajili ya miradi ile 28 ikiwepo na Makambako, naishukuru sana Serikali, wataalam walishakuja katika Mji wa Makambako wakatembelea na mradi ule umelenga kuhudumia kata tisa ikiwepo Lyamkena na mwisho mpaka Mlowa. Je, ni lini sasa mradi huo utaanza ili wananchi wa Makambako waweze kunufaika na mradi huo?

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, kwanza nimpongeze sana Mbunge, mzee wangu Mheshimiwa Deo Sanga lakini ni Mbunge mfuatiliaji; siyo mara moja au mara mbili amekuwa akija katika ofisi yetu katika kuhakikisha wananchi wake wa Makambako wanapata huduma hii muhimu hasa ya maji. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi ule sasa hivi umefikia asilimia 60 ya utekelezaji, nasi tumekuwa wafuatiliaji wa karibu sana katika kuhakikisha Mji ule wa Makambako unapata huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie na tumwagize Mkandarasi aongeze nguvu, nasi kama Wizara hatutokuwa kikwazo katika kudai certificate na kumlipa kwa wakati katika kuhakikisha mradi ule haukwami na ukamilike kama ulivyopangwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala zima la utekelezaji wa mradi wa miji 28, nitumie nafasi hii binafsi nimpongeze Mheshimiwa Waziri wangu lakini pia nimpongeze Katibu Mkuu na wataalam wetu kwa jitihada kubwa zilizofanyika katika kuhakikisha mradi huu unaanza mara moja kwa miji zaidi ya 28 Bara na mradi mmoja utakuwa Zanzibar katika kuhakikisha kwamba tunatatua tatizo la maji nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa ninalotaka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, wataalam washauri walishapita huko katika maeneo. Kikubwa katika mpango wetu ni kuhakikisha kwamba mnapofika mwezi wa Tisa Wakandarasi wawepo katika maeneo yote kwa ajili ya utekelezaji wa miradi. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, ndani ya mwezi wa Tisa Wakandarasi watakuwa site na utekelezaji utakuwepo, ila la muhimu tunaomba ushirikiano katika kuhakikisha tunashirikiana ili tuweze kutatua tatizo hilo.